Na John Gagarini, Kibaha
DEREVA Bodaboda Ally Kasimu (23) mkazi wa Kilimahewa wilayani
Kibaha mkoani Pwani amefariki dunia kwa kuchomwa kisu na waendesha pikipiki
wenzake wakati wakigombea mwakanamke.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha
mwenyekiti wa mtaa wa Mtakuja kata ya Pangani, Ramadhan Mwaya alisema kuwa
marehemu alikufa wakati wa mkesha wa kukaribisha mwaka mpaya wa 2016 na kuaga
mwaka 2015.
Mwaya alisema kuwa marehemu alikutwa na umauti huo akiwa
amekaa pembeni na pikipiki yake huku wenzake wakimgombea mwanamke kisha
kumchoma yeye kutokana na ugomvi wa wenzake waliokuwa wakigombana.
“Madereva hao pamoja na watu wengine walikuwa kwenye sherehe
hizo ambazo ziliandaliwa na Halima Kitwana ambazo ziliambatana na muziki
maarufu Kigodoro ulianza majira ya saa 2 usiku na baada ya muziki kwisha baada
ya saa sita kamili waliondoka lakini baadaye walionekana kumgombea mwanamke
ndipo walipomchoma mwenzao,” alisema Mwaya.
Alisema kuwa marehemu alichomwa kisu sehemu ya tumboni na
kujeruhiwa vibaya ambapo walijaribu kumkimbiza hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Tumbi kwa ajili ya matibabu lakini
alifariki wakiwa njiani.
Kwa upande wake kamanda wa Polisi mkoani Pwani Bonventura
Mushongi alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa watu waliohusika na
tukio hilo walikimbia na wanaendelea kutafutwa kujibu tuhuma za mauaji.
Mushongi aliwataka wananchi wa mkoa huo kuwa makini katika kipindi
hichi cha sherehe za kusherehekea kuukaribisha mwaka mpya kwa kutotumia vilevi
kupita kiasi ili kuepukana na matukio ya uvunjifu wa amani.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment