Tuesday, August 30, 2016

MBUNGE AITAKA DAWASCO KUUNGANISHA MAJI BILA YA UPENDELEO WA FEDHA


Na John Gagarini, Kibaha

MAMLAKA ya Maji Safi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) wilaya ya Kibaha mkoani Pwani imetakiwa kuwaunganishia maji wananchi wa Mlandizi bila ya kujali uwezo wa mtu ili kila mtu aweze kunufaika na mradi wa maji kwenye Kitongoji cha Janga.
Hayo yalisemwa na mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijni Hamoud Jumaa wakati alipofanya ziara kutembelea mradi wa maji wa ya mkopo kwenye kitongoji cha Janga kata ya Janga wilayanai Kibaha.

Mbunge huyo alitoa wito huo kufuatia mwenyekiti wa kitongoji hicho Josephine Maendaenda kudai kuwa baadhi ya wananchi wanalalamika kuwa watu wanaotoa fedha taslimu ndiyo wanaounganishiwa maji huku wale wanaokopa kutakiwa kusubiri.

“Kwanza nawapongeza wananchi kwa kuchimba mitaro ya kulaza mabomba hivyo thamani ya nguvu zao lazima zithaminiwe sawa na wale wanaotoa fedha taslimu kwani mitaro hiyo isingechimbwa na wananchi hao maji yasingeweza kufika kwenye maeneo ya watu,” alisema Jumaa.

Alisema kuwa thamani ya watu iko palepale lakini haiwezi kwani wanaotoa fedha na wale waliotumia nguvu zao kuchimba mitaro wamefanya kazi kubwa ambayo inapaswa kuungwa mkono na siyo ya kubezwa.

“Wananchi hawa wameonyesha uzalendo wa hali ya juu kwa kufanyakazi ya kujitolea na ndiyo tunataka utamaduni huu ufanyike kwenye kila jambo na si kusubiri serikali iwafanyie wananchi kila kitu kwani hata kwenye mikoa iliyoendelea kama Moshi na Arusha imefanikiwa kwa wananchi kujitolea kama huku,” alisema Jumaa.

Kwa upande wake meneja wa Dawasco wilaya ya Kibaha Erasto Emanuel alisema kuwa suala hilo watalifanyia kazi kwa kuwaunganishia wananchi bila ya kujali kama ni malipo ya moja kwa moja au mkopo.

Emanuel alisema kuwa hadi sasa wameweza kuwaunganishaia maji wananchi 40 huku wakitarajia kuwafikia wateja 300 katika hatua ya pili huku wakitarajia maji kuanza kutoka mwezi Oktoba na kuwafikia wateja 600.

Alisema kuwa mradi huo ulikumbwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa jambo ambalo lililalamikiwa na wananchi lakini yote hiyo ilitokana na kila mwaka kuwa na zoezi la kufunga mwaka ambalo huambatana na uhakiki wa vifaa.

Naye mwenyekiti wa Kitongoji cha Janga Josephine Maendaenda alisema kuwa changamoto ya maji ni kubwa kwenye kitongoji hicho na wananchi wamekuwa wakilalamika kiu yao kubwa ikiwa ni kupata maji ambapo wamekuwa wakienda mwendo mrefu kufuata maji ambapo huuziwa dumu la lita 20 kwa shilingi 500.

Mwisho. 

No comments:

Post a Comment