Na John Gagarini, Kilwa
RAISI wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete ameutaka uongozi wa halmashauri ya
wilaya ya Kilwa mkoani Lindi kuwachimbia visima viwili wakazi wa Kijiji cha
Marendego ambapo katika mpango wa uchimbaji wa visima 69 kijiji hicho
hakikuwekwa licha ya kuwa na changamoto ya maji.
Alitoa agizo
hilo juzi kwa mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa Bw Ado Mapunda wakati
anasalimiana na wakazi wa Kijiji hicho kilicho jirani na wilaya ya Rufiji mkoa
wa Pwani akirejea Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokuwa ziarani mkoani Lindi.
Raisi Kikwete
alimtaka mkurugenzi huyo kuhakikisha visima hivyo vinachimbwa na mkuu wa mkoa
wa Pwani Bi Mwantumu Mahiza atasimamia kuhakikisha suala hilo linakamilika ili
kukabiliana na changamoto hiyo ya maji.
Awali mwenyekiti
wa Kijiji hicho Bw Omary Mtungunyu alisema kuwa kwa sasa wanategemea kupata
maji kutoka kwenye mashimo yaliyochimbwa na kampuni ya ujenzi wa barabara ya
Kusini ya Kharafi ambapo visima viwili vilivyopo havitoi maji.
“Hatuna
vyanzo vingine vya maji hali ambayo imekuwa ni changamoto kubwa kwetu ambapo
watu wanaofanya biashara ya kuuza maji safi huuza kiasi cha shilingi 500 hadi
1,000 kwa dumu la lita 20,” alisema Mtunyungu.
Kutokana na
ombi hilo Raisi Kikwete alimwita Bw Mapunda na kumtaka kuelezea mikakati
waliyonayo ya kukabiliana na changamoto hiyo ya maji kwa Kijiji hicho ambapo
alisema kuwa kijiji hicho hakimo kwenye mpango wa uchimbwaji wa visima 67
katika halmashauri hiyo.
“Kutokana na
heshima yako Raisi tutawachimbia visima hivyo viwili lakini hawakuwepo kwenye
mpango huo wa kuchimbiwa visima kukabiliana na tatizo la maji katika
halamshauri hiyo,” alisema Bw Mapunda.
Kufuatia Bw
Mapunda kusema kuwa kuwachimbia visima hivyo viwili ni heshima Raisi Kikwete
alipinga na kusema si kwa heshima yake bali ni haki ya wakazi hao vinginevyo
iwe kwa heshima yake yeye mkurugenzi.
Raisi Kikwete
alimtaka mkurugenzi huyo kuhakikisha anachimba visima hivyo ili wakazi hao
wasiendelee kutaabika na maji ambapo kuna njia ya kuweza kupunguza makali ya
tatizo hilo.
Katika hatua
nyingine alisema chanagamoto ya ukosefu wa zahanati atachangia kiasi cha
shilingi milioni mbili kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ambao umeanza ambapo
wakazi hao huenda umbali wa zaidi ya kilomita 10 kupata huduma za afya.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment