Sunday, January 20, 2013

JESHI LA POLISI LATAKIWA KUDHIBITI UHALIFU NGAZI YA FAMILIA



Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoa wa Pwani limetakiwa kudhibiti uhalifu kuanzia ngazi ya familia ambako ndiko chimbuko la vitendo hivyo.
Hayo yalisemwa jana na mkuu wa mkoa wa Pwani Bi Mwantumu Mahiza alipokuwa akikabidhi pikipiki 25 kwa wakaguzi wa polisi ngazi ya Tarafa kwenye mkoa huo.
Alisema kuwa uhalifu huo ukidhibitiwa kuanzia ngazi hiyo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uhalifu na jamii zitaishi kwa amani.
“Tukianza kudhibiti ngazi ya familia itapunguza matatizo hayo na kuimarisha maendeleo na ustawi wa jamii,” alisema Bi Mahiza.
Bi Mahiza alisema kuwa pikipiki hizo zitasaidia kukabiliana na uhalifu hivyo kuna haja ya kufikia ngazi hiyo ambapo baadhi ya wahalifu wanatoka ndani ya familia.
“Mpango huu utakuwa daraja la kuunganisha kila familia katika kutambua viashiria vya vya uvunjifu wa amani pia kuwa na stadi za utatuzi wa migogoro,” alisema Bi Mahiza.
Kwa upande wake kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani Ulrich Matei alisema kuwa jeshi la polisi lilizindua mradi huo wa kuzuia uhalifu ndani ya jamii mwaka huu kitaifa.
“Wahalifu wengi hutokea ndani ya familia hivyo mkakati huu wa kifamilia katika kuzuia uhalifu utasaidia kutokomeza uhalifu,” alisema Bi Mahiza.
Kamanda Matei aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kutoa ushirikiano kwa jeshi lake ili kuweza kubaini vyanzo vya uhalifu hasa ndani ya jamii.
Na John Gagarini, Kibaha
WAKAZI wa Mkoa wa pwani hususani wa wilaya ya Kibaha wametakiwa kuwa na imani na serikali katika kutatua changamoto ya maji kwani bunge limeidhinisha kiasi cha bilioni 27 kwa ajili ya kuboresha chanzo cha maji cha mto Ruvu.
Akizungumza na wakazi wa kata ya Kongowe wilayani Kibaha mbunge wa Viti Maalumu toka mkoa wa Pwani, Bi Subira Mgalu wakati wa ziara ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na kusema kuwa changamoto hiyo karibu itapatiwa ufumbuzi.
Alisema kuwa serikali inatambua kero wanayoipata wakazi wa Kibaha kutopata maji ya uhakika licha ya chanzo cha maji kuwa kwenye wilaya hiyo.
“Serikali iko kwenye mchakato wa kulipatia ufumbuzi suala hilo na ndiyo sababu bunge limeridhia kutumika fedha hizo ili kuboresha chanzo hicho cha Ruvu ili wakazi wa Kibaha wapate maji ya uhakika,” alisema Bi Mgalu.
Alisema mbali ya kuboresha chanzo hicho pia serikali kupitia benki ya dunia ambapo awamu ya kwanza imeshakamilika sasa itaakuja awamu ya pili kwa vijiji.
“Nawataka watendaji, madiwani kuwajibika ipasavyo kwani sasa hivi si wakati wa kupoteza muda kinachotakiwa ni kazi tu na kila mmoja atomize wajibu wake ili kuwaletea maendeleo wananchi,” alisema Bi Mgalu.
Bi Mgalu ambaye ni mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM pia mkuu wa wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga alisema kuwa wakazi wa mkoa wa Pwani wanapaswa kuwapeleka watoto wao shule hususani kwenye chuo cha ufundi stadi VETA kilichopo Kongowe mkoani humo.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment