Na John Gagarini, Kibaha
MLINZI wa kampuni ya Ulinzi ya Optima inayolinda kwenye jengo
la Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Pwani Primc Bararwirwa
amekutwa amekufa jirani na na kituo kikuu cha Mabasi cha Maili Moja Wilayani Kibaha.
Tukio hilo lilitokea Desemba 4 mwaka huu majira ya asubuhi
jirani na Grosari ya Kilimani ambapo mwandishi wa habari hizi aliushuhudia
mwili wa marehemu ukiwa chali na kufunikwa na shuka huku ukiwa hauna viatu.
Baadhi ya watu waliomshuhudia marehemu kabla ya kifo chake walisema
kuwa usiku wake walimwona marehemu akiwa na wenzake huku wakiongea lakini
walishangaa asubuhi kuona akiwa amekufa na hakuwa na jeraha lolote mwilini
mwake.
Polisi walifika kwenye eneo hilo na kuuchukua mwili wa
marehemu kisha kuupeleka Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani kwa ajili ya
kuchunguza kifo chake na kusubiri ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Kamanda wa polisi mkoani Pwnai Jafary Mohamed alithibitisha
kutokea tukio hilo ambapo wanaendelea na uchunguzi kujua chanzo cha kifo hicho
ambacho kimewashtua wakazi wengi wa Maili Moja waliokuwa wanamfahamu marehemu.
Katika tukio lingine mkulima wa Kijiji cha Zogowale kata ya
Misugusugu Aloyce Chuma (54) amefariki dunia huku watu wengine watatu
wakijeruhiwa baada ya kupigwa na radi ambayo
iliambatana na upepo mkali.
Akizungumza na gazeti hili mwenyekiti wa Mtaa wa Zogowale
Rajab Mhanyige alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 10 jioni wakati
marehemu akiwa amekaa kwenye gogo na wenzake hao waliojeruhiwa wakati
wamepumzika baada ya shughuli za kilimo.
Mhanyige alisema kuwa radi hiyo ilipiga sehemu walipokuwa
wamekaa watu hao na kumwua marehemu na kuwajeruhi wenzake huku yeye akifia eneo
la tukio na hakuwa na jeraha lolote mwilini mwake.
“Siku hiyo ilipiga radi kali iliyoambatana na upepo mkali ambayo
mimi sijawahi kusikia tangu kuzaliwa kwangu ilikuwa na kishindo kikubwa sana na
niliamini kuwa itakuwa imeleta matatizo na kweli kwani baada ya muda nilletewa
taarifa kuwa kuna mtu kafa kutokana na radi hiyo ambapo baadaye mvua kubwa
ilinyesha,” alisema Mhanyige.
Alisema mara baada ya tukio hilo waliuchukua mwili wa
marehemu pamoja na majeruhi na kuwapeleka kwenye kituo cha Afya cha Mlandizi
kwa ajili ya kuhifadhi mwili na majeruhi kwa ajili ya matibabu ambao nao
hawakuwa na majeraha yoyote.
Aidha aliwataja majeruhi ambao baadaye waliruhusiwa kurudi
nyumbani kuwa ni Cosmas Bandula (54), Sultan Kigumu ambaye alirushw aumbali wa
mita 10 na mtu aliyetambuliwa kwa jina moja la Kamugisha (48). Polisi
walithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment