Na John Gagarini, Bagamoyo
MJI Mdogo wa Bagamoyo mkoani Pwani umewataka watu wote
walionunua maeneo ya wazi kwenye kata ya Magomeni na kujenga nyumba waondoke
kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.
Akizungumza na wakazi wa kitongoji cha Magomeni
wilayani humo Meya wa Mji huo Bw Abdul Sharifu alisema kuwa kwa kushirikiana na
baadhi ya maofisa wa ardhi wasio waaminfu wamenunua maeneo hayo kinyume cha
sheria.
Bw Sharifu alisema kuwa maeneo yote ya wakazi katika
kata ya Magomeni yameuzwa yote kinyume cha sheria jambo ambalo linasababisha
kata hiyo kushindwa kupewa miradi ya maendeleo kwa ajili ya huduma za kijamii.
“Wale wote walionunua maeneo hayo ya wazi waondoke
mara moja kwani endapo hawataondoka wataondolewa kwa nguvu kwani haiwezekani
tukakosa eneo kwa ajili ya huduma za kijamii kutokana na watu ambao wanavunja
sheria hivyo lazima waondoke,” alisema Bw Sharifu.
Aidha alisema kuwa tayari baraza hilo limewaagiza watu
wa ardhi kuyaainisha maeneo yote yale ya wazi ambayo yameuzwa.
“Wilaya ina eneo kubwa lakini cha kushangaza watu
wananunua maeneo ya wazi ambayo yametengwa kwa ajili ya huduma za jamii lakini
baadhi ya watu wenye kutaka maslahi yao binafsi wanavunja sheria,” alisema Bw
Sharifu.
Alisema kwa sasa wanataka kujenga soko na zahanati
lakini hakuna eneo la wazi kwa ajili ya kujenga vitu hivyo kutokana na maeneo
hayo kuhujumiwa hivyo watu wengi kukosa fursa ya kujengewa miundombinu.
Aliwataka maofisa ardhi watakaotembelea maeneo hayo
kuyaanisha maeneo hayo kwa kutumia ramani za zamani ili kubaini watu waliokiuka
taratibu za ujenzi kwa kujenga maeneo ya wazi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment