Na John Gagarini, Kibaha
WANAFUNZI 12 wa shule ya Sekondari ya Kata ya Maili Moja wilayani Kibaha mkoani
Pwani wamekamatwa na mgambo wa kata hiyo wakiwa vichakani huku wengine
wakikutwa na kondomu kwenye mifuko yao.
Tukio hilo lilitokea juzi mjini Kibaha baada ya
mgambo hao kuendesha opereshani kuwakamata wanafunzi ambao hawaingii madarasani
na kuishia njiani.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi
ya Kata ya Maili Moja mara baada ya kukamatwa wanafunzi hao, diwani wa kata Bw Andrew
Lugano alisema kuwa zoezi hilo ni endelevu kwani baadhi wanafunzi wamekuwa
hawafiki shuleni.
“Baada ya kuona kuwa wanafunzi wamekithiri kwa
utoro shule ileta suala hili ngazi ya kata na sisi tliamua kuchukua hatua
kuwatuma mgambo kuwasaka wanafunzi ambao hawaingii madarasani tulifanikiwa
kuwakamata wanafunzi hao ambao ni wa kidato cha tatu na nne,” alisema Bw
Lugano.
“Tuliwapekua ambapo tuliwakuta na baaadhi ya
vitu ikiwemo ni pamoja na simu na kondomu jambo ambalo ni kinyume cha taratibu
za shule na kesho baraza la kata litakaa pamoja na wazazi wao ambao
tumewaandikia barua ili waje na ndipo maamuzi yatatolewa dhidi yao,” alisema Bw
Lugano.
Aidha alisema kuwa kata itahakiksha wanafunzi
wa shule hiyo wanazingatia maadili ya shule na kuachana na vitendo ambavyo ni
kinyume na maadili na wataendeleza operesheni hiyo ili kusafisha shule hiyo ili
itoe matokeo mazuri.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule hiyo
Flora Chibululu alisema kuwa shule yao imekuwa ikidhibiti wanafunzi ambao
hawafiki shuleni lakini imekuwa ngumu kwani licha ya kutoa adhabu lakini bado
wanafunzi hao hawabadiliki.
Bi Chibululu alisema kuwa wamekuwa wakitoa
adhabu zikiwemo za kuwataka wakae nyumbani kwa muda Fulani lakini bado vitendo
hivyo bado vinaendelea hali iliyosababisha kuomba kusaidiwa na kata hiyo ambayo
iliwapa mgambo kufanya hivyo.
Aliwataka wazazi kutoa ushirikiano kwa shule
ili wanafunzi waweze kupata elimu bora kwani vitendo hivyo vinasababisha elimu
kushuka kutokana na wanafunzi kutojituma na kufanya matokeo kuwa mabaya.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
TIMU ya soka Lisborn ya Kongowe wilayani Kibaha
imeifunga timu ya Veteran kwa magoli 3-0 kwenye mchezo wa kuwania ngombe wa
Mbepo Cup.
Mchezo huo ulipigwa jana kwenye uwanja wa
Mwendapole wilayani Kibaha mkoani Pwani ulikuwa mkali na wa kuvutia na
kuwakusanya mashabiki wengi akiwemo Diwani wa Kata ya Kibaha Said Nangurukuta
na Meya wa Mji wa Kibaha Adhudadi Mkomambo.
Washindi walipata mabao hayo kupitia kwa
mshambuliaji wao mahiri Kulwa Mwanda akishirikiana na Jesse Joseph Magoli.
Kulwa alifunga magoli hayo kwenye dakika za
22,64 na 72, michuano hiyo itaendelea Januari 26 mwaka huu kwa mchezo baina ya
Mwanalugali na Cargo.
Kutokana na matokeo hayo timu za Nyumbu, Kigogo
na Palasupalasu zimefanikiwa kuingia hatua ya robo fainali.
Akiongelea mashindano hayo diwani wa kata ya
Kibaha Nangurukuta alisema kuwa mashindano hayo yamefanikiwa kukusanya vipaji
vya vijana kwenye kata hiyo na zingine na wilaya ya Kibaha.
Nangurukuta aliwataka wakazi wa eneo hilo
kujitokeza kwa wingi ili kuwahamasisha vijana wao kushiriki michezo na kukuza vipaji
vyao kwani mbali ya kuboresha afya pia ni ajira kwao.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment