Na John Gagarini, Kibaha
WANANCHI wanaoishi jirani na Hifadhi ya Msitu wa Ruvu Kusini
wametakiwa kuacha kufanya uharibifu wa msitu huo badala yake wautumie kama
chanzo cha mapato kwa njia ya Utalii.
Hayo yalisemwa kwenye Kijiji cha Kipangege wilayani Kibaha
mkoani Pwani na ofisa miradi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Usimamizi wa Misitu
ya Asili Tanzania (TFCG) Yahaya Mtonda wakati wa tamasha la Kimataifa la Utalii
wa kutumia Baiskeli.
Mtonda alisema kuwa kutokana na umuhimu wa misitu ukiwemo
msituo ambao unatumika kuchuja hewa safi ukiwa ni mapafu ya kupumulia hewa ya
Jiji la Dar e s Salaam wananchi wanapaswa kuulinda na kuondokana na dhana
kukata miti kwa ajili ya kujiongezea kipato.
“Kwa sasa tumeshaweka mazingira ya kuufanya msitu huu kuwa
wakitalii tofauti na ilivyokuwa mwanzo kwani kwa sasa watalii watakuja
kuutembelea na kufanya utalii kujionea miti mbalimbali ya asili ambayo
inapatikana hapa Tanzania na hakuna sehemu nyingine inakopatikana hivyo ni
wakati sasa wa wananchi kutumia fursa hii kujiongezea kipato kupitia utalii
badala ya kukata miti kwa ajili ya mbao na kuni au mkaa,” alisema Mtonda.
Alisema kuwa endapo wananchi watatumia fursa hiyo watapata
mapato huku wakienedelea kutunza msitu huo pamoja na kuhifadhi mazingira na
kukabilian na changamoto ya tatizo la Tabianchi ambayo inasababisha kukosekana
mvua na kusababisha hali ya hewa kuwa mbaya hususani kuwa na joto kali.
Kwa upande wake Mshauri wa Ufundi wa (TFCG) Andrew Perkin
lengo la tamasha hilo ni kuwapa uelewa wananchi juu ya umuhimu wa kulinda
misitu ili waweze kufurahia mazingira mazuri ambayo uoto wake wa asili
unasababisha hali ya hewa kuwa safi.
Perkin alisema kuwa misitu hiyo ilikuwa ikiharibiwa sana na
wananchi kutokana na kukata miti kwa ajili ya shughuli za kibinadamu zikiwa ni
pamoja na uvunaji wa misitu ambapo kwa sasa tayari wameshawaondoa watu
waliokuwa kwenye msitu huo na hali yake inaanza kurudi kama ilivyokuwa mwanzo.
Naye mwenyekiti wa Umoja wa Wapanda Baiskeli (UWABA) Meja
Mbuya alisema kuwa wamekuwa wakihamasisha watu kupanda baiskeli kwani matumizi
ya magari yamekuwa yakiharibu mazingira kutokana na moshi unaotokanan na magari
hayo.
Mbuya alisema kuwa mbali ya kupanda baiskeli wamekuwa wakitoa
elimu mbalimbali ya juu ya utunzaji wa misitu na kushauri matumizi ya nishati
ya jua na upepo katika baadhi ya matumizi ili kutoharibu mazingira. Jumla ya
watu zaidi ya 100 toka mataifa mbalimbali walishiriki tamasha hilo ambapo
walitembea umbali wa kilometa 30.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment