NAIBU Waziri mpya wa wizara ya Mifugo na Uvuvi Abdalah Ulega amesema hawezi kulifumbia macho hata kidogo suala la baadhi ya viongozi na watendaji ambao wamekuwa na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea kwa kukaa tu ofisini bila ya kutimiza majukumu yao ipasavyo na kuwaagiza kuchapa kazi kwa bidii bila ya kutegeana kwa kuvitembelea vikundi vyote vya uvuvi na ufuga ili kuweza kusikiliza kero na kubaini changamoto zinazowakabili katika kutekeleza majukumu yao.
Ulega alitoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara yake ya kikazi ya siku moja kwa viongozi mbali mbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, ambapo amesema kuna baadhi ya watumishi wengine wamekuwa ni wazembe na kusababisha kukwamisha juhudi za serikali katika kuleta chachu ya maendeleo hivyo ameahidi kulivalia njuga suala hilo kwa lengo la kuweza kuboresha sekta ya uvuvi na ufugaji.
Aidha Naibu Waziri huyo aliwataka maafisa uvuvi na mifugo kuwa wazalendo na nchi yao na kuhakikisha wanazilinda na kuzitunza rasilimali zilizopo pamoja na kuweka mipango endelevu ya kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya kufanyia kazi zao sambamba na kuviwezesha vikundi hivyo katika mambo mbali mbali ikiwemo kujenga,malambo, majosho pamoja na kuwapatia vitendea kazi.
Pia Ulega alisema kwamba kwa sasa kipaumbele chake kikubwa ni kuhakikisha kwamba anavisaidia kwa hali na mali kwa kuviwezesha vikundi mbali mbali vya wafugaji na uvuvi pamoja na kuweka mipango madhubuti ambayo itaweza kusaidia kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo katika sekta hiyo aliyopewa dhamana na Rais Dk. John Pombe Magufuli.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Filbeto Sanga akizungumzia kuhusiana na suala la ardhi alisema kuwa kumeibuka kikundi cha baadhi ya madalali ambao ni matapeli wanachukua hela za watu na kuamua kuuza maeneo ya mashamba ambayo tayari yana hati miliki bila ya kufuata taratibu zozote na kupelekea wananchi wenyewe kujikuta wanakosa maeneo kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao za kimaendeleo.
Katika hatua nyingine Mkugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Mkurunga Mshamu Munde akizungumza katika kikao cha dharura na waandishi wa habari ofisini kwake amekanusha uvumi wa taarifa zinazotolewa na wananchi kuhusiana na shamba linalomilikiwa na mwekezaji wa kampuni ya Soap Allied Industry .
Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa eneo hilo ambalo linalalamikiwa na wananchi hao lina ukumbwa wa hekari 1750 na kuongeza kuwa kwa sasa linamilikiwa kihalali na mwekezaji huo tangu mwaka 1988, na kupiga marufuku wananchi wanaovamia maeneo ya watu kiholela bila ya kuzingatia taratibu.
“Mimi kwa kweli nina shangaa sana huu uvumi unaotokwa kwa baadhi ya wananchi kuhusiana na eneo hili, ndugu zangu waandishi eneo hili linamilikiwa kihalali, hivyo mimi ninachowaomba watu wanaolalamika kufika ofisi za mkurugenzi ili niwape ufafanuzi zaidi na sio kuanza kusababisha migogoro ambayo haina faida hata kidogo katika Wilaya yetu ya Mkuranga nah ii tabia kwa kweli mimi siwezi kuivumilia hata kigogo nitahakikisha kwamba maeneo yote yanatolewa kwa utaratibu unaotakiwa,”alisema Mkurugenzi huyo.
Pia Mkurugenzi huyo alisema katikia kumuunga juhudi mkono Rais wa awamu ya tano Dk. John Pombe Magufuli katika kuwa na Tanzania yenye uchumi wa viwanda wameshatenga maeneo mbali mbali kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda ambavyo vitaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kukuza sekta ya viwanda na kuleta maendeleo kwa wananchi pamoja na upatikanaji wa fursa za ajira kwa vijana.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ya Mkuranga Juma Abed na Diwani wa kata ya Makamba Hssan Dunda hapa wanazungumzia kuhusiana na sakata hilo la mgogoro wa shamba la mwekezaji huo na malalamiko yanayotolewa na wananchi.
Walisema kuwa kwa sasa shamba hilo linamilikiwa kihalali na mwekezaji huyo kwani alishakabidhiwa na halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga baada ya kufuata taratibu zote zinazostahili hivyo wananchi wanatakiwa kuachana na tabia ya kuvamia maeneo mengine ambayo sio yao.
VITENDO vya uvamizi wa maeneo ya mashamba pamoja na viwanja vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa na wenyeviti wa vijiji kwa kushirikiana na madalali ambao ni matapeli kwa kuvamia maeneo ambayo sio yao na kuamua kuuza kinyemela kinyume na taratibu katika Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani vinachangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa migogoro kila kukicha.
MWISHO