Monday, December 21, 2015

WANAFUNZI 204 HAWAKUFANYA MTIHANI WA DARASA LA SABA

Na John Gagarini, Kibaha

WANAFUNZI 204 mkoani Pwani hawakufanya mtihani  wa kumaliza elimu ya Msingi kwa mwaka 2015 kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoro.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Katibu Tawala wa mkoa huo Mgeni Baruan wakati wa kutangaza matokeo ya wanafunzi waliofanya mtihani wa darasa la saba kwa mwaka 2015 na kusema kuwa jumla ya wanafunzi waliofanya mtihani huo walikuwa 22,191 sawa na asilimia 99.1.

Baruan alisema kuwa wanafunzi ambao hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoro 185, vifo watano, ugonjwa wanane, huku sababu nyingine wakiwa ni wawili.

“Ukiachilia mbali wanafunzi hao ambao hawakufanya mtihani  na ufaulu wa wanafunzi kwa mkoa huo umefikia asilimia 63.1 ikilinganishwa na mwaka 2014 sawa na asilimia 56.2.,” alisema Baruan.

Alisema kuwa wanafunzi 14,010 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2016 kati ya wanafunzi baada kufaulu mtihani wao wa kumaliza elimu ya Msingi ambapo wanafunzi wote waliofaulu wamepata nafasi na hakuna aliyekosa nafasi.

“Kati ya idadi ya wanafunzi waliofanya mtihani ni wavulana ni 10,024 na wasichana ni 12,167 huku ikionyesha kuwa mkoa haukupata tuhuma za udanganyifu katika zoezi la ufanyaji mtihani,” alisema Baruan.

“Mkoa umeshika nafasi ya 14 kitaifa hata hivyo ufaulu huo hauridhishi kwani haujafikia kiwango cha asilimia 80 kwa mujibu wa mwelekeo wa Matokeo Makubwa Sasa Big Results Now (BRN) hivyo zinahitajika jitihada zaidi ili kufikia kiwango hicho,” alisema Baruan.

Kwa upande wake ofisa elimu mkoa Yusuph Kipengele alisema kuwa agizo la Rais la Dk John Pombe Magufuli la kuondolewa kwa ada na michango mbalimbali kuanzia shule ya msingi na sekondari liko palepale.

Kipengele alisema kuwa baadhi ya michango iliyoondolewa ikiwa ni pamoja na ada ni vitambulisho, mawadati, majengo,  vifaa vya michezo mlinzi haitakuwepo na mwalimu atakayechangisha mchango wowote atakuwa anakiuka agizo la Rais.

Hata hivyo alisema kuwa jukumu la wazazi ni kumnunulia vifaa vya shule mwanae ikiwa ni pamoja sare za shule, madaftari, kalamu, chakula, nauli na vifaa vingine vidogovidogo ambavyo siyo mzigo kwa mzazi yoyote.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment