Na John Gagarini, Mkuranga
IMEELEZWA kuwa kuishi mbali na vituo vyao
vya kazi kwa baadhi ya maofisa
ugani kwenye vijiji wilayani Mkuranga mkoa wa Pwani kumechangia kudumaza
shughuli za kilimo wilayani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mafunzo kwenye kijiji cha
Msufini kata ya Mbezi, mratibu wa mradi wa Wajibu wa Jamii Katika Usimamizi
wa Rasilimali za Umma za Sekta ya Kilimo wilaya hiyo (POCUSO), Bw Said
Gwaja alisema kuwa maofisa hao wamekuwa hawafiki kwenye vijiji
walivyopangiwa.
Bw Gwaja alisema kuwa kutokana na kuishi mbali na vituo vyao vya kazi
wamekuwa wakiishia ofisini na kushindwa kwenda kwenye maoeneo waliyopangiwa
hasa yale ya vijijini.
“Ni vema wangekaa kwenye maeneo yao ya kazi ili iwe rahisi kwao kutoa
huduma kwa wakulima ambao wanakosa fursa nyingi kutokana na kutofahamishwa
namna ya kuweza kuzipata,” alisema Bw Gwaja.
Alisema kuwa fursa ambazo wakulima walipaswa kuzijua zinashindwa kuwafikia
kwani wanazipata wakati muda wa kilimo unakuwa umepita hivyo kushindwa kupata
pembejeo za ruzuku kwa wakati muafaka.
Aidha alisema kuwa endapo wangekuwa
wanafanya kazi kwenye maeneo waliyopangiwa hususani vijijini ingekuwa raisi
kwao kujua chanagamoto zinazo wakabili wakulima hivyo ingekuwa rahisi
kuwasaidia kuliko ilivyosasa.
Aliwataka wakulima kujitokeza kwenye
mafunzo yanayoandaliwa na shirika lake ili waweze kujua namna ya kufuatilia
matumizi ya rasilimali za wananchi zikiwemo zile za kilimo ambazo nyingine
zinawalenga wao moja kwa moja.
Mwisho.
Na Mwandishi Wetu, Mkuranga
WANANCHI wametaka katiba mpya iwe na kipengele cha
wafanyakazi wa serikali kufanya kazi kwa mkataba wa miaka 10 ili aweze
kuwajibishwa endapo utendaji kazi wake hautaridhisha.
Hayo yalisemwa jana Mkuranga na Bw Mohamed Abdul
wakati wa Mdahalo wa Katiba kwa wakazi wa Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani
uliandaliwa na Mtandao wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali wilayani Mkuranga
(MKUNGONET).
Alisema kuwa baadhi ya wafanyakazi wa serikali
wamekuwa hawatekelezi vema majukumu yao hali inayofanya washindwe kuwaletea
maenedeleo wananchi ambao wanaamini kuwa elimu walizonazo hawazitumii
kikamilifu.
“Tungetaka katiba iwe na kipengele cha wafanyakazi wa
serikali kuwa na mkataba wa miaka 10 ili akifanya vema aongezewe mkataba na
kama akifanya vibaya asiongezewe mkataba wa kazi,” alisema Bw Abdul.
Alisema kuwa endapo kutakuwa na mikataba ya muda wa
kufanya kazi kutaleta uwajibikaji sehemu za kazi tofauti na ilivyo sasa baadhi
ya wafanyakazi kutowajibika kwa kuamini kuwa hawawezi kuondolewa kazini hata kama
wameboronga.
Aidha alisema kuwa pia sifa za wataalamu
mbalimbali ziwekwe kwenye mbao za matangazo ili wananchi waweze kujua uwezo wa
wataalamu hao.
“Hii itasaidia kuwawajibisha wataalamu hao ambao
wataonekana uwezo wao ni mdogo kwani baadhi hawana uwezo,” alisema Bw Abdul.
Kwa upande wake mratibu wa MKUNGONET Bw Mohamed
Katundu alisema kuwa lengo la mdahalo huo ni kuwaelekeza namna ya kutoa maoni
yao juu ya marekebisho ya katiba mpya.
Bw Katundu alisema kuwa mdahalo huo uliofadhiliwa na
The Foundation for Civil Society ulihudhuriwa na madiwani, wataalamu toka
wilayani, mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali na wananchi.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MWANAFUNZI ambaye ni miongoni mwa wanafunzi waliofeli
kidato cha pili mwaka jana kwenye shule ya sekondari ya Tumbi wilayani Kibaha
mkoani Pwani Shaban Kihemele (16) ametoroka nyumbani kwa madai kuwa wanafunzi
wenzake kumzomea kuwa amerudia darasa.
Akizungumza na waandishi wa habari hizi mjini Kibaha
mzazi wa mtoto huyo Bw Shaban Kihemele alisema kuwa mwanae huyo huyo alitoroka
Januari 24 mwaka huu na hadi leo hajaonekana licha ya jitihada za kumtafuta
kushindwa kufua dafu.
Bw Kihemele alisema kuwa mwanae aliondoka nyumbani
majira ya saa 4 asubuhi huku akiwa amevalia kaptura nyeusi ya Jeans iliyokatwa
tisheti ya rangi ya zambarau yenye ufito mweupe kifuani na ndala nyekundu.
“Chanzo cha yeye kutoroka siku ya Januari 23
alimwambia mama yake kuwa kutokana na kufeli mtihani wa kidato cha pili ni vema
wamwamishe shule kuliko kuendelea kusoma hapo kwani wanafunzi wanaomfahamu
wanamzomea lakini mama yake alimwambia asubiri mimi nirudi kwani sikuwepo
nilikuwa Bagamoyo kikazi,” alisema bw Kihemele.
Alisema mama yake alimjibu kuwa asubiri hadi nirudi
lakini kesho yake alirudi kutoka shuleni na kubadilisha nguo huku majirani
wakimwuliza kuwa ni kwanini amewahi kurudi na anakwenda wapi akawaambia yuko
hapa hapa pia baba yake hajalipa ada hivyo amerudishwa.
“Alichukua fedha kiasi cha shilingi 20,000 kati ya
shilingi 50,000 zilizokuwepo kasha akachukua na shuka kisha kuondoka
kusikojulikana na inawezekana aliotoroka kutokana na kuona kuwa ni fedheha
kurudia darasa na madai kuwa wenzake wanamzomea jambo ambalo linatushangaza,”
alisema Bw Kihemele.
Aidha alisema siku ya kwanza walimsubiri hakutokea na
ilipofika usiku walikwenda kutoa taarifa kituo cha polisi cha Maili Moja
KMM/RB/108/2013 juu ya kutoonekana mtoto wao, walikwenda nyumbani kwao Bagamoyo
lakini hawajaweza kufanikiwa kumwona pia waliwasiliana na ndugu zao wote lakini
imeshindikana.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
DIWANI wa kata ya Picha ya Ndege wilayani Kibaha
mkoani Pwani Bw Bosco Mfundo kupitia chama cha demokrasia na maendeleo
(CHADEMA) juzi alitolewa nje kwenye kikao cha baraza la Madiwani wa halmashauri
ya Mji wa Kibaha baada ya kusema kuwa meya wa mji huo Bw Adhudadi Mkomambo ni
mwizi.
Sakata la diwani huyo maarufu kama Obama kutolewa nje
lilikuja wakati wa kikao cha madiwani kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano
wa halmashauri hiyo uliopo Kibaha.
Chanzo cha diwani huyo kutolewa nje ni kukataa kupokea
taarifa ya halmashauri na kusema kuna wizi umefanyika kwenye taarifa ya fedha
na mwenyekiti ni mwizi jambo ambalo lilimfanya meya huyo kumtaka diwani huyo
atoke nje kwa muda kabla ya kurejea na kuendelea na kikao.
“Nilikataa taarifa ya mwenyekiti wa halmashauri kwa
sababu kuna wizi umefanywa na halmashauri ya mji wa Kibahakiasi cha shilingi
milioni 533 zinaoneka zimeibwa ni wazi taarifa hii ni kuanzia mwezi Oktoba hadi
Desemba lakini inaleta matumizi ambayo yalishaletwa kwenye taarifa ya robo ya
mwaka uliopita,” alisema Bw Mfundo.
Alisema kuwa kitendo cha wao kutohoji taarifa na
kuikubali na kuridhia wizi uliofanyika hadi mwenyekiti anamtoa nje ni wazi naye
ni shemu ya wizi huo.
“Mimi ni mwakilishi wa wananchi hivyo siwezi kuridhia
kuona fedha za walipa kodi zinachotwa na kutumika kinyume cha taratibu
sikotayari,” alisema bw Mfundo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri hiyo Bw
Mkomambo alisema kuwa alimtoa kwenye kikao kwa kufuata kanuni za baraza kwa
kutoa lugha mbaya.
“Lugha aliyotumia ilikuwa inahatarisha kikao kishindwe
kuendelea na ni jambo ambalo ni kinyume kwani ni utovu wa nidhamu kutumia lugha
mabya kwenye kikao kama hicho ambacho ni cha kisheria,” alisema Bw Mkomambo.
Bw Mkomambo alisema kuwa anashangaa diwani huyo
kumwita kuwa yeye ni mwizi kwani kama kaiba kaiba nini hasa ikizingatiwa kuwa
taarifa hiyo ya fedha ilipitiwa chama chetu na chama chake kabla ya kuletwa
kwenye baraza na kama kulikuwa na hoja si wangeileta kwa maandishi juu ya hilo.
“Nawasii madiwani kufuata kanuni na taratibu na kuacha
jazba hata kama kuna jambo lazima lifuate taratibu na si kuwa na jazba kwani
wanapaswa kutetea maslahi ya wananchi ili kuwaletea maendeleo,” alisema Bw
Mkomambo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa Mkoa wa Pwani amesema kuwa kupatikana kwa
greda la kuchongea barabara kwa Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuwe changamoto ya
kukabiliana na miundombinu mibovu ya barabara za mji huo.
Aliyasema hayo kwenye uzinduzi wa greda hiloa na gari
la kuzolea uchafu ambapo taarifa yake ilisomwa na mkuu wa wilaya ya Kibaha Bi
Halima Kihemba na kusema kuwa kwa sasa hakuna haja ya kusema kuwa kuna kiporo
cha mradi wa barabara.
Alisema kuwa miradi mingi ya barabara ilikuwa inakwama
kwa sababu ya kuwa na bajeti ndogo ya kuwalipa wakandarasi kwa ajili ya kufanya
kazi hiyo lakini kwa sasa watakuwa wameondokana na kujenga barabara kwa
gaharama kubwa.
“Tunawapongeza kwa kununua greda hili ambalo lina
thamani ya shilingi milioni 528 zikiwa ni fedha za mapato yenu ya ndani, sasa
mtaondokana na kuweka viporo vya miradi ya barabara kwani sasa hivi mtakuwa
mkiweka mafuta tu na kutengeneza barabara zenu wenyewe,” alisema Bi Mahiza.
Bi Mahiza alisema kuwa mbali ya kutengeneza barabara
hizo wao wenyewe kwa gharama nafuu pia wataweza kulikodisha kwa wakandarasi
mbalimbali ndani na nje ya mkoa hali itakayosababisha kujiongezea mapato ya
halmashauri.
Aidha alisema kuwa mbali ya kununua greda hilo
changaamoto nyingine inayowakabili ni namna ya kulitunza hivyo wanapaswa kuwa
makini ili liweze kuleta manufaa kwa halmashauri na wananchi ambao sasa
wataondokana na kero ya barabara.
Akizungumzia gari la kuzolea uchafu ambalo limetolewa
kama msaada na kutoka Gotland Sweden alisema litasaidia kuboresha mazingira ya
mji huo kwani gari walilokuwa nalo mwanzo lilikuwa dogo hivyo kushindwa kumudu
uchafu uliopo.
Aliwataka wananchi kulitumia gari hilo kwa kuweka
mazingira yao katika hali ya usafi kuondokana na kero hiyo ambayo ilikuwa ni
kubwa kwa muda mrefu
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Mji
wa Kibaha Bi Lweah Lwanji alisema kuwa wamejipanga kuvitumia vyombo hivyo
katika kuboresha barabara za mji na kuuweka katika usafi ili ufanane na ile ya
Moshi na Arusha.
Mwisho.