Thursday, January 10, 2013

HABARI MOTOMOTO TOKA PWANI


Na John Gagarini, Bagamoyo
KUFUATIA wakazi wa Kijiji cha Ruvu Darajani wilayani Bagamoyo kuuondoa madarakani uongozi hatimaye tume ya watu sita imeundwa kuchunguza tuhuma zinazoukabili uongozi huo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mkuu wa wilaya hiyo Bw Ahmed Kipozi alisema tume hiyo imepewa muda wa wiki mbili ili kutoa majibu juu ya uongozi huo.
Bw Kipozi alisema kuwa tume hiyo itachunguza baadhi ya tuhuma ikiwa ni pamoja na kuuza eneo la umoja wa wauza mboga mboga wa Ruvu, kuingia mikata na wawekezaji isiyokuwa na masalahi na wananchi ikiwa ni kinyume cha taratibu, ubadhirifu wa fedha na uongozi kujihusisha na uingizwaji ngombe kinyume cha taratibu.
“Tume hii itaundwa na maofisa mbalimbali wakiwemo wale wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamaba na Rushwa (TAKUKURU), mkagazi wa wa hesabu wa ndani, ofisa ardhi, ofisa anayehusika na Vijiji na ofisa usalama,” alisema Bw Kipozi.
Alisema kuwa tuhuma hizo endapo zitabainika viongozi hao watachukuliwa hatua za kisheria kutokana na makosa endapo yatakuwepo.
“Wananchi walikuwa na hoja za msingi kwani kwa sasa wameamka na kujua namna ya kuhoji jinsi gani rasilimali zao zinavyotumika hivyo lazima viongozi wazingatie taratibu za uongozi,” alisema Bw Kipozi.
Aidha alisema kuwa wananchi wana haki ya kuhoji pale wanapoona mali zao zinatumika vibaya na milango iko wazi kwenye ofisi yake kwa wananchi ambao wanaona kuwa kuna mambo ambayo yanakwenda kinyume.
Alisema kutokana na tatizo hilo umeteuliwa uongozi wa muda ambapo Bw Ramadhan Kondo ataongoza kama mwenyekiti na Jama Ramadhan atakuwa ofisa mtendaji wa kijiji hadi uchunguzi utakapokamilika.
Mwisho.
Na John Gagarini, Bagamoyo
WILAYA ya Bagamoyo mkoani Pwani inawafuatilia watu 11 ambao wako kwenye mtandao wa wanaowatishia watu kuwa maeneo wanayoishi ni mali yao kwenye baadhi ya Vijiji.
Mtandao huo ambao hutwaa maeneo makubwa ya Vijiji hivyo na kuyauza hali ambayo imekuwa ikileta mtafaruku kwa wakazi hao.
Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya hiyo Ahmed Kipozi alisema kuwa majina ya watu hao wanayo na kwa sasa wanaendelea kuwafuatilia ili kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
“Mtandao huu ni wa watu waishio Jijini Dar es Salaam wenye asili ya Bagamoyo wamekuwa wakifanya vitendo hivyo ambavyo ni vya kitapeliwa kwa kuyachukua maeneo ya watu wakidai kuwa yaliachwa na mababu zao jambo ambalo si la kweli,” alisema Bw Kipozi.
Aidha alisema kuwa watu wanaotaka kununua maeneo au mashamba lazima wafuate taratibu za kisheria ili kukabiliana na matapeli hao ambao wanamtandao mkubwa unaowahusisha baadhi ya viongozi wa vijiji.
“Mtandao huo umekuwa ukitumia vyombo vya habari kuhalalisha utapeli wa maeneo na mashamba ya watu kwa kudai kuwa wao ni wamiliki wa maeneo husika,” alisema bw Kipozi.
Alitaja baadhi ya vijiji ambnavyo vimekumbwa na mtandao huo wa kutapeli mashamba ya watu kuwa ni pamoja na Talawanda, Masuguru na Msoga.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
SERIKALI wilayani Kibaha mkoa wa Pwani imetakiwa kuwadhibiti matapeli wa viwanja ambao wamekuwa wakiwaibia watu kwa kuwauzia viwanja ambavyo ni mali za watu wengine.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mchungaji kiongozi wa Kituo cha Maandiko kilichopo wilayani Kibaha Gervase Masanja alisema kuwa matapeli hao wamekuwa wakitapeli watu lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi yao.
Mch Masanja alisema kuwa watu hao ambao wanajihusisha na vitendo hivyo wamekuwa wakitumia fedha kupindisha sheria pale wanapopelekwa kwenye vyombo vya sheria.
“Tunashangaa watu hawa kuendelea kutapeli watu lakini hawachukuliwi hatua zozote hata pale wanapopelekwa kwenye vyombo vya sheria tunaomba serikali iwashughulikie kwani wanafahamika,” alisema Mch Masanja.
Mch Masanja alisema kuwa hata yeye mwenyewe alitapeliwa kiasi cha shilingi milioni 2.3 kwa kuuziwa kiwanja ambacho ni mali ya mtu hata alipompeleka kwenye vyombo vya sheria malalamiko yake yaliondolewa na kupoteza fedha zake.
“Mambo kama haya ndiyo yanayoichafua serikali na kuonekana kama vile inawakumbatia watu hao ambao wamekuwa wakiwaumiza wananchi,” alisema Mch Masanja.
Aliitaka serikali kuwachukulia hatua kali baadhi ya viongozi wa vijji na mitaa kwa kushirikiana na matapeli hao katika kuwadhulumu wananchi kwani ofisi zao hutumika kufanya makubaliano ya mauzo ya maeneo.
Mwisho.          
Na Mwandishi Wetu, Kibaha

KUFUATIA aliyekuwa mgombea wa nafasi ya uenezi wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bw Suleiman Ndombogani kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa kimepata mpiganaji na si mzigo kama wanavyodai CCM.

Akizungumza na gazeti hili mjini Kibaha mwenyekiti wa Baraza la Vijana (BAVICHA) mkoa wa Pwani Bw Elison Kinyaha alisema kuwa chama hicho kimelamba dume kumpata mwanachana huyo.

Bw Kinyaha alisema kuwa Bw Ndombogani ni mtu makini na atakiletea ushindi chama hicho kwenye uchaguzi ujao na CCM wataona umuhimu wake.

“CCM wamesema kuwa huyu ni mzigo lakini kwetu ni sawa na almasi na fisi anapokosa anasema sizitaki mbichi hizi,” alisema Kinyaha.

Aidha alisema kuwa Bw Ndombogani ambaye ni mwandishi wa habari atakuwa ni mwenezi wa habari za chama hivyo watu kukijua ipasavyo.

Alisema kuwa moja ya changamoto ambayo wanataka ifanyiwe kazi ni kukuza soko la mkulima kwenye mkoa huo ambao una chanagamoto nyingi za kimaendeleo.
“Tunatarajia kuwapatia mafunzo vijana juu ya kujua haki zao za msingi ili waweze kujikwamua na changamoto mbalimbali zinazowakabili,” alisema Bw Kinyaha.

Aliwataka wanachama katika wilaya hiyo kuhakikisha kuwa wanajipanga kwenye chaguzi zijazo ili waweze kuongoza kwenye nafasi mbalimbali.

Mwisho.        




Na John Gagarini, Kibaha
BENKI ya Familia kupitia Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa imetoa kiasi cha shilingi bilioni 10 kila mkoa kwa ajili ya uanzishwaji wa benki.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha mkurugenzi wa benki hiyo Bw Dauda Salmin alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa benki hizo ni kuiwezesha jamii kuondokana na umaskini kwa kukopa kwa masharti nafuu.
Bw Salmin alisema kuwa uanzishwaji wa benki hizo utakuwa kwenye mpango wa operesheni jamii kukabiliana na watu wasio kuwa na ajira ili waweze kupata mikopo kwa ajili ya mitaji ya kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali bila ya kujali itikadi ya chama cha siasa.
“Jumuiya iliamua kuanzisha benki hizo ambazo zitakuwa zikitoza riba ya asilimia 1.6 kwa kila mkopo ambapo ni ndogo ukilinganisha na taasisi nyingine za kifedha ambazo ziko kibiashara zaidi na  mbali ya kuweka riba kubwa pia zinaweka masharti magumu mfano kutoa hati ya nyumba au gari hali inayosababisha watu wengi kushindwa kukopa hasa wale wenye mitaji midogo,” alisema Bw Salmin.
Aidha alisema kuwa mikopo hiyo itatolewa kwa vikundi vya watu watano watano ambao kila mmoja atakopeshwa kiasi cha shilingi 500,00 na kila familia ambao ndiyo wakopaji lazima iwe na shughuli ambayo inaingiza kipato si chini ya shilingi 7,500 kwa siku na marejesho yatakuwa kwa kipindi cha miezi sita.
“Benki hizo ambazo zitakuwa kila kata tayari zimeshaanza kufanya kazi kwenye mkoa wa Dar es Salaam na sasa wanatarajia kuanza kutoa mikopo kwenye mkoa wa Pwani na wakopaji wataunganishwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya kukabiliana na majanga mbalimbali,” alisema Bw Salmin.
Alibainisha kuwa changamoto kubwa wanayoipata ni wakopaji wengi kuonekana kutaka kukopa kiwango kidogo cha fedha tofauti na ile iliyopangwa na watakaonufaika na mikopo hii ni wajasiraiamali wadogowadogo kama vile mama lishe, wenye magenge, waendesha bodaboda na wengineo.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment