Friday, December 28, 2012

AJINYOFOA SEHEMU ZA SIRI KUKWEPA MADENI



 Na John Gagarini, Kibaha
WASWAHILI wanasema ukistaajabu ya Musa basi utaona ya Firauni yaliyomkuta Bw  Charles Malosha (44) mkulima wa Visiga Kati wilaya ya Kibaha mkoa wa Pwani yanasikitisha kwani amekumbwa na masahibu ambayo hataweza kuyasahau katika maisha yake yote na kila aliyesikia hakika anashikwa na simanzi kutokana na kuondolewa sehemu zake za siri katika mazingira ya kutatanisha.
Akizungumza jana kwenye kituo cha afya cha Mlandizi Bw Malosha mwenye watoto sita alisema kuwa alitokewa na tukio hilo la kikatili akiwa kwenye kituo cha polisi Visiga lakini cha kushangaza watu walivumisha kuwa amengofoa sehemu zake za siri na kuzitafuna jambo ambalo si la kweli.
Bw Malosha alisema kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 26 mwaka huu  majira ya mchana ambapo alichukuliwa na mgambo na kuambiwa kuwa anaitwa kituo cha polisi ambapo alikwenda na ndipo alipoambiwa kuwa kuna watu kadhaa wanamdai fedha ambazo walimpa kwa ajili ya kuwanunulia kwa ajili ya kujengea.
“Wakati niko polisi kwenye selo walifika walalamikaji wakiwa na polisi mmoja ambapo kati yao mmoja alikuwa na rungu ambalo alinipiga nalo kichwani na kupoteza fahamu na nilipozinduka sehemu zangu za siri (Korodani) zilikatwa na nikajikuta damu nyingi zinamwagika na ndipo nilipokimbizwa hospitali kupata matibabu,” alisema Bw Malosha.
Alisema kuwa kimsingi alikuwa akidaiwa milioni tatu na watu watatu ambao walimpa fedha kwa ajili awauzie maeneo lakini alishindwa kuwapatia maeneo hayo kwa wakati waliokuwa wakiyataka.
“Kweli walikuwa wakinidai na mimi nilikuwa najipanga aidha kuwarudishia fedha zao au kuwatafutia sehemu nyingine ambapo tangu tuanze kuwasiliana ni kama miezi minne imepita sasa,” alisema Bw Malosha.
Kwa upande wake mkewe Bi Martha Boni alisema kuwa siku ya tukio hilo alimwaga na kumwambia hata mwona tena hivyo alee watoto wake jambo ambalo lilimshangaza lakini hakuweza kumfafanulia kuwa alikuwa akimaanisha nini.
“Baada ya muda nilipigiwa simu na kuambiwa kuwa mume wangu yuko hoi hospitali na hawezi kuongea kwa kweli nilichanganyikiwa na kutaka kujua yaliyomsibu lakini nilijulishwa kuwa ameondolewa sehemu zake za siri jambo ambalo lilizidi kuniumiza na kushindwa kujua nini cha kufanya na kuanguka chini kasha kupoteza fahamu,” alisema Bi Boni.
Bi Boni alisema kuwa anashangaa kusikia watu hao wakisema kuwa wanamdai milioni 20 jambo ambalo si lakweli kwani wanamdai shilingi milioni sita tu na alichukua milioni mbili kwa kila mmoja kwa watu watatu ambao wanatokea Jijini Dar es Salaam.
Naye mganga wa kituo hicho cha afya cha Mlandizi Dkt Nicetus Matem alisema kuwa alimpokea mgonjwa huyo ambaye alifika hapo huku akiwa anatokwa na damu nyingi na kumhudumia hadi damu ilipoacha kutoka.
“Ni kweli sehemu zake hizo za kiwanda cha kuzalishia mbegu (Korodani) zimeondolewa kabisa lakini hazikuondolewa na kitu chenye ncha kali bali kwani zilondolewa kwa kitu kiischo na ncha kali na nilipomuuliza alisema kuwa amezinyofoa yeye mwenyewe,” alisema Dkt Matem.
Dkt Matem alisema kuwa alirudishia vizuri lakini cha kusikitisha ni kwamba Bw Malosha hataweza kuzaa tena lakini hali ya sehemu yake kuu ya siri itakuwa ikifanya kazi kama kawaida na hali yake inaendelea vizuri.
Naye kamanda wa polisi mkoa wa Pwani  Ulrich Matei alisema kuwa taarifa alilzozipata ni kuwa mtu huyo alijijeruhi mwenyewe na alikuwa akidaiwa na milioni 11.5 na watu wanne tofauti.
“Aliachiwa shamba na bibi mmoja ambapo alikuwa akikata maeneo na kuyauza na yule mmiliki alipofika alisema kuwa maeneo aliyoyauza ni ya kwake kwani hakumruhusu kuyauza hivyo atajuana na watu hao hivyo awalipe yeye mwenwe,” alisema Matei.
Kamanda Matei  alisema kuwa watu hao walianza kumdai na kusema kuwa aliwadanganya kuwa eneo hilo ni lake hivyo arejeshe fedha zao kutokana na kuchanganyikiwa alifikia hatua ya kutaka kujiua.
“Lengo lake kujidhuru alitaka kujiua na hakufanyiwa kitendo hicho na mtu bali alifanya yeye mwenye na kwamba alifanyiwa na mtu si kweli na kama kuna mtu kamfanyia na kama kuna mtu anaficha ukweli nitafutailia kujua na akipata nafuu tutamhoji kupata ukweli kwani hana nia ya kumlinda mtu yoyote kwani kila mtu ana haki zake za msingi,” alisema Matei.
Aliongeza kuwa mtu huyo aliamua kufanya hivyo baada ya kuona kuwa sasa hana njia na ana deni na kuona njia ni kujiua na haiwezekani afanyiwe kitendo hicho kwenye kituo cha polisi.
 Mwisho

No comments:

Post a Comment