Tuesday, March 25, 2025

JK AWASILISHA UJUMBE MAALUMU KWA RAIS WA SENEGAL KUTOKA KWA RAIS SAMIA

Mhe. Rais Mstaafu  Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amewasilisha  ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Senegal, Mhe. Bassirou Diomaye Faye jijini Dakar.

Katika mazungumzo  yao ya kirafiki,  Rais Mstaafu alieleza dhamira ya dhati ya Rais Samia na Serikali anayoiongoza ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii kati ya Tanzania na Senegal.

Pamoja na masuala ya ushirikiano wa kiserikali, Rais Mstaafu pia alisisitiza umuhimu wa kukuza uhusiano baina ya wananchi wa mataifa haya mawili kupitia sekta za elimu, biashara, utalii, na maendeleo ya vijana na wanawake.

Ziara hii ni sehemu ya juhudi endelevu za Tanzania kuimarisha uhusiano wa kimataifa na mataifa ya Afrika Magharibi, huku ikiweka msisitizo kwa diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa watu kwa watu.

MAANDALIZI UWASHWAJI MWENGE WA UHURU KITAIFA PWANI MBIONI KUKAMILIKA



MAANDALIZI ya Uzinduzi wa mbio za Mwenge Kitaifa yamefikia asilimia 96 ambapo Mwenge huo utawashwa Wilayani Kibaha Mkoani Pwani Aprili 2 Mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa maandalizi yanaenda vizuri.

Kunenge amesema kuwa kwa sasa zimebaki siku sita ambapo Mwenge utazinduliwa Aprili 2 na utatembelea kwenye Halmashauri tisa za mkoa huo kwa kuanza na Halmashauri ya Mji Kibaha utakapoanzia.

"Uwanja umekamilika yamebaki maeneo machache ambapo hadi leo sehemu kubwa itakuwa imekamilika na kubaki mambo madogo madogo,"amesema Kunenge.

Amesema kuwa majukwaa yamekamilika na matarajio ni kuwa na watu 16,000 ambapo miundombinu ya maji, sehemu ya magari kukaa tayari, taa, mifumo ya majitaka na ulinzi viko tayari.

Thursday, March 20, 2025

TANROADS YATOA UFAFANUZI LORI LILILOZIDISHA UZITO MIZANI YA VIGWAZA.

WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) imetoa ufafanuzi juu ya taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ya lori la mizigo lililokamatwa kwenye mizani ya Vigwaza kuwa taratibu za kulikamata lori hilo ulifuatwa.

Aidha gari hilo lilipigwa faini hiyo kwa kuzingatia sheria ya udhibiti wa uzito barabarani ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018.

Akizingumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za mizani hiyo ya Vigwaza Mtaalamu wa Kitengo cha Mizani Tanroads Makao Makuu Vicent Tarmo amesema kuwa gari hilo lilizidisha uzito zaidi ya tani moja.

Tarmo amesema kuwa gari hilo lenye namba za usajili T 137 DLR na tela namba T 567 CUR lilikuwa limetokea nchini Congo likiwa limebeba madini ya Shaba ambapo uwezo wake ni kubeba tani 48 lakini lilikutwa likiwa na uzito tani 48.1.

"Kutokana na kuzidisha uzito huo gari hilo lilitakiwa kulipiwa faini ya shilingi 900,000 ikiwa ni adhabu ya kuzidisha uzito halisi lakini dereva huyo alisema kuwa amezidishiwa uzito hivyo kupinga faini hiyo,"amesema Tarmo.

Amesema kuwa sheria inataka magari yote yenye uzito kuanzia tani 3 na nusu lazima yapime uzito ili kuepusha uharibifu wa barabara hivyo kutokana na gari hilo kuzidisha uzito alipaswa kulipa faini hiyo.

"Dereva huyo amesema kuwa amepita mizani mbalimbali uzito haukuzidi hivyo kwa nini hapa uzidi lakini kwa mujibu wa sheria alipaswa kulipa na siyo kukaidi kulipa,"amesema Tarmo.

Amesema kuwa gari hilo lilipita hapo Machi 13 ambapo kwa siku hiyo yalipimwa mwagari 819 ambapo saba yalibainika kuzidisha uzito ambapo mengine yalilipa na kuendelea safari lakini gari hilo dereva wake aligoma kulipa akidai amezidishiwa uzito.

"Mzani huu ni automatiki lakini yeye alitaka uzito  urudiwe kupimwa jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu ambapo hupaswa kupunguza na kulipa uliizidi na kupima tena na siyo kupima upya,"amesema Tarmo.

Ameongeza kuwa uzito unaweza kuzidi kutokana na sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na kuongeza mafuta, abiria na busta endapo zitakuwa na hitilafu ambapo hata walipofuatilia mizani nchini Zambia uzito ulikuwa na mabadiliko ikionekana kuzidi.

