Tuesday, January 1, 2013

UONGOZI WA KIJIJI WANGOLEWA



Na John Gagarini, Bagamoyo
SAKATA la viongozi wa Vijiji kuondolewa madarakani limezidi kushika kasi kwenye kata ya Vigwaza wilayani Bagamoyo ambapo juzi wananchi wa Kijiji cha Ruvu Darajani wameuondoa madarakani uongozi wa Kijiji hicho.
Vijiji vingine ambavyo uongozi wake umeondolewa na wananchi kwenye mikutano ya Kijiji ni Kitonga na Milo ambo wamewaondoa viongozi wao kutokana na tuhuma mbalimbali.
Wananchi wa Kijiji cha Ruvu Darajani waliukataa uongozi huo kwa tuhuma za kutoa eneo la soko kwa mwekezaji bila ya kupitishwa na wananchi ambao ndiyo wenye ridhaa ya kukubali maeno kupewa watu kwa ajili ya kuwekeza.
Uongozi huo chini ya Mwenyekiti Bw Kambona Athuman Kwaro na ofisa mtendaji wake Bi Mwajuma Bigo na wajumbe wa halmashauri ya Kijiji uliondolewa kwenye mkutano wa dharura  ambao uliitishwa kwa lengo la kuwapitisha wawekezaji walioomba maeneo  kwa ajili ya kuwekeza.
Mwenyekiti huyo bila ya kujua kilichokuwa kikiendelea alifungua mkutano na kusema kuwtaakuwa na ajenda mbalimbali lakini kubwa ilikuwa ni kuwapitisha wawekezaji hao ili wapatiwe hati za kumiliki maeneo hayo kwa kipindi watakachokuwa wamekubaliana.
Wananchi hao waliwapinga wawekezaji hao huku wakiwa na mabango wakiwataka viongozi wao kuachia ngazi na kusema kuwa mazingira ya kuwapitisha hayakuwahusisha wao hivyo hawako tayari kuwakubali kuwekeza kwenye kijiji hicho kwani kwa kipindi walioomba hawajaweza kutoa mchango ndani ya Kijiji.
“Mbali ya wawekezaji hawa wengine kilichotuudhi zaidi ni uongozi kumpa mwekezaji eti ajenge ofisi kwenye eneo ambalo lilipangwa kwa ajili ya soko na tayari kulishawekwa mabanda ambayo yameondolewa na kibaya hawajatushirikisha tunashangaa mtu kaanza kujenga,” alisema Bw Athuman Mnyamani.
Bw Mnyamani alisema kuwa maeneo mengi yametolewa kinyemela huku maeneo mengine wamewaongezea ukubwa tofauti na makubaliano ambapo hili eneo la soko walikubaliana ajenge lakini leo wanaitisha mkutano kutaka tumkubali au kumkataa wakati ameanza ujenzi kwa kuchimba msingi.
“Hapa hatuna hata maeneo ya wazi kwani yote yametolewa kwa wawekezaji ambao hatuoni manufaa yao kwani wanaahidi wakishapewa maeneo hayo hawatoi msaada wowote hivyo hawastahili kuwa viongozi ndiyo sababu ya sisi kuwakataa,” alisema Bw Mnyamani.
Akijibu tuhuma hizo mwenyekiti Bw Kwaro alisema kuwa ni kweli walikubalina na mwekezaji huyo kujenga ofisi kwa ajili ya mambo ya biashara lakini tulimwambia aanze ujenzi mwezi huu na si mwezi uliopita jambo ambalo alikwenda kinyume na kuanza kuchimba msingi.
“Tulikubaliana aanze ujenzi januari lakini yeye aliwahi na wakati anafanya hivyo mimi sikuwepo na tulimkubalia kwa nia njema hakukuwa na jambo lolote la kificho ambapo kama kijiji hakina uwezo wa kujenga hivyo tulikubaliana atakuwa akikilipa kijiji kiasi cha shilingi 100,000 kwa mwezi,” alisema Bw Kwaro.
Kutokana na majibu hayo watu walianza kupiga kelele za kusema kuwa hawana imani na uongozi huokila mtu aliyetakiwa kuuliza swali au akutoa mchango wake alikuwa akisema uongozi uondoke madarakani huku wananchi wengine wakizomea.
Kwa upande wake ofisa mtendaji wa kata ya Vigwaza Bw Masukuzi Masukuzi alijaribu kuwazuia wananchi hao kuacha makelelena  vurugu na kutoa hoja zao za msingi ili maamuzi yaweze kuwa sahihi.
“Kama mlivyoona wananchi wametoa kauli moja kuwa hawautaki uongozi na kikubwa ni tuhuma kuwa wametoa maeneo bila ya ridhaa yao likiwa hili la hapa ambapo ni makosa kwani wananchi ndiyo wenye maamuzi ya kumkubali au kumkataa mwekezaji,” alisema Bw Masukuzi.
Kutokana na wananchi kuukata uongozi inabidi nafasi hiyo kuongoza ichukuliwe aidha na mwalimu mkuu wa shule au ofisa ugani hadi pale halmashauri itakapotoa utaratibu mwingine namna ya kupata uongozi mwingine.
Wananchi hao kwa pamoja walimpitisha mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ruvu Darajani Bi Meri Nzowa kuongoza Kijiji hicho hadi utakapochaguliwa uongozi mwingine. Mkutano huo ulihudhuriwa na diwani wa kata hiyo Bw Mbegu Dilunga na mkuu wa kituo cha polisi Vigwaza Bw Salim Msangi
Mwisho.        

No comments:

Post a Comment