Na John Gagarini, Bagamoyo
WAFUGAJI wote waliovamia kwenye vijiji mbalimbali kwa
ajili ya malisho ya mifugo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wametakiwa kuondoka
ili kuepusha migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
Hayo yalisemwa na Meya wa Mji Mdogo wa Bagamoyo Bw
Abdul Sharifu kwenye Kijiji cha Kwamduma wakati wa ziara yake kutembelea wilaya
hiyo kubaini changamoto zinazowakabili wakazi wa wilaya hiyo, kupitia Jumuiya
ya Wazazi (CCM) ya wilaya.
Bw Sharifu alisema kuwa kero ya wafugaji kuingia
wilayani humo imekuwa kubwa na kusababisha migogoro kutokana na wafugaji
kulisha mifugo kwenye mashamba ya wakulima.
“Kuanzia sasa wale wafugaji wote walioingia katika
wilaya hii kwa ajili ya kutafuta malisho waondoke ili kuepusha vurugu ambazo
zimekuwa zikitokea mara kwa mara kwa mazao kuharibiwa na mifugo hiyo,” alisema
Bw Sharifu.
Alisema kuwa kila kijiji alichotembelea kilio kimekuwa
ni wafugaji ambao wamekuwa wakiingiza makundi makubwa ya mifugo hasa ngombe
wakitokea mikoa mingine.
“Huko tunakoelekea hali ya amani inaweza kuvurugika
kutokana na ngombe kuharibu mazao ya wakulima ambapo wafugaji ambao wamevamia
wilaya hii wakitafuta malisho lakini hata hivyo hawathamini wakulima,” alisema
Bw Sharifu.
Meya huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya
Wazazi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo alisema kuwa suala
la mifugo ndani ya wilaya hiyo limekuwa chanagamoto kubwa kwa viongozi wa
wilaya hiyo.
Aidha alisema katika kukabuilina na changamoto hiyo
halmashauri imeanzisha mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa baadhi ya vijiji
ambapo yametengwa maoeneo ya wakulima na wafugaji.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment