Wednesday, December 26, 2012

TOENI MISAADA KWA WATU WENY UHITAJI NA SI KUFANYA ANASA


Na John Gagarini, Kibaha

JAMII nchini imetakiwa kutoa misaada kwa watu wenye uhitaji katika kipindi cha sikukuu badala ya kuzitumia kwa anasa.

Hayo yalisemwa na Bi Mwajuma Yasini wakati akishukuru kupewa misaada iliyotolewa kwenye sikukuu ya Krismasi kwenye hopsitali ya wilaya ya Kibaha Tumbi.

Bi Yasini alisema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitumia vibaya fedha kwenye sikukuu kama hizo kwa kufanya vitendo vya kifahari huku watu wenye uhitaji wakiwa hawana msaada.

“Ni vema Watanzania wangetumia sikuu kwa kutoa misaada kwa watu wenye mahitaji wakiwemo watoto waishio kwenye mazingira magumu, yatima na wagonjwa,” alisema.

Aidha alisema kuwa ibaada ya kweli ni kuwakumbuka watu wenye uhitaji ambapo wao kama wagonjwa kwao imekuwa faraja katika sikukuu hii ya Krismasi.

Kwa upande wake mwandishi wa habari na Diwani Viti Maalumu Kibaha Mjini (CCM) Bi Selina Wilson ambaye ndiye aliyetoa misaada hiyo alisema kuwa alitoa ikiwa ni kama ibaada kwa watu wenye mahitaji.

“Niliona niungane na wagonjwa kwa kuwapatia zawadi za Krismasi ili nao wajione kuwa jamii ina wajali na iko pamoja katika hali zote ikiwa ugonjwa na furaha,” alisema Bi Wilson.

Naye muuguzi wa zamu wa hospitali ya Tumbi Bi Ndenisaria Ntuah alisema wagonjwa nao wanahitaji kufarijiwa kwa kupewa misaada mbalimbali.

Misaada hiyo ilitolewa kwenye wodi za watoto, wazazi na wanawake na wanaume wenye magonjwa ya kawaida, misaada iliyotolewa ni sabuni, mafuta ya kujipaka, juisi na biskuti

Mwisho.

No comments:

Post a Comment