Thursday, January 24, 2013

ASKARI AFA AKIELEKEA KUTULIZA GHASIA

Na John Gagarini, Pwani

ASKARI wa Jeshi la Polisi mkoani Pwani Pc Dominik amefariki dunia baada ya gari alilokuwa akisafiria kupinduka baada ya tairi kupasuka.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi mkoani humo Ulrich Matei alisema kuwa askari huyo alikufa alipokuwa na wenzake wakitokea wilayani Kibaha kwenda kutuliza ghasia zilizotokea Kibiti wilayani Rufiji.

Kamanda Matei alisema kuwa askari huyo alikufa kwenye ajali ambayo ilitokea jana majira ya kuelekea mchana walipokua wakienda kwenye kutuliza vurugu hizo.

Ajali hiyo iliyotokea ilikuwa ni ya kawaida tu lakini kwa bahati mbaya tumempoteza askari huyo ambaye alikuwa akienda kuwajibika hivyo tunasikitika kutokana na hali hiyo ambayo imeleta majonzi kwa watu wengi, alisema Matei

Awali kabla ya ajali hiyo watu wanaodhaniwa kuwa ni vibaka wamechoma nyumba za polisi na kuharibu mali zao baada ya kuvamia kituo cha polisi kilichopo Kibiti wilayani Rufiji mkoani Pwani kwa madai kuwa polisi walimwua mtuhumiwa.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani Pwani Ulrich Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea jana hali iliyofanya vikosi vya jeshi hilo kwenda huko kutuliza ghasia zilizoibuka.

Kamanda Matei alisema kuwa watu hao walivamia kituo na kutaka kukichoma moto ambapo polisi waliwadhibiti watu hao ndipo walipochoma na kuharibu nyumba za polisi kwa hasira.

Idadi kamili ya nyumba zilizoharibiwa au kuchomwa moto bado haijafahamika rasmi lakini zinakaribia nne hivi na bado tunaendelea kufuatilia kujua idadi kamili za mali zilizoharibiwa na watu hao, alisema Matei.

Alisema mtu aliyekufa alikamatwa na alifia hospitali lakini hakuuwawa na polisi kama baadhi ya madai ya watu ambao waliamua kufanya fujo hizo ambazo zimesababisha hasara ambayo gharama bado haijafahamika mara moja.

Inashangaza kuona watu wanafanya uharibifu ambao hauna maana kwani hata kama mtu huyo aliuwawa na polisi ndiyo sababu ya kufanya fujo kwani huwezi ukaharibu mahakama kwa au kituo cha polisi kwani kinahusiana nini na mtu kuuwawa aliuliza kamanda Matei.

Aidha alisema kuwa tayari watu kadhaa wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo na kusema kuwa elimu inatakiwa kutolewa kwa wakazi wa eneo hilo la Rufiji kutokana na kufanya fujo mara kwa mara hali ambayo imekuwa ikivunja amani.

mwisho.





No comments:

Post a Comment