Na John Gagarini, Kibaha
WAKAZI wa Kijiji cha Kiluvya B wilaya ya Kisarawe mkoa wa
Pwani wameiomba Wizara ya Ujenzi na Makazi iangalie upya tafsiri ya upanuzi wa
barabara kuu kwani upanuzi uliofanyika ni urefu wa mita 120 upande mmoja wakati
sheria inasema kila upande wa barabara itapanuliwa kwa urefu wa mita 60 kwa 60 kutoka
katikati ya barabara kuu.
Kutokana na sheria hiyo kutafsiriwa mita 120 nyumba zilizojengwa
kando ya Barabara ya Morogoro baadhi zimebomolewa na nyingine zimeekewa alama
ya X zikitakiwa kubomolewa baada ya muda usiozidi zaidi ya wiki moja na
kupelekea kilio kikubwa kwa wakazi hao.
Wakizungumza waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho
moja ya wakazi hao aliyejitambulisha kwa jina la Abubakary Yusuph alisema kuwa athari
ya kubomolewa nyumba hizo ni kubwa sana hivyo kuomba suala hilo liangaliwe
upya.
Yusuph alisema kuwa wao hawana tatizo la kuondoka kwenye eneo
hilo kwa ajili ya kupisha shughuli za maendeleo bali wameomba sheria ifuatwe
ili wasinyimwe haki zao kwani wao wako hapo tangu vilipoanzishwa vijiji vya
ujamaa miaka ya 70.
“Tunaomba wizara na serikali kuliangalia upya suala hili
kwani sisi hatuna shida kwa wale waliojenga ndani ya mita 60 kwani tunajua
suala hilo ni la kisheria lakini mita 120 tunaona kuwa hatujatendewa haki ni
vema wanapotekeleza suala hilo wakazingatia sheria ya barabara na kama wanataka
eneo zaidi ni vema wakatulipa ndipo waendelee na zoezi hilo,” alisema Yusuph.
Alisema kuwa watu wengi walijenga umbali zaidi ya mita 60
kwani walikuwa wakijua kuwa kama watakuwa ndani ya mita hizo basi bomobomoa
ikija wangebomolewa nyumba zao lakini walikojenga walijua wako salama
wanashangaa kuona nyumba zao zinabomolewa.
Naye Alfonce Kejo alisema kuwa baadhi yao ni wastaafu na
hawana kipato chochote na waliwekeza kwenye nyumba zao kwa ajili ya makazi mara
baada ya kustaafu kazi hivyo wanaomba suala lao lishughulikiwe ili wapate haki
yao.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Kijiji hicho Julius Bukoli
ambaye naye amekumbwa na bomoa bomoa hiyo alisema kuwa nyumba yake aliijenga
kabla ya mwaka 2000 na iko umbali wa karibu mita 100 toka barabara kuu lakini
ametakiwa kubomoa.
Bukoli alisema kuwa hata wanaohusika katika kubomoa nyumba
hizo hawafuati taratibu za kutoa taarifa kwenye uongozi wa Kijiji bali wanakuja
nyakati za jioni na kubomoa au kuweka alama za X kisha kuondoka.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA Cha Kuweka na Kukopa Cha TCCIA
Saccos mkoa wa Pwani kimeweza kukopesha mikopo inayofikia zaidi ya shilingi
milioni 398 kwa wanachama wake.
Akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake mjini Kibaha, Meneja wa chama hicho Arestide Temu alisema kuwa
fedha hizo zimetolewa kwa wanachama waliofuata taratibu za mikopo kwa
lengo la kukuza mitaji yao ya biashara.
Temu alisema kuwa hata hivyo biashara
nyingi kwenye mkoa huo zinashindwa kukua vizuri kutokana na kutokuwa na
mzunguko mkubwa wa fedha kwa sababu ya kuwa na shughuli chache za kiuchumi
ikiwa ni pamoja na ukosefu wa viwanda.
“Sababu nyingine ya wafanyabiashara
kushindwa kufikia malengo ni kutokana na kufanya biashara zinazofanana na
kusababisha kushindwa kufikia malengo hata hivyo tumepata mafanikio tumeweza
kupata faida ya shilingi milioni 26 tofauti na lengo la kupata faida ya
shilingi milioni 20 tulizokuwa tumejipangia kwa mwaka huu ambapo faida hiyo ni
hadi mwezi Novemba mwaka huu,” alisema Temu.
Alisema kuwa maendeleo ya chama
yanakwenda vizuri ambapo kwa sasa wamanachama wanaweza kukopa mara tatu ya
fedha walaizojiwekea kama akiba na wanaweza kukopa hadi shilingi milioni 15 kwa
mara moja.
“Riba ni asilimia 15 ya mkopo wowote
anaoomba mwanachama ambapo hisa moja inauzwa kiasi cha shilingi 10,000 huku
mwanachama akitakiwa kununua hisa kuanzia 10 na kuendelea,” alisema Temu.
Aidha alisema kuwa chama hicho cha
kuweka na kukopa kilianzishwa mwaka 2001 kikiwa na wanachama 600 ambapo kwa
sasa kina wanachama 227 huku wengine wakiwa wameondolewa kwa kushindwa kufuata
taratibu za chama.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment