Na John Gagarini, Kibaha HUKU watumiaji wa stendi kuu ya mabasi ya Maili Moja wilayani
Kibaha mkoani Pwani wakilalamika kukosekana kwa taa kwenye stendi hiyo kwa
kipindi cha miezi 10 Halmashauri ya Mji wa Kibaha imesema kuwa iko katika
harakati za kutafuta fedha kiasi cha shilingi milioni 16 kwa ajili ya
kukarabati taa hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha Mhandisi wa
Halmashauri ya Mji huo Dismas Marango alisema kuwa baadhi ya taa kwenye stendi
hiyo zimeungua hali inayofanya stendi hiyo kuwa gizani kwa kipindi chote hicho.
Marango alisema kuwa mara baada ya baadhi ya taa hizo kuungua
waliwasiliana na Temesa ambao ndiyo wanaohusika na ukarabati wa umeme na magari
ya serikali walifuatilia juu ya tataizo hilo na kugundua kuungua kwa baadhi ya
taa hizo ambazo ziko zaidi ya 10.
“Waligundua kuungua kwa taa hizo huku nyingine zikiwa hazina
mwanga mkali ambapo gharama ya kukarabati ni shilingi milioni 16 ili huduma
hiyo iweze kurejea katika hali yake ya kawaida na kuondoa adha ya watumiaji wa
stendi hiyo kuwa gizani,” alisema Marango.
Alisema kuwa gharama hizo ni kubwa sana hali ambayo
inawafanya washindwe kurejesha huduma ahiyo ya taa kwa muda sasa lakini hata
hivyo wanaendelea na michakato ya kutafuta fedha hizo ili kurejesha huduma
hiyo.
“Suala hili ni la ghafla hivyo hata bajeti yake haikuwepo
lakini tunaendelea na michakato mbalimbali ili kupata fedha hizo ili
kuhakikisha taa zinawaka na kuondoa usumbufu kwa watumiaji wa stendi wakiwemo
abiria na wale wanaofanyabiashara kwenye stendi yetu,” alisema Marango.
Aliwataka watumiaji wa stendi hiyo kuwa na uvumilivu wakati
Halmashauri ikihangaika kupata fedha kwa ajili ya kurudisha huduma ya taa kwani
hata wao wanachukizwa na hali hiyo lakini mipango inafanywa kurudisha hali ya
kawaida.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment