Saturday, December 29, 2012

CHENCHI DOLA KUKARIBISHA MWAKA MPYA


Na John Gagarini, Kibaha
BONDIA machachari anayechipukia wa Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani Zumba Nkukwe (Chenchi Dola) anatarajia kuzikipiga na bondia Maisha Samson wa Mbeya mwaka mpya Januari Mosi 2013.
Chenchi Dola alisema kuwa yuko sawasawa kwa ajili ya pambano hilo ambalo litapigwa wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha jana alisema kuwa hana wasiwasi na bondi huyo kwani amefanya mazoezi ya kutosha chini ya mwalimu wake aitwaye Poti ambapo mazoezi yake amekuwa akiyafanya Jijini Dar es Salaam.
“Nimejiandaa vya kutosha na siogopi bondia yoyote kwani nimejiandaa ipasavyo na hata raundi ya tatu hatafika ijapokuwa yeye atakuwa yuko nyumbani mbele ya mashabiki wake,” alisema Chenchi Dola.
Alisema kuwa watu wa Kyela wanatakiwa wajipange sawa sawa kupata burudani ya nguvu siku ya kufungua mwaka wa 2013 na ndipo anapoanza safari yake ya kuapambana na mabingwa waliopo sasa.
“Malengo yangu ni kuja kupambana na mabondia wakubwa wanaotamba kwa sasa ili tuweze kwenda sawa kwani malengo yangu ni kuwa bingwa kwani nitajiweka sawa ili nije kupambana na bondia mmoja wapo maarufu,” alisema Chenchi Dola.
Kwa upande wake meneja wa bondia huyo Ibrahim Kame kutoka TPBO alisema kuwa lengo la pambano hilo ni kutafuta mshindi ambaye atashiriki kwenye mashindano mbalimbali ili kujiongezea uzoefu.
“Bondia Chenchi Dola ni mzuri na natarajia atafanya vizuri na kumshinda mpinzani wake na baadaye tutamtafutia mapambano mengi zaidi ili aweze kuonyesha kipaji chake,” alisema Kame.
Aliongeza kuwa katika pambano hilo mabondia wakongwe kama vile Rshid Matumla “Snake Boy” na Maneno Oswald “Mtambo wa Gongo” watakuwepo kuangalia vijana wanavyopambana.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment