Na John Gagarini, Kibaha
MWENYEKITI wa
Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoa wa Pwani Bi Zainabu Vullu amewataka
wanawake Mkoani humo kuimarisha vyama vyao vya kuweka na kukopa (SACCOS) ili
ziweze kuwakomboa kiuchumi.
Aliyasema
hayo mjini Kibaha wakati wa baraza la umoja huo lililoambatana na uchaguzi viongozi
wa kamati ya utekezaji ya mkoa wa Pwani.
Bi Vullu
alisema kuwa wanawake kwa kiasi kikubwa ndiyo wanaoendesha familia hivyo ni
vema wakaviimarisha vyama vyao vya kuweka na kukopa ili waweze kuboresha maisha
yao na familia zao.
“Vyama hivi
maarufu kama Vicoba vimekuwa mkombozi kwa wanawake wengi kwani zamani walikuwa
na wakati mgumu kutokana na taasisi za kifedha kuwa na masharti magumu,”
alisema Bi Vullu.
Bi Vullu
ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu kutoka mkoani Pwani alisema kuwa Vicoba
vimewasaidia wanawake na kuwafanya waweze kuwa na maisha bora na familia zao.
“Baadhi ya
mafanikio waliyoyapata wanawake kupitia vyama hivi ni pamoja kujenga nyumba,
kusomesha watoto, kuanzisha vitega uchumi na kuendesha familia zao,” alisema Bi
Vullu.
Alizipongeza
baadhi ya wilaya kwa kuweza kujiwekea akiba ambapo wilaya ya Bagamoyo
imejiwekea kiasi cha shilingi milioni 11 huku wilaya ya Kisarawe wakiwa
wamejiwekea kiasi cha shilingi milioni 5.
Aidha
aliwataka wanawake katika mkoa huo kuanzisha miradi mbalimbali ya kimaenedeleo
kwa kutumia fedha hizo za Vicoba pia wajitokeze kuwania nafasi za uongozi ndani
ya chama.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment