Thursday, January 10, 2013

WANANCHI HALMASHAURI ZAKUBALIANA


Na John Gagarini, Kibaha
HATIMAYE wakazi wa mtaa wa Tangini wilayani Kibaha mkoani Pwani wameridhia kuwekwa kalavati kwenye eneo ambalo walidai halmashauri imehamisha mkondo wa maji ya mvua na kuuelekeza kwenye makazi ya watu.
Pande hizo mbili zilifikia makubaliano baada ya mkurugenzi wa halmashauri Bi Jenifa Omolo na Injinia Bw Ezekiel Kunyaranyara kufika kwenye eneo hilo na kufikia makubaliano.
Wananchi hao walifikia hatu ya kumzuia mkandarasi wa barabara kuweka klavati hilo kutokana na kupata vitisho kutoka kwa wakazi hao.
Moja ya wakazi wa mtaa huo Bw Michael Mwambashi alisema walizuia kuwekwa kalavati kwani halmashauri ilihamisha mkondo wa maji na kuelekezea kwenye nyumba za watu badala ya kutumia mkondo wa zamani.
“Baada ya kupata ufafanuzi tumekubaliana waweke kisima kwa ajili ya kutuliza kasi ya maji kisha yaendee mbele lakini awali hawakutuambia kuwa watachimba kisima,” alisema Bw Mwambashi.
Kwa upande wake Injinia Bw Kunyaranyara alisema kuwa eneo walilokuwa wakitaka maji yapite si sahihi kwani tayari maji ya mvua yamebadilisha mwelekeo hivyo kalavati lazima liwekwe eneo jingine na si pale walipokuwa wakitaka wananchi.
“Lengo ni maji haya ya mvua yasileta madhara kwenye nyumba za watu na si kama watu wanavyofikiri na hatuna nia mbaya hata hivyo tumefikia makubaliano na wamekubali kama tulivyowashauri,”  alisema Kunyaranyara.
Naye mkandarasi wa barabara za halamshauri ya Mji wa Kibaha Bw Lebulu Mfinanga alisema kuwa baadhi ya watu wamejenga kwenye maeneo ambayo ni njia ya maji hali inayosdababisha malumbano wakati wa kujenga barabara.
Aliwataka wananchi kujenga kwa kufuata ramani ya Mji ili kuondoa migogoro kama hiyo ambayo imesababisha kuchelewa kukamilika kwa barabara ambazo amekabidhiwa na halmashauri.
Mwisho.     


No comments:

Post a Comment