Monday, January 14, 2013

MWIZI AUWAWA


Na John Gagarini, Kibaha
WANANCHI wenye hasirakali wa Kitongoji cha Umwelani eneo la Kibaha Kwa Mathiasi mkoani Pwani wamemwua mtu anayedhaniwa kuwa ni mwizi baada ya kuvunja nyumba na kuiba.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kamanda wa Polisi mkoani humo Ulrich Matei alisema kuwa mtu huyo alikuwa na wenzake wawili ambao walikimbia mara baada ya tukio hilo.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 14 mwaka huu majira ya saa 8 usiku, ambapo watu hao walivamia nyumbani kwa Bi Mwajab Shaban (30) mfanyabiashara  wa eneo hilo.
“Watu hao walivunja nyumba hiyo kwa kutumia jiwe kubwa maarufu kama fatuma kisha kuingia ndani ndipo mlalamikaji alipopiga simu kwa majirani wakati huo wezi hao walikuwa wakiwa kwenye chumba cha watoto ndipo watu walipofika na kumkamata marehemu kisha kumpiga hadi kumwua,” alisema Matei.
Alisema kuwa watu hao walifanikiwa kuiba  na kuiba vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na fedha taslimu kiasi cha shilingi 400,000, simu mbili aina ya Techno zenye tahamani ya shilingi 100,00 na Dvd Player yenye thamani ya shilingi 65,00.
“Katika eneo la tukio kulipatikana waya wa kufyatulia baruti ambapo wezi hao hutumia kuwatisha watu kabla ya kufanya uhalifu, hata hivyo kitendo cha kumwua mhalifu si kitendo chema kwani wangempeleka kwenye vyombo vya sheria ili hatua zichukuliwe,” alisema Matei.
Aidha alisema kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye hospitali ya Tumbi kwa uchunguzi wa wa daktari na hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na mauji hayo na juhudi za kuwasaka wezi hao zinaendelea.
Aliwataka wananchi kutojichukulia sheria mkononi kwani vitendo vya kuwaua wahalifu ni kinyume cha sheria kwani watuhumiwa wanapaswa kupelekwa kwenye vyombo vya sheria.
Mwisho.
   


No comments:

Post a Comment