Na John Gagarini, Kibaha
MKOA wa Pwani unatarajia kujenga Kituo Kikubwa cha Mabasi pamoja
na Soko baada ya kupata mkopo wa zaidi ya shilingi bilioni 20 toka Benki ya
Uwekezaji ya (TIB) na kuufanya mji wa Kibaha kuwa wakisasa.
Hayo yalisemwa na mkuu wa mkoa wa Pwani alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo
na kusema kuwa kwa sasa taratibu zinaendelea baina ya Halmashauri ya Mji wa
Kibaha na benki hiyo.
Ndikilo alisema kuwa ujenzi huo unatarajiwa kuanza wakati wowote
kuanzia sasa mara taratibu za kitaalamu zitakapokamilika ambapo kwa sasa bado
zinaendelea ikiwa ni pamoja na kupata kibali .
“Tunatarajia kuwa na stendi ya kisasa ambayo thamani yake
itakuwa ni shilingi bilioni 20 pamoja na soko litakalokuwa na thamani ya
shilingi bilioni 9 hasa ikizingatiwa mkoa ulikuwa hauna soko kubwa bali lililopo
ni dogo na halina uwezo wa kuchukua bidhaa nyingi,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa wafanyabiashara wa mkoa wa Pwani hususani wale wa
makao makuu ya mkoa Maili Moja na vitongoji vyake huwalazimu kwenda kununua
bidhaa Kariakoo au kwenye masoko mengine Jijini Dar es Salaam jambo ambalo
linafanya bei za bidhaa kuwa juu.
“Kibaha ambako ndiyo makao makuu ya mkoa ni kama malango wa Jiji
la Dar es Salaam lakini bidhaa zimekuwa zikipita hapa na kwenda huko kisha
wafanyabiashara kwenda kununua na kuzirudisha hapa hivyo kupandisha bei
kutokana na gharama kuwa kubwa,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa soko hilo ambalo litajengwa sambamba na
stendi litakuwa la kisasa ambapo magari yatakuwa na uwezo wa kuingia na
kushusha bidhaa na si kama ilivyo sasa ambapo kutokana na udogo wa soko
lililopo hubidi magari ya bidhaa yashindwe kuingia.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment