Na John Gagarini, Kisarawe
KUTOKANA na kukosa umeme zahanati ya Vikumburu tarafa ya
Chole wilayani Kisarawe mkoa Pwani inatumia vibatari kutoa matibabu kwa
wagonjwa nyakati za usiku.
Pia vibatari hivyo hutumika hata kuzalisha mama wajawazito wanaokwenda
kujifungua nyakati hizo.
Hayo yalibainishwa na baadhi ya wakazi wa kata ya Vikumburu
wakati wa ziara ya siku tatu kwenye wilaya ya Kisarawe iliyofanywa na Katibu wa
Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa Bi Amina Makilagi
Wakazi hao walibainisha kuwa ukosefu wa uememe kwenye kata
hiyo pamoja na maeneo mengine imekuwa ni changamoto kubwa kwao wanapokwenda
kupata matibabu hasa nyakati za usiku.
Kwa upande wake ofisa mtendaji wa kata ya Vikumburu Mohamed
Lusonzo alikiri kuwepo tatizo hilo na kudai kero hiyo ianatokana na kutokuwepo
kwa umeme.
Aidha alisema kuna tatizo la ukosefu wa gari la kubeba
wagonjwa la kuwapeleka kwenye hospitali ya wilaya na endapo wakihitaji gari la
wagonjwa hutakiwa kutoa kiasi cha shilingi 20,000 ya mafuta na 10,000 kwa ajili
ya muuguzi.
“Mgonjwa akizidiwa akihitaji gari la wagonjwa hutakiwa kutoa
kiasi cha shilingi 30,000 ambazo ni kwa ajili ya mafuta shilingi 20,000 na shilingi
10,000 kwa ajili ya muuguzi jambo ambalo linawapa wakati mgumu kupata fedha
hizo,” alisema Bw Lusonzo.
Kutokana na malalamiko hayo Bi Makilagi alitaka apelekewe majina
ya watumishi wanaowatoza fedha hizo wagonjwa kwani ni kinyume cha taratibu.
“Ningependa nipewe majina ya watu hao wanaotoza fedha hizo ili
hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao kwani ni kinyume cha taratibu
wagonjwa kulipishwa hela ya mafuta,” alisema Bi Makilagi.
Bi Makilagi alilaani tabia hiyo inayofanywa na baadhi ya watumishi
hao kutoza fedha wagonjwa ikizingatiwa hali ya maisha ni ngumu vijijini ambako
kipato chao ni kidogo.
Pia zahanati hiyo ya Vikumburu inakabiliwa na ukosefu wa
nyumba za watumishi ambapo watumishi wanne wamepanga chumba kimoja hali
iliyosababisha kuhamisha familia zao.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment