Na John Gagarini, Kibaha
BONANZA la kuuaga mwaka 2015 na kuukaribisha mwaka 2016
linatarajiwa kufanyika Januari Mosi mwakani kwenye uwanja wa Shirika la Elimu
Kibaha (KEC) Tumbi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Msajili Msaidizi wa
Vilabu na Vyama vya Michezo wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Abdul Haufi alisema
kuwa Bonanza hilo litakuwa la wazi kwa watu wote.
Haufi alisema kuwa shindano hilo litakuwa la michezo
mbalimbali litashirikisha mashirika ya Umma, binafsi pamoja na watu binafsi au
mtu mmoja mmoja kwenye michezo ya soka, mpira wa pete kwa wanawake, kuvuta
kamba, riadha mita 100.
Alitaja michezo mingine kuwa ni kukimbia na magunia, kurusha
kisahani, tufe, mpira wa wavu, kijiko na ndimu ambapo usajili unafanyika kwenye
ofisi za Halmashauri hiyo.
“Tunatarajia jumla ya wanamichezo 250 kushiriki Bonanza hilo
la aina yake kufanyika mjini Kibaha na vitongoji vyake ambapo lengo ni
kuhamasisha watu kushiriki michezo pamoja na kudumisha urafiki baina ya
mashirika bianafsi, ya umma pamoja na watu binafsi,” alisema Haufi.
Aidha alisema kuwa juu ya wadhamini tayari baadhi
wameshajitokeza huku wakiwasubiri wengine wamalizia taratibu za kudhamini
Bonanza hilo na matarajio ni kutolewa zawadi nono.
Bonanza hilo limeandaliwa kwa pamoja na Halmashauri ya Mji
Kibaha, Majeshi ya mkoani Pwani ikiwa ni pamoja na Magereza, Polisi na Jeshi la
Wananchi Tanzania (JWTZ).
Mwisho.
No comments:
Post a Comment