Tuesday, January 15, 2013

STORY ZA PWANI


Na John Gagarini, Bagamoyo
MKUU wa wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Bw Ahmed Kipozi ametaka apewe majina ya ofisa aliyetoa viwanja kwenye hifadhi ya Misitu ya Mikoko wilayani humo.
Akizungumza na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya mara baada ya zira kutembelea misitu ya hifadhi ya Uzigua na Mikoko iliyoandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Bagamoyo na kusema uharibifu uliofanyika alisema kuwa misitu hiyo imeharibiwa kwa kiasi kikubwa.
Bw Kipozi alisema kuwa inashangaza kuona maofisa hao kugawa viwanja kwenye hifadhi ya misitu badala ya kutoa viwanja kwenye maeneo yaliyotengwa maalumu kwa ajili ya viwanja.
“Siwezi kukubaliana na watu ambao hawawajibiki ipasavyo kwani inashangaza kuona kuwa watu wanatoa maeneo ambayo ni hifadhi kwani misitu ni muhimu kwa viumbe hai hivyo nataka niwajue waliofanya hivi ili hatua ziweze kuchukuliwa,” alisema Bw Kipozi.
Aidha alisema kuwa watu waliopewa viwanja kwenye maeneo hayo ya hifadhi ya mikoko wamekata miti hiyo ambapo baadhi walikata ili kuona madhari ya bahari na wengine walianzisha miradi ya samaki.
“Wameharibu hifadhi hii kwa kiasi kikubwa kwani kila mtu anaelewa umuhimu wa misitu kwani kukata miti kuna athari nyingi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mvua kuharibu mazalio ya samaki na kubadili uoto wa asili hivyo lazima wahusika wawajibike,” alisema Bw Kipozi.
Kwa upande wake meneja wa wilaya ya Bagamoyo Bw Charles Mwamfute alisema kuwa hifadhi za misitu hiyo zimeharibiwa na watu kwa ajili ya kukata miti, kuchoma mkaa na wafugaji kuingia kwenye misitu hiyo.
“Sisi wakala mpya ambao umeanzishw akwa ajili ya kulinda misitu ya asili kila wailaya hivyo hatua ya kjwanza ni kuangalia eneo ambalo limeathirika na uharibifu ambapo tutawachukulia hatua za kisheria wale waliongia kwenye hifadhi za misitu,” alisema Bw Mwamfute.
Bw Mwamfute alisema kuwa Misitu ya Uzigua zaidi ya nusu ya misitu hiyo imeharibiwa ambayo ni hekta 24,436 kwenye msitu wa Uzigua huku ile ya mikoko hekta 70 zimeharibiwa kati ya hekta zaidi ya 5,000.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Bi Mwantumu Mahiza ni moja kati ya wagombea watakaowania nafasi ya skauti mkuu wa Tanzania ambapo mchakato wa kumpata unaendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamishna mkuu wa mkoa huo Bw. Hamis Masasa alimpongeza mkuu wa mkoa wa mkoa wa Pwani kwa kuweza kujitokeza kwenye mchakato huo na kushinda nafasi ya kwanza katika mchakato wa kumpata Skauti mkuu wa Tanzania.
Alisema kuwa kutokana na kuongoza katika kinyang'anyiro hicho kwa kuwashinda kwa kura 47 huku  wagombea wengine wawili ambao wamepata kura 22 kila mmoja ambao ni Bw.Abdulkarim Shah Mbunge wa Mafia na Bw. Kajungumjuli kutoka mkoa wa Mwanza.
“Baada ya hatua hiyo majina matatu yatawasilishwa kwa Rais wa Chama cha skauti Tanzania, ambaye ni Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi Bw Shukuru Kawambwa kama utaratibu unavyoelekeza ambaye naye atayawakilisha kwa mlezi wa Chama cha Skauti Tanzania, Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt Jakaya Kikwete  ambaye yeye atakuwa na jukumu la kuchagua jina moja kati ya matatu yaliyochaguliwa ili kumpata skauti mkuu na badaye kuapishwa kwa mujibu wa taratibu,” alisema Bw Masasa.
 
Aidha alisema kuwa Bi Mahiza anauwezo wa kupanga mipango mbalimbali ya kumuendeleza kijana na mfano ni uanzishaji wa kambi ya maarifa iliyokufanyika katika kijiji cha Msoga wilayani Bagamoyo ambapo vijana walikusanywa kutoka wilaya za Mkoa wa Pwani na kupatiwa mafunzo ya ujenzi wa nyumba kwa gharama nafuu na kuwezesha vijana hao kupatiwa mashine za kufyatua tofali na mifuko 100 ya udongo ulaya.
 
Kwa hatua hiyo yeye kama kamishna wa Skauti mkoa wa Pwani kwa niaba ya skauti wa mkoa huo amechukua fursa hiyo kumpongeza mkuu huyo wa mkoa wa Pwani kwa kuweza kuongoza katika mchakato huo na hasa ikizingatiwa toka amefika mkoa wa Pwani, Agenda yake kubwa imekuwa ni maendeleo ya vijana na kuna uhakika mkubwa akibahatika kupata nafasi hiyo ataweza kusaidia vijana wa nchi nzima badala ya wale mkoa wa Pwani pekee yake.

Mwisho.
 
Na John Gagarini, Bagamoyo

KATIKA kuwajengea uwezo Vijana Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo imetenga kiasi cha shilingi milioni 75 kwa ajili ya kuwakopesha vijana wanaojishughulisha na biashara mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari mwenyekiti wa kamati ya elimu,afya, na maji katika halamshauri hiyo Bw Said Zikatimu alisema kuwa fedha hizo ni kutoka kwenye mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwakopesha vijana ambao wameunda vikundi vya ujasiriamali.

Bw Zikatimu alisema kuwa halmashauri imetenga fedha hizo kwa lengo la kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana ili kupunguza kero hiyo kwa vijana wanaojitambua kwa kuanza kijituma.

“Hadi sasa  baadhi ya kata tayari zimenufaika kwa vijana hao kuanzisha vikundi ambazo ni ikiwa ni pamoja na Zinga,Chalinze Saccos,Kerege na Kiwangwa na kuzitaka kata nyingine kuanzisha saccos ili ziweze kupata fedha hizo ambazo zimetengwa na Halmashauri,” alisema Bw Zikatimu.

Bw Zikatimu ambaye ni diwani wa kata ya Talawanda alisema kundi la vijana halina mwamko katika masuala ya kuunda vikundi vya ujasiliamali ambavyo kwasasa ndio mkombozi kwa wajasiliamali walio wengi katika maeneo mbalimbali nchini.

“Vikundi mbalimbali vikiwemo vya vijana vinasaidiwa kupata mikopo na misaada kwa urahisi mara panapotokea fursa ya ufadhili kuliko kutoa msaada kwa mtu mmoja mmoja,” alisema Bw Zikatimu.

Aidha aliwaasa vijana hao kuachana na tabia ya kukaa vijiweni kujadili masuala yasiyo na tija kwao badala ya kushauriana kuanzisha vikundi vya ujasiliamali ili kupunguza wimbi la vijana wasio na ajira wilayani humo.

Aliongeza kuwa mbali ya kundi la vijana kutengewa fungu hilo pia wanawake wametengewa kiasi cha shilingi Milioni 65 kutoka mfuko wa Women Development Fund (WDF) ambao awali ulikuwa ukitoa Milioni Kumi huku wanawake wakipewa mikopo kutokana na kuwa na sifa za yakuwa na  mwamko wa kuunda vikundi hivyo na wengi wameshanufaika navyo.

Mwisho
 

Na John Gagarini, Bagamoyo

MEYA wa Mji wa Bagamoyo mkoa wa Pwani Bw Abdul Sharif amewataka wananchi wa mji huo kutotupa takataka hovyo ili kuepukana na mlipuko wa magonjwa ya mlipuko ukiwemo ule wa kipindupindu.

Akizungumzia hofu hiyo kwa waandishi wa habari,mjini Bagamoyo ,Meya huyo alisema kutupwa ovyo kwa taka hizo kunasababisha mvua zinazoendelea kunyesha kuzisomba taka na kuweka mkusanyo wa mafungu ya uchafu.
 
Alisema kuwa kutokana na tabia ya watu kutupa taka hovyo kuna hatari ya kutokea kwa magonjwa hayo ya mlipuko hivyo hatua za dharura za kusafisha mji huo zinahitajika ili kuweka mji safi.
“Mamlaka ya mji mdogo imekuwa ikichukua jitihada za makusudi mara kwa mara kusafisha na kuzolewa taka zinazolundikwa lakini jitihada hizo zinakwama kutokana na kukosa fedha za kufanyia usafi,” alisema Bw Sharif .

Aalisema kuwa Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo imewapa jukumu la kusimamia usafi wa mji huo lakini bila kupewa nyenzo yoyote ,magari ya kubeba uchafu wala kiwango cha fedha na kupewa agizo la kushirikiana na  idara ya afya ambayo nayo imesema imebaki na kiasi cha shilingi Milioni mbili ambazo hazikidhi mahitaji .
 
“Ukosefu wa fedha unasababisha kushindwa hata kuzibua vyoo vya stendi kuu ambavyo vimekuwa vinatitirisha vinyesi katika baadhi ya makazi ya watu pale mvua zinaponyesha na soko linalotegemewa mjini humo limekuwa kama kisiwa kwa kuzungukwa na mabwawa ya maji huku hali ya ndadi ya soko ni mbaya,” alisema Bw Sharif.

Aidha alisema Halmashauri inatakiwa kutafakari namna ya kusaidia mamlaka hiyo ili kuweka mji safi kwa manufaa hasa ikizingatiwa kuwa kuna wageni wengi wanaotembelea mji huo.
Hivi karibuni Mwenyekiti wa baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo,Bw Shukuru Mbatto alisema yeye binafsi anachukua dhima ya kwenda kutembelea katika eneo hilo na kuhakikisha anakaa na Mkurugenzi mtendaji wa wilaya ya Bagamoyo ili kutatua tatizo hilo lakini hadi sasa mambo yanakwenda ndivyo sivyo.
Mwisho

Na John Gagarini, Kibaha
IMEELEZWA kuwa kitengo cha Dawati la jinsia na watoto kinakabiliwa na changamoto ya watu kuwa na mwamko mdogo kutoa taarifa juu ya unyanyasaji wa kijinsia hali inayosababisha vitendo hivyo kukithiri.

Kwa mujibu wa katibu wa Dawati hilo lililopo kwenye ofisi ya Jeshi la polisi Mkoa wa Pwani, Bi Mwamshamba Rashid alisema wakati wa mafunzo juu ya ukatili yaliyoandaliwa kikundi cha Inuka.

“Vitendo hivyo vinakithiri kwa kiasi kikubwa pembezoni mwa miji kutokana na ushirikiano hafifu hivyo kuna kila sababu ya kujenga ukaribu  ili kutokomeza vitendo hivyo,” alisema Bw Rashid.

Aidha Bi Rashid alibainisha kuwa suala hilo si la wanaofanyiwa pekee bali linaigusa jamii inayowazunguka wahusika hivyo wananchi watambue ushirikiano utasaidia urahisi wa utendaji kazi dawati hilo.
 
Kwa upande wake  Mkurugenzi wa Kikundi cha wajasiliamali cha Inuka Bw David Msuya aliipongeza serikali kwa uongozi kwa kuzingatia utawala bora na uwajibikaji uliopelekea matukio ya uhalifu mbalimbali nchini ikiwemo ujambazi kupungua.
 
Bw Msuya ambae pia ni mwanasheria wa kujitegemea alisema jitihada za dhati zilizowezesha kutokomeza matukio hayo zinalipa imani taifa kwa kuwa na imani na  serikali yao.
 
Mafunzo hayo ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia na watoto, yalifanyika Mwendapole, Kibaha na kuandaliwa na kikundi cha Inuka na kuendeshwa na dawati hilo kutoka Jeshi la Polisi Mkoani Pwani.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
KUFUATIA kuanzishwa kwa benki ya Familia ya Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Kibaha mkoani Pwani wajasiriamali wengi wamejitokeza kukopa kwa ajili ya kuendeleza shghuli zao za ujasiriamali.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake katibu wa Jumuiya hiyo Kibaha Mjini Bw David Mramba alisema kuwa hadi sasa watu zaidi ya 400 wamejitokeza kukopa fedha hizo ambazo zinatolewa kwa vikundi vya watu watano watano.
Bw Mramba alisema kuwa kwa sasa wanaendelea kupokea maombi ikiwa ni pamoja na kuwasajili ili waeze kuwa na akaunti kwa ajili ya kuwekea akiba zao.
“Malengo ni kupata watu 800 lakini kwa kasi hii watu wanaweza kufikia 1,000 ambao wanataka kukopa fedha kwa ajili ya shughuli zao za ujasiriamali,” alisema Bw Mramba.
Alisema kuwa benki hiyo ya familia ilitenga kiasi cha shilingi millioni 800 kwa ajili ya wakopaji kwenye wilaya kwa lengo la kuwainua wajasiriamali wadogo.
“Mara taratibu zitakapokamilika tutawakopesha na zopezi linaendelea vizuri kwani watu wengi wanajitokeza kutaka kukopa hasa ikizingatiwa masharti yaliyowekwa ni mepesi tofauti na sehemu zingine,” alisema Bw Mramba.
Aidha alisema kuwa changamoto kubwa wanayoipata ni baadhi ya wananchi kuwa na hofu kwani baadhi ya taasisi za kifedha ziliondoka na fedha zao.
“Lengo ni kuwainua wajasiriamali wadogo wadogo  ili nao waweze kuinua biashara zao ndiyo sababu tumeweka taratibu rahisi ili kila mtu aweze kukopa bila ya kujali chama,” alisema Bw Mramba.
Aliwataka wananchi kujitokeza kukopa kwani masharti yaliyopo ni nafuu kwa mtu yoyote kuweza kukopa ambapo riba yake ni ndogo sawa na asilimia moja tu.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment