Na John Gagarini, Bagamoyo
KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka
Nchini (TFF) Selestine Mwesigwa amewaomba wabunge kwenye Majimbo mbalimbali
kuendeleza soka ngazi za chini ili kuibua wachezaji watakaokuwa wachezaji wa
vilabu vikubwa pamoja na timu ya Taifa kwa siku za baadaye.
Aliyasema hivi karibuni wakati
akikabidhi zawadi za washindi wa kombe la Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Dk
Shukuru Kawambwa (Kawambwa Cup) ambapo timu ya Jitegemee iliibuka mabingwa
baada ya kuichapa Buma 2-0 kwenye uwanja wa Mwanakalenge wilayani Bagamoyo
mkoani Pwani.
Mwesigwa alisema kuwa wachezaji wengi
walianzia ngazi za chini hivyo wabunge wana nafasi kubwa ya kuibua vipaji
ambavyo vimejificha huko Vijijini na mashindano kama hayo ndiyo yenye uwezo wa
kuwaibua vijana.
“Wabunge wengine wanapaswa kuiga
mfano wa mashindano hayo ya Kawawmbwa Cup ni jambo la busara kwani linainua
vipaji vya vijana, kujenga afya zao pia nakuomba usiishie hapa anzisha na
mashindano ya mpira wa wanawake na sisi TFF tutakuunga mkono kwa hilo”, alisema
Mwesigwa.
Aliwataka wachezaji wanaopata nafasi
ya kwenda kucheza kwenye timu kubwa kujenga nidhamu na kuzingatia mafunzo ya
makocha ili waweze kufikia mafanikio makubwa.
Kwa upande wake Dk Kawambwa aliwashukuru wadau
wote walioshirikiana nae kufanikisha mashindano hayo na kusema kuwa mashindano
hayo yamedumu kwa miaka 10 mfululizo ambapo ameahidi kuyaboresha na
kuyaendeleza katika kipindi kingine cha miaka mitano ijayo.
Dk.Kawambwa alisema lengo la kuanzisha mashindano hayo ni kuibua vipaji vya vijana kuanzia vijiji, kata na wilaya pamoja na kuwaepusha kukaa vijiweni bila shughuli yoyote.
Timu ya Jitegemee Fc kata ya Magomeni iliibuka
Kidedea katika mashindano hayo ya 2015 nakujinyakulia zawadi ya kombe, seti ya
jezi, mipira miwili, pikipiki na medali ya dhahabu.
Mshindi wa pili alikuwa ni Buma waliopata seti ya jezi na mipira, na mshindi wa tatu timu ya Mwambao ilikabidhiwa seti ya jezi na mipira na timu yenye nidhamu pamoja na kipa bora walipatiwa zawadi ya ngao. Mashindano ya Kawambwa Cup yalishirikisha vilabu 73 kutoka kata Saba za Jimbo la Bagamoyo.
No comments:
Post a Comment