Monday, January 21, 2013

MIKOKO KUTOWEKA BAGAMOYO

WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU (TFS) WILAYANI BAGAMOYO NA MIKAKATI YA KUNUSURU MIKOKO KUMALIZWA

Na John Gagarini

KATIKA kuhakikisha misitu inalindwa hivi karibuni serikali ilianzisha Wakala wa Huduma za Misitu kwenye wilaya zote hapa nchini ili kuboresha usimamizi.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imechukua baadhi ya majukumu kutoka idara ya misitu.
TFS imepewa jukumu la kutunza misitu ya hifadhi ya Taifa (Misitu ya Asili na Mashamba ya Miti), Hifadhi za nyuki na mazao yatokanayo na nyuki.
 Majukumu ambayo TFS imeyachukua ni pamoja na kuanzisha na kusimamia hifadhi za misitu ya asili na hifadhi za nyuki zinazomilikiwa na serikali kuu, kuanzisha na kusimamia mashamba ya miti na mashamba ya nyuki yanayomilikiwa na serikali kuu.
Majukumu mengeine ni kusimamia rasilimali za misitu na nyuki katika misitu ya wazi, kusimamia utekelezaji wa sheria na kanuni katika maeneo yanayoihusu, kuendeleza watumishi, ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kutokana na mazao ya misitu na nyuki, kutunza mali na rasilimali na kutafuta masoko ya mazo na huduma ya misitu na nyuki.
TFS imegawanyika kwenye kanda mbalimbali ambapo moja ya Kanda ni ile ya Mashariki ambapo misitu ya serikali kuu wilayani Bagamoyo inaangukia kwenye kanda hiyo.
Meneja wa TFS wilayani humo Bw Charles Mwamfute anaelezea changamoto zinazokabili wilaya hiyo katika misitu ambapo ina eneo la misitu ya hifadhi lenye ukubwa wa hekta 3,883 huku misitu ya hifadhi ya Mikoko ikiwa na ukubwa wa Hekta 5,636.  
Bw Mwamfute akizungumzia hifadhi ya Mikoko ambayo iko pembezoni mwa Bahari ya Hindi kuanzia Kusini mwa Mto Mpiji hadi Kasakazini mwa mto Mlingani ambapo upande wa Mashariki ni Bahari ya Hindi na Magharibi ni bamvua (yanapoishia maji ya Bahari baada ya kujaa) kubwa la maji chumvi ya Bahari.
Alisema misitu ya hifadhi ya Mikoko ni muhimu katika uhifadhi wa viumbe hai wa baharini ikiwemo mazalia ya samaki na kuzuia mmomonyoko wa  kingo za bahari na utunzaji wa mazingira kwa ujumla.
 Alisema kuwa ndani ya eneo hilo kuna Visiwa vyenye miti isiyo ya Mikoko na maeneo hayo maji ya bamvua hayafiki ambapo misitu imezungukwa na Vijiji tisa na maeneo hayo huvamivamiwa mara kwa mara kwa kuwa si mikoko.
“Maeneo mengi yenye Mikoko yameharibiwa sana ambapo kwenye majangwa ya chumvi yana migogoro mingi ambapo wanaotumia maeno hayo hawafuati taratibu ndani ya hifadhi pia hawana hata hati miliki na kuweka Bikoni kinyume na matumizi ya hifadhi ambpo hujiongezea maeneo na kuharibu Mikoko,” alisema Bw Mwamfute.
Alisema baadhi ya athari zilizotokana na kuvunwa miti ya Mikoko ni pamoja na kukosekana mazalio ya samaki jambo ambalo linafanya samaki washindwe kuzaliana na kusababisha kitoweo hicho kuwa adimu.
Alisema baadhi ya maeneo ya hifadhi za Mikoko imekatwa na watu hao, kuchimba chumvi, kuanzisha mabwawa ya kuvua samaki huku wengine wakiifyeka misitu hiyo kwa ajili ya kuona mandhari ya bahari ikiwa baadhi ya wamiliki wa hoteli na watu binafsi.
Aliendelea kusema athari za kufyekwa misitu hiyo ya mikoko kumeanza kuonekana kwani maji yamekuwa yakifika hadi kwenye hoteli na nyumba hizo ambazo zinaonekana kuliwa na maji ya bahari kwa zilizojengwa pembeni ya Bahari.
Alisema kuwa zaidi ya hekta 70 za hifadhi ya misitu ya Mikoko imeharibiwa na watu hao wengine wakiwa ni wawekezaji ambapo katika kukabiliana na uharibifu huo wameshaanza kuchukua hatua kwa kuwapeleka mahakamani waharibifu hao pia kuanza kupanda upya miti hiyo muhimu kwa viumbe hai ambapo moja ya adhabu watakazo zipata watu hao ni pamoja na kupanda miti ya Mikoko na kuwajibika endapo miti hiyo itakatwa.
“Pia tumeanzisha kamati za utunzaji wa misitu hiyo kwenye vijiji ambavyo vinazunguka hifadhi hizo ambapo hutuletea taarifa za waharibifu hao ambao wengine huharibu misitu hiyo nyakati za usiku na kufanya ufuatiliaji kuwa mgumu,” alisema Bw Mwamfute.
Hata hivyo alibanisha changamoto kubwa inayowakabili ni idara ya ardhi kuwapatia watu ardhi kwenye maeneo ya hifadhi jambo ambalo limekuwa likisababisha uharibifu kuendelea kwani watu hao wanabainisha kuwa wanapewa maeneo hayo kihalali.
Aliongeza kuwa ramani za hifadhi hizo ziliwekwa tangu enzi za mkoloni miaka ya 50 kabla hata nchi haijapata uhuru ambapo wakoloni waliilinda misitu hiyo bila ya kuiharibu kinyume na ilivyo sasa ambapo watu wanaiharibu bila ya kuangalia athari zinazoweza kujitokeza.
“Changamoto kubwa tuliyonayo ni ushirikiano mdogo na baadhi ya taasisi ikiwemo ardhi kwenye halmashauri kwani sheria ya misitu inasema mwisho wa hifadhi ya Mikoko ni pale Bamvua linapoishia lakini watu wa ardhi wanagawa ardhi ndani ya eneo hilo ambalo liko ndani ya hifadhi,” alisema Bw Mwamfute.
Alisema changamoto nyingine ni kuwa na watumishi wachache ambapo ni watumishi wawili tu ndiyo wanaofuatilia eneo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 5,000 ya hifadhi ya Misitu ya Mikoko.
Aidha Bw Mwamfute alisema kuwa kutokana na wakala kupewa majukumu ya kusimamia msitu watatumia sheria kuwadhibiti watu wanaoharibu misitu hiyo kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria.
Kwa upande wake ofisa misitu wa wilaya ya Bagamoyo Bw Joseph Msaki alisema kuwa kikubwa kinachotakiwa ni watu kupewa mafunzo juu ya utunzaji wa misitu hiyo.
“Kitu kingine tutahakikisha tunapata ramani ya eneo la hifadhi ili kuondoa utata uliopo na kisha kuunda kamati mpya za mazingira za kila kijiji kisha kuweka sheria ndogo ndogo na kuwa na ushirikiano na sekta zingine,”  alisema Bw Msaki.
 Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya ya Mikoko katika Kijiji cha Kiharaka Bw Msafiri Kiponda alisema kuwa baaadhi ya wawekezaji wamefanya uharibifu mkubwa wa kukata mikoko wakidai kuwa wamepewa vibali na watu wa ardhi.
Bw Kiponda alisema kuwa kutokana na mitkoko kufyekwa na wawekezaji hao mazalio ya samaki hakuna hali inayowafanya wakose samaki hivyo kukosa miradi ya uhifadhi wa viumbe hai na hawatoi asilimia yoyote kwenye Kijiji kama sheria inavyowataka.
Kutokana na uharibifu mkubwa wa hifadhi ya Misitu ya mikoko na ile mingine kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Bagamoyo ikongozwa na mkuu wa wilaya hiyo Bw Ahmed Kipozi ilitembelea misitu hiyo na kujionea hali mbaya ya misitu.
Mkuu wa wilaya hiyo alitaka apewe majina ya watu waliojenga kwenye hifadhi ya misitu ya Mikoko kwani wamesababisha uharibifu mkubwa ambo hautaweza kuvumiliwa kwani athari za kuharibu misitu hiyo ni kubwa ikilinganishwa na faida itakayopatikana ni kwa watu wachache huku wengi wakiathirika kwa kuharibiwa mazingira.
Bw Kipozi alisema kuwa mbali ya kupewa majina ya watu waliojenga na kuharibu mikoko pia apewe majina ya maofisa wa ardhi toka halmashauri ambao waliwapatia watu ardhi kwenye maeneo ya hifadhi ya Mikoko na kusababisha uharibifu huo mkubwa kwa wilaya ya Bagamoyo.
Aliwataka watendaji wa halmashauri kushirikiana na wakala hao ili kuepusha kuvunwa misitu hiyo ya Mikoko kwani kugawa maeneo hayo ya hifadhi ni kuchangia kuendeleza uharibifu ndani ya hifadhi hiyo.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment