Na John Gagarini, Kibaha
NAIBU Waziri wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo
Anastazia Wambura amewataka watu wanaovamia maeneo ya viwanja vya michezo
kukomesha tabia hiyo kwani inawanyima fursa vijana kushiriki kwenye michezo.
Aliyasema hayo hivi karibu mjini Kibaha wakati akifunga
michuano ya kombe la Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka (Koka Cup)
kwenye uwanja wa Mwendapole wilayani humo na kusema kuwa watu hao hawapaswi
kuungwa mkono kwani wanawanyima ajira vijana.
Wambura alisema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakivamia maeneo
ya michezo na kujenga jambo ambalao linakwenda kinyume na matumizi yaliyopangwa
na serikali hivyo vijana kushindwa kuendeleza vipaji vyao.
“Watu wenye tabia hii inabidi waiache kwani inadumaza azma ya
serikali kuendeleza michezo mbalimbali hapa nchini hasa ikizingatiwa licha ya
michezo kuwa ni burudani lakini pia inatoa fursa ya ajira hasa kwa vijana,”
alisema Wambura.
Alisema kuwa serikali imekuwa na mipango mbalimbali ya
kuendeleza michezo ikiwa ni pamoja na kuwa na viwanja ambavyo vitawawezesha
vijana kushiriki michezo hivyo watu wanaovamia na kujenga ni dhahiri
wanakwamisha juhudi hizo.
“Tunaomba wadau wa michezo wahamasishe ujengwaji wa viwanja
vya kisasa ambapo baadhi ya watu wameonyesha uzalendo kwa kujenga viwanja
ambavyo vinaendeleza jitihada za serikali kuendeleza michezo,” alisema Wambura.
Kwa upande wake Koka alisema kuwa lengo la kuandaa mashindano
hayo ni kuwahamasisha vijana kushiriki michezo kwenye Jimbo lake ambapo
alizipatia timu zote vifaa vya michezo kwa ajili ya kushiriki ligi hiyo.
Koka alisema kuwa jumla ya timu 168 katika Jimbo hilo
zilishiriki ligi hiyo iliyoanzia ngazi ya mitaa hadi kata na baadaye kupata
mshindi wa Jimbo ambapo jumla ya wachezaji zaidi ya 4,000 walishiriki michuano
hiyo na bingwa alikuwa ni Home City toka kata ya pangani baada ya kuifunga
Lisborn kutoka kata ya Kongowe kwa Penati 6-5.
Mshindi wa tatu ni Phata Farm ya Mkuza iliyoifunga
Visiga 3-0, Bingwa alijinyakulia kiasi
cha shilingi 500,000 na kombe huku mshindi wa pili akijinyakulia 500,000 na
medali na mshindi wa tatu akijinyakulia 200,000 ngao na medali
Mwisho.
No comments:
Post a Comment