John
Gagarini, Mkuranga
WANANCHI
wametaka katiba mpya iwe na kipengele cha wafanyakazi wa serikali kufanya kazi
kwa mkataba wa miaka 10 ili aweze kuwajibishwa endapo utendaji kazi wake
hautaridhisha.
Hayo
yalisemwa jana Mkuranga na Bw Mohamed Abdul wakati wa Mdahalo wa Katiba kwa
wakazi wa Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani uliandaliwa na Mtandao wa Mashirika
yasiyo ya Kiserikali wilayani Mkuranga (MKUNGONET).
Alisema kuwa
baadhi ya wafanyakazi wa serikali wamekuwa hawatekelezi vema majukumu yao hali
inayofanya washindwe kuwaletea maenedeleo wananchi ambao wanaamini kuwa elimu
walizonazo hawazitumii kikamilifu.
“Tungetaka
katiba iwe na kipengele cha wafanyakazi wa serikali kuwa na mkataba wa miaka 10
ili akifanya vema aongezewe mkataba na kama akifanya vibaya asiongezewe mkataba
wa kazi,” alisema Bw Abdul.
Alisema kuwa
endapo kutakuwa na mikataba ya muda wa kufanya kazi kutaleta uwajibikaji sehemu
za kazi tofauti na ilivyo sasa baadhi ya wafanyakazi kutowajibika kwa kuamini
kuwa hawawezi kuondolewa kazini hata kama wameboronga.
Aidha alisema
kuwa pia sifa za wataalamu mbalimbali
ziwekwe kwenye mbao za matangazo ili wananchi waweze kujua uwezo wa wataalamu
hao.
“Hii
itasaidia kuwawajibisha wataalamu hao ambao wataonekana uwezo wao ni mdogo
kwani baadhi hawana uwezo,” alisema Bw Abdul.
Kwa upande
wake mratibu wa MKUNGONET Bw Mohamed Katundu alisema kuwa lengo la mdahalo huo
ni kuwaelekeza namna ya kutoa maoni yao juu ya marekebisho ya katiba mpya.
Bw Katundu
alisema kuwa mdahalo huo uliofadhiliwa na The Foundation for Civil Society
ulihudhuriwa na madiwani, wataalamu toka wilayani, mashirika mbalimbali yasiyo
ya kiserikali na wananchi.
Mwisho.
Na Mwandishi
Wetu, Mkuranga
WATU wenye
ulemavu wametaka kuwe na mchakato wa kuwapata wabunge wanaowakilisha kundi hilo
ili kila moja liwe na mwakilishi wake tofauti na sasa kuwa na mwakilishi mmoja
ambaye hawezi kutoa mawazo ya makundi mengine.
Akizungumza wilayani
Mkuranga kwenye mdahalo wa katiba ulioandaliwa na mtandao wa mashirika yasiyo
ya kiserikali wilayani Mkuranga (MKUNGONET) Ester Waziri alisema kuwa wabunge
wanaochaguliwa kwa ajili ya uwakilishi watu wenye ulemavu uwakilishi wake bado
unalegalega.
Waziri alisema
kuwa kuna karibu iana tano za watu wenye ulemavu lakini uwkailishi unakuwa wa
kundi moja huku mengine yakiwa yamesahauliwa.
“Tungependa
katiba ionyeshe kila kundui kuwa na uwakilishi bungeni kwani kila moja lina
mahitaji yake na vipaumbele vyake,” alisema Waziri.
Alitaja baadhi
ya makundi hayo ni kama vile walemavu wa viungo, ngozi, wasioona, viziwi, bubu
na wengineo ambao kila mmoja ana mahitaji yake.
“Kila kundi
ni vema lingekuwa na mwakilsihi wake bungeni kuliko mmoja kuwakilisha makundi
yote hivyo mengine kushindwa kuwekewa mazingira mazuri ya kupata fursa mbalimbali
za kimaendeleo,” alisema Waziri.
Mratibu wa
shirika hilo Mohamed Katundu alisema kuwa waliamua kuandaa mdahalo huo ili
wananchi wajue namna ya kutoa maoni yao juu marekebisho ya katiba mpya kwenye
mchakato unaoendelea.
Mwisho.
Na John
Gagarini, Kibaha
KATIKA
kuihamsisha jamii wilayani Kibaha mkoani Pwani kushiriki kwenye michezo wadau
wa michezo wameanzisha klabu ya mazoezi ijulikanayo kama Kongowe Jogging Club.
Akizungumza na
mwandishi wa habari hizi mjini hapa moja ya waanzilishia wa klabu hiyo Simon
Mbelwa alisema kuwa lengo la kuanzisha klabu hiyo ni kuwahamasisha watu
kushiriki michezo kwani mbali ya kutoa burudani pia ni ajira.
Mbelwa ambaye
pia ni mwamuzi wa ligi Kuu ya Voda Com alisema kuwa tayari wana wanachama 18 na
tayari wameshaanza mazoezi ambayo hufanyika kila siku ya Jumamosi na Jumapili.
“Michezo hapa
bado haijahamasishwa vya kutosha hivyo wao kama wadau wameona njia mojawapo ni
kuanzisha klabu hiyo ambayo itayahusisha michezo mingi kama vile soka, mpira wa
pete, riadha na michezo mingine,” alisema Mbelwa.
Alisema kuwa
jamii imekuwa haina mwamko wa michezo hivyo wao watashirikiana na wadau wengine
kuhakikisha michezo inakuwa kwenye wilaya ya Kibaha
“Wataalamu wa
michezo hiyo wapo nikiwemo mimi mwenyewe ambapo nitafundisha michezo mingi kama
soka na mingne pia walimu wa michezo mbalimbali tayari tumeshwapata hivyo
wapenda michezo wajitokeze kutuunga mkono,” alisema Mbelwa.
Alisema changamoto
kubwa ni ukosefu wa vifaa kwa wanamichezo wa klabu yao na kuwataka wafadhili
mbalimbali kujitokeza kuwasaidia ili waweze kufanikisha michezo.
Aliwataka wazazi
kuwaruhusu watoto wao kujitokeza kushiriki michezo kwani ni moja ya njia za
kupata ajira na kuboresha afya zao na kuondokana na magonjwa madogomadogo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment