Sunday, December 27, 2015

HABARI MBALIMBALI ZA MKOA WA PWANI

Na John Gagarini, Kibaha

MKOA wa Pwani unatarajiwa kuwa moja ya mikoa ambayo itakuwa kwa kasi kutokana na kuongezeka kwa shughuli nyingi za uwekezaji za kiuchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bandari wilayani Bagamoyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa mkoa una fursa nyingi za uwekezaji na watu binafsi pamoja na makampuni yameonyesha nia ya kuwekeza.

Ndikilo alisema kuwa uwekezaji umeanza kuchukua nafasi yake baada ya Jiji la Dar es Salaam kuonekana kuwa limejaa hivyo fursa iliyopo ni mkoa huo ambao uko jirani na Dar es Salaam.

“Kwa sasa tunajivunia na mojawapo ya uwekezaji mkubwa ni ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ambayo itaongeza pato la mkoa huo kwani utazalisha ajira nyingi na wageni wengi wataingia kwa ajili ya shughuli nyingi za kibiashara,” alisema Ndikilo.

Alisema uwekezaji mwingine ni pale Kisarawe ambapo kimejengwa kiwanda cha saruji, Kibaha kuna viwanda vya Jipsam, Nondo na uwekezaji sehemu nyingine mbalimbali za wilaya zinazounda mkoa huo.

“Tukija kwenye zao kuu la biashara la Korosho nalo limezidi kunufaisha wakulima ambapo kwa sasa kilo ya korosho imepanda na kwa mnada sasa inauzwa kati ya 2,600 na 2,700 kutoka chini ya shilingi 1,000 na hii ni kutokana na mfumo wa stakabadhi ghalani,” alisema Ndikilo.

Aidha alisema kuwa kwa kipindi kirefu mkoa huo haukuwa na fursa nyingi hali ambayo ilisababisha uonekane kama uko nyuma kiuchumi tofauti na ilivyo sasa fursa zimekuwa nyingi sana hivyo mafanikio ya kiuchumi yatakuwa makubwa.

Aliwataka watu wa mkoa huo hususani vijana kutumia fursa hizo zilizopo ambazo zimejitokeza kwa sasa ili kujikwamua na hali ngumu ya kimaisha pia watumie fursa za kilimo ambazo ni nyingi.

Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha

MKOA wa Pwani unaendelea na uhakiki wa watu walioweka mashamba pori ili taarifa zipelekwe kwa Waziri husika na baadaye kwa Rais ili kutengua umiliki wao endapo watashindwa kuyaendeleza hususani wale walionunua kwenye kitovu cha Mji wa Kibaha.

Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa kuna mashamba pori mengi makubwa ambayo hayajaendelezwa kwenye wilaya zote za mkoa huo ikiwa ni pamoja na Kibaha, Kisarawe, Rufiji, Bagamoyo na Mkuranga.

Ndikilo alisema kuwa tayari wameshaanza kuyafanyia kazi mashambapori hayo kwa kushirikiana na wakurugenzi wa Halmashauri kwa mashamba yasiyoendelezwa.

“Tayari tumeshawapelekea notisi baadhi yao ili wajieleze ni kwanini wameshindwa kuyaendeleza mashamba hayo na kwanini wasinyanganywe kutokana na kushindwa kuyaendeleza,” alisema Ndikilo.

Kwa upande wa kitovu cha Mji wa Kibaha ambako ndiyo makao makuu ya mkoa huo alisema kuwa wamiliki binafsi pamoja na taasisi ambazo ni nyingi wameshapewa barua kujieleza kwanini hawakuviendeleza viwanja hivyo.

“Tunawashangaa ni kwa nini wameshindwa kuendeleza viwanja hivyo ambavyo endapo vingejengwa vingeweka suraa nzuri ya mji kwani hapo ndiyo kwenye mandari ya uso wa mji,” alisema Ndikilo.

Alisema kuwa licha ya kutakiwa kujieleza kwa nini hawakuviendeleza viwanja hivyo pia waeleze kuwa watavijenga lini na muda watakaokubaliana hawapaswi kuupitisha tena.

“Kwa watakaoshindwa kuviendeleza baada ya makubaliano watanyanganywa viwanja hivyo ili wapewe wengine watakaoweza kuviendeleza kwa kujenga kwa wakati ukaoakuwa umepangwa,” alisema Ndikilo.

Mwisho.

Na John Gagarini, Kibaha

JUMUIYA ya Wazazi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini kimezigawia Jumuiya za Kata ardhi yenye ukubwa wa hekari moja kwa lengo la kuziendeleza kiuchumi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha baada ya zoezi hilo la kuwagawia ardhi hiyo ambalo lilifanyika kwenye sherehe za siku ya Uhuru, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Kibaha Mjini Dk Athuman Mokiwa alisema kuwa eneo hilo litakuwa kitovu cha uchumi wa Jumuiya hiyo.

Mokiwa alisema kuwa eneo hilo lenye ukubwa wa hekari 15 wameligawa kwa kata 14 za kichama ambapo kila kata inapaswa kuziendeleza kwa kulima na baadaye kufanya ujenzi.

“Kipindi cha nyuma tulishindwa kuliendeleza kutokana na kukosa fedha kwa ajili ya kulipima lakini baada ya kulipima sasa tumegawa kila kata wawe na eneo lao kwa ajili ya shughuli za kiuchumi,”alisema Dk Mokiwa.

Alisema kuwa shamba hilo lilikuwa likivamiwa na watu kutokana na kutokuwa na hati za umiliki lakini kwa sasa wameshalimiliki kisheria hivyo hakuna mtu atakayeweza kuvamia tena.

Naye katibu wa Wazazi kata ya Kibaha lilipo shamba hilo Rehema Ally alisema kuwa wanaushukuru uongozi kwa kuwapatia eneo ambapo wanatarajia kuliendeleza na hiyo ni rasilimali yao kiuchumi.

Ally alisema kuwa baada ya kupatikana hati watawakaribisha wawekezaji kwa ajili ya kujenga taasisi zikiwemo za shule au zaahanati na huduma nyingine za kijamii.

Viongozi wa Jumuiya hizo za kata wamekubaliana kufanya usafi kila baada ya wiki mbili ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Dk John Magufuli juu ya usafi kukabiliana na magonjwa ya milipuko pia kuweka maeneo mbalimbali katika hali ya usafi.

Mwisho.

Na John Gagarini, Kibaha

KUFUATIA dereva wa Pikipiki wa Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani Ally Rashid (35) kuuwawa kwa kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kisha kumpora pikipiki aliyokuwa akiieendesha madereva wenzake wameomba uchunguzi wa kina ufanyike kuhusiana na tukio hilo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha katibu wa Chama Cha Madereva Pikipiki Kibaha (CHAWAMAPIKI) Shaban Kambi alisema tukio hilo ni la kushangaza kwa watu kutumia bunduki kwa ajili ya kupora pikipiki likiwa ni tukio la pili.
Kambi alisema kuwa kumekuwa na matukio ya wizi wa pikipiki lakini kwa kutumia bunduki si hali ya kawaida hivyo tunaomba polisi wafuatilie tukio hilo la kusikitisha kwa mwenzetu kuuwawa.

“Matukio ya kutumia silaha ni matatu ambapo mtu mmoja alivamiwa nyumbani kwake na kupigwa risasi na kufa la pili ni mwenzetu mwingine alipigwa risasi ya mguuni na kuporwa pikipiki lakini hakufa huku mwenzetu wa juzi naye alipigwa risasi na kufa ambapo cha kushangaza matukio yote yametokea upande mmoja,” alisema Kambi.

Alisema matukio yote hayo yametokea maeneo ya machinjioni hali ambayo inawapa hofu wakazi wa Maili Moja kwa kuona kuwa maisha yao sasa yako hatarini kwa watu hao kufanya uahalifu kwa kutumia bunduki.

“Tumesha waambia madereva pikipiki kuwa makini kwani kuna baadhi ya maeneo kwa sasa ni hatarishi pia wakiwa na wasiwasi wasiwabebe watu wasiowafahamu hasa nyakati za usiku hasa katika kipindi hichi cha mwisho wa mwaka,” alisema Kambi.

Aidha alisema kuwa wao wako tayari kushirikiana na jeshi la polisi katika kufuatilia watu wanaojihusisha na matukio hayo ya uporaji wa pikipiki pamoja na mali za watu.

Mwisho.

Na John Gagarini, Kibaha

MKOA wa Pwani unatarajia kujenga Kituo Kikubwa cha Mabasi pamoja na Soko baada ya kupata mkopo toka Benki ya Uwekezaji ya (TIB) na kuufanya mji wa Kibaha kuwa wakisasa.

Hayo yalisemwa na mkuu wa mkoa wa Pwani alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo na kusema kuwa kwa sasa taratibu zinaendelea baina ya Halmashauri ya Mji wa Kibaha na benki hiyo.

Ndikilo alisema kuwa ujenzi huo unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa mara taratibu za kitaalamu zitakapokamilika ambapo kwa sasa bado zinaendelea.

“Tunatarajia kuwa na stendi ya kisasa pamoja na soko hasa ikizingatiwa mkoa ulikuwa hauna soko kubwa bali lililopo ni dogo na halina uwezo wa kuchukua bidhaa nyingi,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa wafanyabiashara wa mkoa wa Pwani hususani wale wa makao makuu ya mkoa Maili Moja na vitongoji vyake huwalazimu kwenda kununua bidhaa Kariakoo au kwenye masoko mengine Jijini Dar es Salaam jambo ambalo linafanya bei za bidhaa kuwa juu.

“Kibaha ambako ndiyo makao makuu ya mkoa ni kama malango wa Jiji la Dar es Salaam lakini bidhaa zimekuwa zikipita hapa na kwenda huko kisha wafanyabiashara kwenda kununua na kuzirudisha hapa hivyo kupandisha bei kutokana na gharama kuwa kubwa,” alisema Ndikilo.

Aidha alisema kuwa soko hilo ambalo litajengwa sambamba na stendi litakuwa la kisasa ambapo magari yatakuwa na uwezo wa kuingia na kushusha bidhaa na si kama ilivyo sasa ambapo kutokana na udogo wa soko lililopo hubidi magari ya bidhaa yashindwe kuingia.

Mwisho.
  

   

   

  




No comments:

Post a Comment