Na John Gagarini, Kibaha
WAKANDARASI wanawake nchini wametakiwa kuomba kandarasi kubwa
zikiwemo za ujenzi wa barabara kubwa pamoja na viwanja vya ndege kupitia
kampuni zao za ujenzi ili kujiongezea kipato na kuiletea nchi maendeleo.
Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na Mkurugenzi wa iliyokuwa Wizara
Ujenzi Kegora wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo makandarasi wanawake katika
maandalizi ya zabuni na manunuzi kwa kazi za ujenzi wa barabara yaliyoandaliwa
na wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano.
Kegora alisema kuwa wanawake wameonyesha uwezo mkubwa kwa
kufanya kazi za ujenzi wa barabara kwa viwnago vinavyokubalika hivyo ni vema
wakaomba kandarasi za ujenzi mkubwa ambao zinatarajiwa kufanyika.
“Kwa sasa ombeni kazi za ujenzi mkubwa kama vile wa viwanja
vya ndege, bandari, madaraja na reli ili muonyeshe umahiri wenu katika kazi za
ujenzi na mnapaswa kuacha woga kwani uwezo mnao na mmeonyesha kuwa manaweza,”
alisema Kegora.
Alisema wanawake wakandarasi wanapaswa sasa kuacha kubaki
nyuma kwa kujenga miradi midogo midogo ya ujenzi bali wafanye miradi mikubwa ili
wapate mafanikio kama walivyofanikiwa kupitia ujenzi.
“Jiendelezeni kitaaluma mfikie madaraja ya juu ili mpate
kuimarika kitaaluma muwe juu pia muongeze idadi ya wakandarasi wanawake kwani
mmeonyesha kazi nzuri na ndiyo maana mnapewa mafunzo haya,” alisema Kegora.
Kwa upande wake mratibu wa mafunzo hayo Mhandisi Rehema Myeya
alisema kuwa mafunzo hayo yana lengo la kuwawezesha wakandarasi hao wanawake
kujua namna ya ujazaji wa zabuni na mikata wakati wa kuomba kandarasi.
Myeya alisema kuwa makandarasi wanawake wanakabiliwa na
changamoto kubwa ya kushindwa kujaza vizuri zabuni hizo hivyo kusababisha
kukosa kandarasi za ujenzi wa barabara hapa nchini hasa ikizingatiwa kuwa wengi
wao hawana elimu kubwa.
Jumla ya wakandarasi wanawake 26 kutoka mikoa Dar es Salaam,
Morogoro, Tanga, Singida, Kilimanjaro na Arusha ambapo hadi sasa tayari wamewapatia
mafunzo makandarasi zaidi ya 200 kwenye mikoa yote hapa nchini.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment