Wednesday, December 12, 2012

MTOTO ATOKWA UVIMBE KICHWANI

MTOTO Fred Wiliam (4) ambaye ana uvimbe kichwani kwenye shavu hadi shingoni akiwa amekaa huko nyumbani kwao kijiji cha Mizuguni wilayani Kibaha Vijijini Mkoani Pwani Picha na John Gagarini.



Na John Gagarini, Pwani 

MTOTO Fred Wiliam mwenye umri wa miaka (3) anaishi kwenye hali ngumu kutokana na kutokwa na uvimbe kichwani ambao unamsababishia maumivu makali na kumsababisha kukosa raha kwa muda mwingi.

Mwandishi wa habari hizi alifika kijijini hapo akiwa na baadhi ya viongozi wa chama cha albino Tanzania (CCT) mkoa wa Pwani kwa lengo la kufanya sensa na mahitaji ya watoto wenye ulemavu kwenye kata ya Magindu iliyofadhiliwa na shirika la Plan International tawi la Kibaha.

Mtoto huyo anaishi katika Kijiji cha Mizuguni kata ya Magindu mbali ya kuwa na maumivu hayo pia anapata maumivu mengine ya kumpoteza mama yake mzazi ambaye alifariki mwaka jana hivyo kumwongezea simanzi kubwa.

Anaonekana kuwa ni mchangamfu huku akicheza na wenzake pamoja na kaka yake ambaye alimleta kwa mwandishi baada ya kuambiwa kuwa kuna mtoto ana matatizo ya kutoka uvimbe kwenye kichwa chake hali ambayo alizaliwa nayo.

Mtoto huyo yuko kwenye wakati mgumu kwani mama yake alifariki dunia na kumwacha akiwa bado mdogo huku akiwa na uvimbe huo na hali ni mbaya sana kwani wakati mwingine anapata maumivu makali na kuishia kulia tu

Baba wa mtoto huyo ni mkulima pamoja na kuchoma mkaa humwacha muda mwingi peke yake akiwa amekwenda kwenye shughuli zake hizo za kujiongezea kipato cha familia yake ya watoto wanne.

Kwa upande wa baba yake aliyejitambulisha kwa jina la Bw Wiliamu Joseph (30) alisema kuwa mwanae alizaliwa akiwa na uvimbe kichwani na baada ya kuzaliwa hivyo walimpeleka kwenye hospitali iyopo Kijijini hapo ambapo walishindwa na kumpeleka hospitali Teule ya Tumbi lakini hata hivyo nao walishindwa.

Amesema ilibidi wammpeleke Jijini Dar es Salaam Msasani kwenye hospitali ya CCBRT ambapo alifanyiwa operesheni kutoa uvimbe huo mara mbili miaka miwli mfululizo lakini kwa mwaka jana mwezi wanne mama yake alifariki hivyo alishindwa kumpeleka

Amesema kwa mwaka huu anatarajia kumpeleka tena ambapo kwa gharama ya watoto ni bure ila gharama za yeye kumhudumia wakati wa matibabu ni kiasi cha kama sh 70,000 ambazo inambidi kuzitafuta ndipo akatibiwe.

Amesema kuwa tatizo ni uwezo wake kuwa ni mdogo kwa ajili ya matumizi hayo na kuacha nyumbani kwa familia yake na inambidi achome mkaa na kilimo ili kuweza kulisha familia yake.

Amewaomba watu mbalimbali kujitokeza kumsaidia ili kumpeleka mtoto huyo akapatiwe matibabu aweze kurudia katika hali yake ya kawaida kwani kwa uvimbe wa mwanzo uliotolewa hali imekuwa nzuri.

Katibu wa chama hicho cha albino mkoa wa Pwani Bi Aichi Ngure alisema kuwa watoto wenye ulemavu wamekuwa wakikosa matibababu kutokana na jamii kuwa na mtizamo mbaya juu ya watoto hao hivyo kuwaficha.

Bi Ngure alisema kuwa serikali na wadau wengine wanapaswa kutupia macho vijijini ili kuangalia changamoto zinazowakabili watoto zikiwemo za afya, elimu na maji

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha albino mkoani Pwani Bw Thomas Diwani amesema kuwa watoto wenye ulemavu vijijini ni wengi sana na wamekuwa wakikosa huduma za afya na elimu.

Bw Diwani amesema kuwa jamii inapaswa kuzisiadia familia zenye watoto wenye ulemavu ili wapate matibabu na elimu ambavyo ni vitu vya msingi katika maisha ya kawaida ya kila siku.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment