Na John Gagarini, Kibaha
MARIAMU Mpembenwe (85) mkazi wa Mkoani A kata ya Tumbi
wilayani Kibaha mkoani Pwani anakabiliwa na tatizo la maumivu ya viungo mbalimbali
vya mwili ikiwemo mguu na mkono hali iliyomfanya ashindwe kutoka nje kwa kipindi
cha miaka mitano.
Aidha anaomba kupatiwa baiskeli ya watu wenye ulemavu ili
iweze kumsaidia kuweza kutembelea kwenda kupata huduma muhimu ikiwemo za
matibabu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Kibaha waliomtembelea
nyumbani kwa mwanae alisema kuwa hali yake kiafya ni mbaya kutokana na kukosa matibabu
pamoja na chakula kwani mwanae ambaye anamtegemea hana kipato chochote cha
kujikimu zaidi ya kuomba misaada.
Mpembenwe alisema kuwa anakabiliwa na matatizo mengi ikiwa ni
pamoja na kutoona huku nyumba anayoishi kuvuja kipindi cha mvua.
“Nawaomba watu mbalimbali weneye uwezo ikiwemo serikali ili
niweze kukabiliana na changamoto zinazonikabili kwani sipati huduma bora za afya,
chakula, hata sehemu ninayolala kitanda hakina godoro na huduma za haja napata hapa
hapa mazingira ni mabaya naomba msaada wa fedha kwa ajili ya kujikimu,” alisema
Mpembenwe.
Kwa upande wake mtoto wa mama huyo Iddy Mtegya (65) alisema
kuwa ni kweli mama yake anakabiliwa na matatizo mengi likiwemo la kiafya licha
ya kwamba amekuwa akipatiwa matibabu hapo hapo nyumbani.
Mtegya alisema kuwa ni kweli hajatoka nje kwa kipindi hicho
kwani ana matatizo ya mguu wa kulia na mkono wa kulia hivyo kushindwa kutemebea
na kutokana na hali yake ya unene wanashindwa kumbeba kumtoa nje au kumpeleka
sehemu nyingine.
“Naomba msaada kwa watu wenye uwezo watusaidie kiti cha
magurudumu ili tuweze kumsaidia mama ili tuweze kumtoa mama nje pia kumpeleka
sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na hospitali licha ya kwamba yeye mwenyewe
hataki kwenda hospitali,” alisema Mtegya.
Naye diwani wa kata ya Tumbi Hemed Chanyika alisema kuwa
suala hilo linasikitisha kwani licha ya hali aliyokuwa nayo mama huyo anapaswa
kupatiwa huduma zote za kibinaadamu kwani kumnyima huduma hizo ni kumuongezea
matatizo.
Chanyika alisema kuwa hata baadhi ya watendaji wa mtaa
walipaswa kulieleza tukio hilo sehemu husika ili aweze kusaidiwa kupitia
vitengo mbalimbali vya misaada kwani wameonekana kutoliweka wazi suala hilo kwa
kipindi hicho cha miaka mitano.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mkoani A Titus Kabora alisema kuwa
wanataarifa ya mama huyo na familia hiyo ilianza kuhudumiwa kupitia mfuko wa
maendeleo ya jamii TASAF lakini tatizo misaada hiyo ni midogo na haitoshelezi
mahitaji.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment