Saturday, December 29, 2012

JUMUIYA YA WAZAZI KUTUMIA MAWAKILI KUREJESHA MALI ZAKE PWANI

Na John Gagarini, Kibaha

JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Pwani imesema kuwa imeandaa mawakili ili kuhakikisha mali zote za Jumuiya hiyo zilizouzwa au kuchukluliwa kinyume cha sheria zinarudi.
Hayo yalisemwa jana na mwenyekiti wa mkoa wa jumuiya hiyo Bw Jackson Josian wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua semina juu ya uajasiraiamali kwa viongozi wa Jumuiya Kibaha Mjini.
Alisema kuwa Jumuiya hiyo ina mali nyingi ambazo baadhi zimechukuliwa au kuuzwa kinyume cha sheria jambo ambalo linafanya washindwe kujitegemea licha ya kuwa na rasilimali na tayari wameshawapata mawakili ili kurejesha mali hizo kisheria.
“Tuna rasilimali nyingi ambazo tunatarajia kuzirejesha kwani nyingine zimeporwa lakini tutahakikisha kuwa mali zote zinarudi mikononi mwetu ili kujenga uchumi wa Wazazi na chama kwa ujumla,” alisema Bw Josian.
Alizitaja baadhi ya mali za Jumuiya kuwa ni pamoja na shule, viwanja na mashamba ambapo baadhi ya viongozi wa Jumuiya hiyo wamehusika kusababisha mali hizo kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Jumiya ya Wazazi Kibaha Mjini Dkt Athuman Mokiwa alisema kuwa moja ya lengo la semina hiyo ni kuwafundisha juu ya kulinda mali za Jumuiya.
Dkt Mokiwa alisema kuwa viongozi wengine wameshindwa kabisa namna ya kusimamia miradi ya Jumuiya hiyo na kuifanya mingine iyumbe ambapo ingesimamiwa vema ingekuwa mkombozi ndani ya chama.
Mwisho.         

No comments:

Post a Comment