Na John Gagarini, Kibaha
JUMLA ya Wanafunzi 14,010 wamechaguliwa kujiunga na kidato
cha kwanza mwaka 2016 kati ya wanafunzi baada kufaulu mtihani wao wa kumaliza
elimu ya Msingi ambapo wanafunzi wote waliofaulu wamepata nafasi na hakuna
aliyekosa nafasi.
Akitangaza matokeo hayo jana mjini Kibaha kwa wanafunzi
waliofanya mtihani wa darasa la saba kwa mwaka 2015 katibu Tawala wa mkoa wa
Pwani Mgeni Baruan alisema kuwa jumla ya wanafunzi waliofanya mtihani huo
walikuwa 22,191 sawa na asilimia 99.1.
Baruan alisema kuwa waliotarajiwa kufanya mtihani
walitarajiwa kuwa ni 22,191 ambapo wanafunzi 204 hawakufanya mtihani huo na ufaulu
wa wanafunzi kwa mkoa huo umefikia asilimia 63.1 ikilinganishwa na mwaka 2014
sawa na asilimia 56.2.
“Mkoa umeshika nafasi ya 14 kitaifa hata hivyo ufaulu huo
hauridhishi kwani haujafikia kiwango cha asilimia 80 kwa mujibu wa mwelekeo wa
Matokeo Makubwa Sasa Big Results Now (BRN) hivyo zinahitajika jitihada zaidi
ili kufikia kiwango hicho,” alisema Baruan.
Alisema kuwa alisema kuwa kati ya idadi ya wanafunzi
waliofanya mtihani ni wavulana ni 10,024 na wasichana ni 12,167 huku ikionyesha
kuwa mkoa haukupata tuhuma za udanganyifu katika zoezi la ufanyaji mtihani.
“Wanafunzi ambao hawakufanya mtihani ni 204 ni kutokana na
sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoro 185, vifo watano, ugonjwa wanane,
huku sababu nyingine wakiwa ni wawili,” alisema Baruan.
Kwa upande wake ofisa elimu mkoa Yusuph Kipengele alisema
kuwa agizo la Rais la Dk John Pombe Magufuli la kuondolewa kwa ada na michango
mbalimbali kuanzia shule ya msingi na sekondari liko palepale.
Kipengele alisema kuwa baadhi ya michango iliyoondolewa ikiwa
ni pamoja na ada ni vitambulisho, mawadati, majengo, vifaa vya michezo mlinzi haitakuwepo na mwalimu
atakayechangisha mchango wowote atakuwa anakiuka agizo la Rais.
Hata hivyo alisema kuwa jukumu la wazazi ni kumnunulia vifaa
vya shule mwanae ikiwa ni pamoja sare za shule, madaftari, kalamu, chakula,
nauli na vifaa vingine vidogovidogo ambavyo siyo mzigo kwa mzazi yoyote.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment