Na John Gagarini, Bagamoyo
JUMUIYA ya Wazazi wilaya ya Bagmoyo mkoani Pwani
imesema kuwa itawachukulia hatua za kisheria viongozi wote waliohusika
kuhujumu mali za chama hicho ikiwa ni pamoja na kuziuza kinyemela.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mafunzo
kwa viongozi wa kata za wilaya ya Bagamoyo mwenyekiti wa Jumuia ya hiyo
Bw Abdul Sharifu alisema kuwa baadhi ya viongozi wamehusika kuhujumu
mali za Jumuiya hiyo.
Bw Sharifu alisema kuwa Jumuiya hiyo ni moja ya
Jumuiya za Chama zenye mali nyingi lakini baadhi ya viongozi wamehusika
kuzihujumu.
"Kwa kiongozi yoyote aliyehusika kuhujumu mali za
Jumuiaya akae tayari kuwajibika kwa kurudisha mali husika na endapo
atashindwa kufanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake
kwani kwa sasa tunataka tuijenge upya Jumuiya yetu ili iwe tegemeo kwa
Chama," alisema Bw Sharifu.
Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya
Bagamoyo ambaye pia ni Meya wa Mji wa Bagamoyo alisema kuwa baadhi ya
mali zilizohujumiwa ni pamoja na mashamba viwanja na shule.
"Moja ya mali zilizohujumiwa ni shule ya sekondari
ya Kaole ambayo inasemekana imeuzwa kinyume cha taratibu na haikupaswa
kuuzwa kwani hiyo ni mali ya Jumuiya na si mali ya mtu binafsi na ni
moja ya kitu ambacho kina manufaa makubwa kwa watu kwa kuwaptia elimu,"
alisema Bw Sharifu.
Akielezea juu ya semina hiyo elekezi alisema ina
lengo la kuwaelekeza viongozi kujua wajibu wao kwani baadhi ya viongozi
wanaochaguliwa wamekuwa hawajui majukumu yao ipasavyo.
Aidha alisema kuwa yeye wakati anachaguliwa aliahidi
kuwapatia semina viongozi wa kata na matawi jambo ambalo ndiyo
analitekeleza kwani viongozi hao wa kata mara baada ya kupata semina
hiyo nao watakwenda kuwafundisha viongozi wa matawi kwenye kata zao.
mwisho.
No comments:
Post a Comment