Na John Gagarini, Kibaha
KAMPUNI ya Equator Suma Jkt inatarajia kuanza
kuunganisha magari ya zimamoto na matrekata mwishoni mwa mwaka huu ikiwa ni
moja ya njia ya kukabiliana na majanga ya moto pamoja na kuinua kilimo cha Tanzania
ambacho ni uti wa mgongo wa uchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari ambao
walitembelea kiwanda hicho kilichopo Ruvu Mlandizi wilayani Kibaha mkurugenzi
Robert Mangazeni alisema kuwa kwa sasa kiwanda hicho kiko kwenye hatua za
mwishi ikiwa ni pamoja na uunganishaji wa mitambo na mashine.
Mangazeni alisema kuwa teknolojia ya uunganishaji
wa magari ya zimamoto ambapo watatumia magari ya kawaida kwa kuyabadilisha na
kuwa ya zimamoto wameitoa nchi ya Urusi kutoka kwenye makampuni ya St Auto na
Ural huku ile ya matekta wakiitoa kwenye kampuni za Escort kutoka nchini India
na Farmtrac kutoka nchini Poland.
“Tukizungumzia kuhusu uunganishaji wa magari ya
zimamoto ni teknolojia ambayo imeboreshwa na kuwa ya kisasa zaidi ambapo
tutakuwa na uwezo wa kuunganisha magari ya aina mbalimbali kutegemeana na mteja
anavyotaka ambayo yatakuwa na ujazo wa aina tofauti tofauti kuanzia magari
makubwa hadi madogo siyo lazima yawe makubwa kama tulivyozoea hivyo hata
majanga haya ambayo yamezikumba shule sasa taasisi zitaweza kudhibiti moto,”
alisema Mangazeni.
Alisema kuwa ujazo huo utaanzia lita za maji 300
hadi 10,000 kutegemea na ukubwa hivyo kulinagana na miuondombinu ya barabara za
mitaani wataunganisha hata magari madogo ili yaweze kufika kwenye eneo
lililopata maafa ya moto.
“Ikumbukwe Tanzania itakuwa nchi ya pili kuwa na
teknolojia hii ya uunganishaji wa magari ya zimamoto baada ya Afrika Kusini
ambapo kwa nchi za Maziwa Makuu itakuwa ni ya kwanza na itaweza kuokoa asilimia
30 ya gharama ya kununua gari jipya la zimamoto pia watakuwa na uwezo wa
kuyatengeneza magari hayo badala ya kuagiza wataalamu toka nje ya nchi mara
yanapoharibika,”alisema Mangazeni.
Aidha alisema kuwa kwa upande wa matrekta wataweza
kuyaunganisha ambapo kwa miaka ijayo watakuwa na uwezo wa kutengeneza trekta
ambalo litakuwa ni zao la Tanzania tofauti na ilivyo sasa kuagizwa toka nje ya
nchi.
“Miaka ijayo tutatengenza trekta la kwetu ambapo
kwa sasa vitakuwa vinakuja vifaa vyake na kuunganishiwa hapa na tatizo la
matrekta kufa haraka litakwisha kwani mafundi wa matrekta watazalishwa hapa na
yatadumu kwani wengi hawana utaalamu wautengenzaji bali wanatumia uzoefu tu,”
alisema Mangazeni.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kibaha Asumter
Mshama alisema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho umekuja wakati mwafaka kwa upande
wa janga la moto na kilimo bora.
Mshama alisema kuwa kiwanda hicho ambacho kitafanya
shghuli hizo kwa pamoja itakuwa mwarobaini wa changamoto hizo ambazo ni kubwa
na pia ni kutekeleza sera ya Rais John Magufuli ya kutaka Tanzania kuwa nchi ya
viwanda ili baada ya miaka ijayo nchi kuwa na uchumi wa kati.
Ujenzi wa kiwanda hicho ulianza ulianza 2011
ambacho hadi kukamilika kwake kitakuwa na thamani ya shilingi bilioni tatu
kitaajiri wafanyakazi 100 na kamapuni hiyo imeingia ubia na Suma Jkt na
inaundwa na wanajeshi wastaafu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment