Thursday, October 8, 2026

MZABUNI WA USAFI SOKO LA LOLIONDO APEWA SIKU TATU SOKO LISIWE NA UCHAFU

MZABUNI wa usafi wa soko la Loliondo amepewa siku tatu kuhakikisha anaondoa uchafu uliopo sokoni hapo na kutoa takataka kwa wakati ili kuliweka soko hilo kwenye hali ya usafi.


Agizo hilo limetolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo alipotembelea soko hilo kusikiliza kero na changamoto za soko na kuzitatua.

Mawazo memwagiza mzabuni huyo Sosamy kuhakikisha soko hilo linakuwa safi na kuacha kurundika uchafu ambao unakaa muda mrefu na kuwa kero kwa wananchi wanaohudumiwa na soko hilo pamoja na wafanyabiashara hao.

Amesema kuwa amepata malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara wa soko hilo kwani mzabuni huyo amekuwa akichelewesha kuondoa takataka kwa wakati hivyo anatoa siku tatu soko hilo lisiwe na uchafu ikiwa ni pamoja na kusafisha mitaro ya soko hilo.

Naye Mwenyekiti wa soko hilo Mohamed Mnembwe amesema kuwa wamekuwa wakimhimiza mzabuni huyo kutoa takataka kwa wakati lakini ameshindwa kutekeleza na kulundika takataka hivyo kusababisha kero sokoni hapo.

Nao baadhi ya wafanyabiashara Wastara Kilindo na Sheba Kalage wamesema kuwa uchafu huo unaozalishwa ni mwingi na unapaswa kutolewa kwa wakati ili kuondoa kero za uchafu.

Ziara hiyo ya Mstahiki Meya wa Manispaa ikiwa na lengo la kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya usafi na barabara ili kukabilina na mvua za Elnino zinazotarajiwa kunyesha hivi karibuni.


KIWANDA KUONDOA KEMIKALI ILIYOSAMBAA KWENYE MAKAZI YA WATU

KIWANDA cha Lake chakubali kuondoa mabaki ya kemikali ya salfa inayolalamikiwa na wananchi kuleta athari za kiafya eneo la Matunda Mtaa wa Lulanzi Kata ya Picha ya Ndege Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.

Kiwanda hicho kiliridhia kuondoa mabaki hayo baada ya wananchi kulalamika wakati wa ziara ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo kutembelea kiwanda hicho ambacho kiko kwenye hatua za ujenzi.

Mawazo amesema kuwa ili kuepuka athari za kiafya ambazo zinaweza kujitokeza hasa katika kuelekea mvua kubwa za Elnino zinazotarajiwa kuanza kunyesha hivi karibuni kuna haja ya kiwanda hicho kutoa mabaki ya kemikali hizo hadi ifikapo Oktoba 17.

"Wananchi hapa wanalalamika kuwa kuna kemikali ambazo zina athari kiafya hivyo fanyeni kila njia kuziondoa ili zisilete madhara hasa wakati wa mvua ndipo zinaposambaa kwenye makazi ya wananchi,"amesema Mawazo.

Alisema serikali inahitaji uwekezaji lakini uzingatie afya za watu kwani endapo kemikali hizo zitaendekea kubaki hapo na kusambaa kwenye makazi ya watu zinaweza kuleta madhara makubwa kwa wananchi.

Moja ya wananchi wa eneo hilo la Matunda Yusuph Mohamed amesema kuwa kemikali hiyo imemwathiri kwani nyumba yake imepasuka migomba imekauka na ametoa taarifa kwa uongozi lakini hakuna msaada wowote.

Naye Frida Kitundu amesema kuwa hivi karibuni kiwanda hicho kilitoa kemikali hiyo lakini hawakuimaliza kwani ilikuwa nyingi sana na hutiririka hasa kipindi cha mvua na ni changamoto hasa kwa watoto ambao hucheza bila ya tahadhari.

Kitundu amesema ili kuwe na usalama waitoe kemikali hiyo kwa kuchimba na kuweka udongo mwingine pale watakapokuwa wameitoa na wasitiririshe maji toka kwenye kiwanda hicho bali wawe na mfumo wa kuyatibu maji.

Akijibu malalamiko hayo Msimamizi wa ulinzi wa kiwanda hicho cha Lake Rajab Masanja amesema kuwa watafanya itaratibu wa kuondoa mabaki hayo ya kemikali hiyo ili kuondoa changamoto hiyo.

Masanja amesema kuwa kemikali hiyo ilikuwa inatumika zamani lakini kwa sasa haipo tena na wamekuwa wakiitoa na watahakikisha hadi muda uliopangwa watakuwa wamekamilisha zoezi hilo.
 



Wednesday, October 7, 2026

KEDS YAPONGEZWA YATAKIWA KUSAFISHA MTARO SEHEMU ILIYOBAKI ILI KUKABILIANA NA MVUA ZA ELNINO

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha imekipongeza kiwanda cha KEDS kikichopo Picha ya Ndege kwa kutekeleza agizo la kusafisha mtaro wa maji yanayotoka kiwandani hapo na kuondoa kero ya majitaka kwenda kwenye makazi ya watu.

Aidha kimepongezwa kwa kuweza kutoa ajira kwa vijana wa Tanzania zaidi ya 500 ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuzalisha ajira kwa wananchi.

Akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda hicho kinachojihusisha na uzalishaji wa sabuni Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Dk Nicas Mawazo amesema kiwanda hicho kilikuwa kinatiririsha maji taka ambayo yalikuwa ni kero kwa wananchi wa eneo la Matunda Kata ya Picha ya Ndege.

Mawazo amesema kuwa kiwanda hicho kimetekeleza agizo walilopewa la kutakiwa kusafisha mtaro huo ili maji hayo yasiende kwenye makazi ya watu na kuondoa kero kwa wananchi na kuepusha athari za kiafya.

"Tunawapongeza kwa kutekeleza agizo mlilopewa tulipotembelea changamoto ilikuwa ni kubwa lakini tumeona kazi mliyoifanya hasa tukielekea kipindi cha mvua kubwa za Elnino pia tumeambiwa kuna eneo limebaki kama mita 300 fanyeni mpango msafishe na kuboresha ili mvua zikianza maji yapite na yasielekee kwenye makazi ya wananchi,"amesema Mawazo.

Katika hatua nyingine ameomba kiwanda hicho kisaidie ukarabati wa mabati ya Shule ya Msingi Lulanzi ambayo iko kwenye hali mbaya licha ya kuwa shule hiyo ni moja ya shule zinazoongoza kwa kuwa na ufaulu mkubwa kwenye Manispaa hiyo.

Mawazo amesema ni utaratibu wa kisheria wawekezaji kusaidia jamii ambayo iko jirani na uwekezaji hivyo waangalie namna ya kusaidia shule hiyo kwani mvua kubwa zitakaponyesha kunaweza kutokea changamoto kubwa ya usomaji kwa wanafunzi.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Lulanzi Thobias Shilole unakopita mtaro huo amesema kuwa mvua inaponyesha maji yamekuwa yakiingia kwenye makazi ya watu hivyo kwa kusafishwa mtaro huo kutasidia kuondoa changamoto hiyo.

Moja ya wananchi wa Mtaa huo Farid Hamis amesema kuwa eneo hilo lililobaki walisafishe kwani mvua kidogo ikinyesha maji yabaelekea kwenye nyumba zao hivyo hofu yao mvua za Elnino zikinyesha changamoto itakuwa kubwa sana.

Kwa upande wake Meneja Biashara wa kiwanda hicho Derick Doedatus amesema kuwa eneo lililobaki kusafishwa lilishindikana baada ya mmoja ya wananchi kugoma kuwa ardhi yake inapunguzwa kutokana na mtaro huo kutanuliwa ili maji yapite kwa urahisi hata hivyo watamalizia sehemu iliyobakia.

Deodatus amesema kuwa ombi la kusaidia Shule ya Msingi Lulanzi wamelichukua na kutaka uongozi wa shule hiyo kuandikia kiwanda ili kiweze kusaidia changamoto hiyo ya mabati.


MEYA DK MAWAZO ATOA SIKU SABA KIWANDA KUACHA KUTIRIRISHA MAJI MACHAFU KWENYE MAKAZI YA WATU

MSTAHIKI meya wa Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo ametoa siku Saba Kwa kiwanda Cha Cordy kuhakikisha kinasitisha kutiririsha maji machafu kwenye makazi ya watu.

Ameyasema hayo Wakati wa ziara yake ya kutembelea viwanda kwenye Kata ya Picha ya Ndege ikiwa ni maandalizi ya kujikinga na athari za mvua za Elnino 

Mawazo amesema kuwa kiwanda hicho ambacho kiko kwenye Mtaa wa Picha ya Ndege kilitakiwa kitengeneze miundombinu ambayo itaepusha maji hayo kutiririka kwenye makazi ya wananchi ambapo maji hayo yanakemikali.

Kwa upande wake ofisa mazingira wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Bryson Mpogoza amesema kuwa tayari kiwanda hicho kilishapewa onyo na kupigwa faini lakini bado hakijatekeleza maagizo ya Ofisi yake.

Naye ofisa uajiri wa kiwanda cha Cordy Vicent Emanuel amesema kuwa wamepokea maagizo hayo na watatekeleza kuanzia siku ya Jumapili.

Naye Mkazi wa eneo kilichopo kiwanda hicho Sanura Amir amesema kuwa maji yayo yamekuwa kero kubwa na kuhofia kuathiri afya zao.

Monday, October 5, 2026

SERIKALI KUGHARAMIA MAFUNZO YA VITENDO KWA WALIMU KUIMARISHA TAALUMA

SERIKALI kupitia Bodi ya Kitaaluma ya Walimu  imejipanga kugharamia mafunzo ya vitendo kwa kuwapatia fedha za kujikimu wakati watakapokuwa katika mafunzo hayo kama sehemu ya kuimarisha taaluma zao ambayo wameipata vyuoni na mafunzo hayo kwa vitendo yataendelea kutolewa kwa wahitimu wa Vyuo vikuu kwa maana ya walimu wenye Shahada.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda kwenye Chuo cha Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) Bagamoyo wakati akitoa salamu ya Siku ya Walimu Duniani.

Mkenda amesema kuwa Wizara itaimarisha mafunzo endelevu ya walimu kazini (MEWAKA) na ambapo ADEM ni Taasisi muhimu katika kuwajengea uwezo walimu ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji na iendelee kutekeleza wajibu huo kwa weledi na ufanisi kuuwalinda walimu katika ajira zao na kuendelea kuwajengea uwezo wakiwa kazini ili kuwaimarisha kitaaluma.

“Serikali inaendelea kuimarisha utoaji wa mafunzo ya walimu kwa kupanga upya Vyuo vya Ualimu na kuvipa majukumu kuendana na hali halisi ya sasa ili kuboresha uwezo wa taaluma wa wahitimu kwa mfano Chuo cha Ualimu Marangu ambacho awali kilikua kwa ajili ya lugha kitaongezewa uwezo wa kuwaandaa walimu ambao watakwenda kufundisha lugha mbalimbali za kigeni mara watakapohitimu masomo yao,”amesema MKenda.

Aidha amesema kuwa ili kuendana na Sera ya Elimu ya sasa ambayo imeongeza masomo ya lugha za kigeni kwenye Mtaala wa sasa ukiacha lugha ya Kiingereza, Kichina, Kifaransa na Kiarabu ni lugha ambazo zinaweza zikachukuliwa na mwanafunzi anayetaka kusoma kama kuna walimu wa kufundisha.

Naye Mtendaji Mkuu wa Dk Maulid Maulid alisema kuwa wanaendelea kutekeleza majukumu yake kikamilifu ili kuendana na mageuzi yanayokwenda sambamba na mabadiliko ya Sera ya Elimu na kutekeleza dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 kwa kuendesha mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa elimu nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Shaibu Ndemanga alisema kuwa anaipongeza sana Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kazi kubwa wanayoifanya kuboresha sekta ya elimu nchini kwa kusimamia ubora wa elimu inayotolewa katika ngazi zote.

Sunday, October 4, 2026

NYONGO KUKABILI MIGOGORO YA ARDHI KWA MBINU MPYA

MKUU wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo amekuja na mkakati kabambe wa kupambana na migogoro ya ardhi kwa kuanzisha kituo cha uuzaji ardhi badala ya kutumia matapeli.

Nyongo aliyasema hayo Mjini Kibaha wakati wa hafla ya kumuapisha Mkuu mpya wa Wilaya ya Kibiti Luteni Kanali Fortunatus Kipeta.

Alisema kuwa migogoro ya ardhi ndani ya Mkoa imekuwa ni mingi sana hivyo lazima kuja na njia mbadala ya kudhibiti changamoto hiyo ili kupunguza migogoro hiyo.

"Njia mojawapo ni kuwa na kituo cha uuzaji ardhi ambapo mtu akitaka kuuza ardhi anapeleka taarifa na kununua ardhi atakwenda kwenye kituo hicho na kupata taarifa na kununua,"alisema Nyongo.

 Alisema kuwa kituo hicho kitakuwa na vitengo vyote vinavyohusiana na uuzaji na umilikaji wa ardhi ambapo taratibu zote zitafuatwa na mtu akiuziwa kiwanja hakitakuwa na changamoto yoyote.

"Matapeli wote wasakwe mmoja baada ya mwingine kwani hatutaki migogoro ya ardhi na wanauchafua Mkoa wetu kwani hawa wamewaibia hadi wawekezaji hali ambayo inaleta taswira mbaya na kuchelewesha maendeleo,"alisema Nyongo.

Aliwataka wakuu wa wilaya na timu za usalama kutatua migogoro ya ardhi ambayo baadhi inasababishwa na watumishi wa serikali kwa kushirikiana na genge linalojihisisha na kuuza ardhi za watu hivyo watenge siku maalumu kusikiliza kero hizo.

"Pia wakuu wa wilaya tatueni changamoto mapema msisubiri wananchi waje kulalamika kwa viongozi wa ngazi za juu na mzingatie weledi na utaalam na ushirikiano na hakikisheni mnaongeza mapato pia anzeni maandalizi ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kidato cha kwanza 2028 wanafunzi watakuwa wengi sana,"alisema Nyongo.

Alimtaka Mkuu huyo wa Wilaya ya Kibiti kutumia fursa kuhamasisha uwekezaji kwani wilaya hiyo haina viwanda kupitia sekta za kilimo uvuvi na kutumia bomba la gesi linalopita kwenye wilaya hiyo.

Naye Mkuu mpya wa Wilaya ya Kibiti Luteni Kanali Fortunatus Kipeta alisema kuwa atawatumikia wananchi kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu kwani cheo ni dhamana pia kutumia fursa mbalimbali zilizopo ili kuleta maendeleo kwa wananchi.

Kipeta alisema kuwa atahakikisha anahamasisha amani kwa kushirikiana na makundi mbalimbali wakiwemo wazee vijana wanawake na watu wenye ulemavu.

MDAU WA MAENDELEO MILANZI ASAIDIA SEKONDARI YA MBOGA

MDAU wa maendeleo wa Shule ya Sekondari ya Mboga Expeditor Milanzi ametoa kiasi cha shilingi milioni moja kwa ajili ya kununua samani za walimu wa shule hiyo ili kuwapunguzia changamoto ya vifaa walimu wa shule hiyo.

Aidha kupitia kampuni  ya Starlink Gulf Trading Limited imesaidia mashine ya kudurusu karatasi kwa ajili ya kudurusu mitihani mingi kwa wakati mmoja ili kurahisisha upatinaji wa mitihani kwenye hiyo iliyopo Kata ya Msoga Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo.

Milanzi ambaye ni Meneja uendeshaji wa kiwanda hicho alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 13 ya kidato cha nne ya Shule hiyo ya Sekondari ya Mboga amesema kuwa mchango huo utasaidia kukabilina na baadhi ya changamoto shuleni hapo.

Amesema kuwa bada ya kusomewa changamoto ya shule hiyo ameona kuna haja ya kusaidia shule hiyo ili iweze kukabili changamoto ya kudurusu mitihani ambapo waliyokuwa nayo ni ndege hivyo kutokidhi mahitaji kwa wanafunzi waliyoko shuleni hapo.

“Ukosefu wa samani za walimu zimenifanya nijisikie vibaya kwani hawana samani jamboi ambalo limenigusa mimi binafsi hivyo nimeona nichangie ili walimu waweze kukaa kwenye mazingira mazuri waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi,”amesema Milanzi.

Aliomba wadau wengine wajitokeze kuchangia ili kutatua changamoto mbalimbali zilizopo shuleni hapo ili watoto waweze kusoma kwenye mazingira mazuri na walimu waweze kufundisha kwenye mazingira bora na rafiki.

Naye mwenyekiti wa bodi ya Shule hiyo Tatu Kikwete amesema kuwa kwa ushirikiano wa shule na wadau wameweza kupunguza vitendo vya utoro na kuchukua hatua kwa wanafunzi ambao wanakwenda kinyume na taratibu za shule.

Tatu amesema kuwa wazazi walezi na jamii kwa ujumla inapaswa kushirikiana ili kukabili changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo ili iweze kutoa matokeo mazuri kwa wanafunzi wanaosoma shule hiyo. 

Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo Archard Kyokola amesema kuwa changamoto nyingine ni ukosefu wa fedha kwa ajili ya umaliziaji wa mabweni mawili ya wavulana ili wahamie shuleni upungufu wa matenki makubwa ya maji kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi kukosekana kwa mfumo wa usambazaji wa maji katika nyumba za walimu.

Kyokola amesema kuwa mbali ya changamoto hizo pia kuna mafanikio ambayo wameyapata ikiwa ni pamoja na asilimia 100 ya waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana kufaulu daraja la kwanza mpaka la nne na kuchaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano na cha sita pamoja na vyuo vya kati kuongeza ufaulu kwa daraja la kwanza na la pili na tatu kwa asilimia 50 na kuondoa daraja sifuri na kupunguza daraja la nne jumla ya wanafunzi 155 walitunukiwa vyeti huku shule hiyo ikiwa na wanafunzi 821.