"Dereva baada ya kuona hizo tofauti alipaswa kuangalia mfumo wa gari lake kwani kutokana na baadhi ya changamoto kama hizo uzito unaweza kuongezeka,"amesema Tarmo.

Kwa upande wake Meneja wa Tanroads Mkoa wa Pwani Baraka Mwambage amesema kuwa kama kunatokea changamoto yoyote kuna taratibu za kufuata ili kuweza kupata haki zao na si kutumia mitandao kutoa malalamiko yao.

Mwambage amesema kuwa malalamiko yanaweza kupelekwa ofisini au kama wana wasiwasi wanaweza kupeleka kwenye vyombo vingine ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) kama sehemu ya kujua ukweli zaidi.

Hivi karibuni zilisambaa habari kupitia mitandao ya kijamii ambapo picha mjongeo ilimuonyesha dereva mmoja akilalamikia mizani ya Vigwaza kuwa imezidisha uzito.

TCRA KUSHIRIKIANA NA TBN KUSADIA KUZALISHA MAUDHUI YENYE TIJA

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeahidi kufanyakazi na Mtandao wa Wana Blogu Tanzania (TBN) pamoja na vyama vingine vya waandishi wa habari ambavyo vinawakilisha mahitaji na matakwa ya wanachama wao.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe  19 Machi 2025 Jijini Dar es Salaam na Meneja wa Huduma za Utangazaji wa TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka, alipokutana na ujumbe wa TBN ofisini kwake, katika kikao cha kujadiliana changamoto mbalimbali zinazowakabili Bloga nchini.

“Sisi huwa tunapenda kufanya kazi na vyama ambavyo vinawakilisha mahitaji na matakwa ya wanachama wao, badala ya kufanyakazi na mwaandishi mmoja mmoja…tunafurahi sana kufanyakazi na waandishi kupitia vyama vyao,” amesema Mhandisi Kisaka.

Mhandisi Kisaka amesema kuwa TCRA imefurahi kukutana na TBN kwa kuwa wanafahamu kuwa Bloga wanasehemu kubwa sana kwenye maudhui ya ndani, na hata kwenye usajili wa TCRA Bloga wanachukua nafasi kubwa sana katika maudhui ya mtandaoni.

“Kwa hiyo TBN mtakuwa silaha moja wapo nzuri sana yakutuwezesha sisi kama Mamlaka ya Mawasiliano nchini, tunao simamia utangazaji pamoja na maudhui ya mtandaoni kuwa karibu na nyinyi na kuhakikisha maudhui ya mtandaoni yanaleta tija na maendeleo kwa wananchi,” amesema Mhandisi Kisaka.

Friday, March 14, 2025

RAIS MSTAAFU DK KIKWETE AFANYA ZIARA NCHINI JAPAN KUIMARISHA USHIRIKIANO KATI YA BODI YA SHIRIKA LA ELIMU LA KIMATAIFA (GPE) NA JAPAN


Rais mstaafu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa  Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Elimu la Kimataifa (GPE), yupo Tokyo nchini Japan kwa ziara maalum yenye lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya GPE na serikali ya Japan katika kutatua changamoto za elimu ya msingi katika nchi zinazoendelea.

Katika siku yake ya kwanza Tokyo, Dkt. Kikwete amefanya mazungumzo na Waziri wa Fedha wa Japan, Mhe. Shin-ichi Yokohama, pamoja na Naibu wake, Mhe. Atsushi Mimura. 

Mazungumzo hayo yalijikita katika ushirikiano wa kifedha ili kusaidia miradi ya elimu inayosimamiwa na GPE, ikiwemo upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wa nchi zinazoendelea.

Baada ya mazungumzo hayo, Rais Mstaafu Kikwete alikutana na Bw. Akihiko Tanaka, Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA). 

Shirika hili limekuwa na mchango mkubwa katika miradi ya maendeleo barani Afrika, na mazungumzo yalihusu namna JICA inaweza kusaidia jitihada za GPE katika kukuza elimu bora.

Dkt. Kikwete pia alikutana na Bw. Yohei Sasakawa, Mwenyekiti wa Taasisi ya Nippon. Bw. Sasakawa, mwenye umri wa miaka 86, ni mtu mashuhuri wa kusaidia miradi ya kijamii duniani. 

Katika mazungumzo yao, waligusia nafasi ya sekta binafsi katika kusaidia elimu, hasa kupitia taasisi zisizo za kiserikali. Vilevile, Bw. Sasakawa alishangaza dunia baada ya kufanikisha kupanda Mlima Kilimanjaro tarehe 12 Februari 2024, kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 85 ya kuzaliwa kwake – hatua inayothibitisha kuwa umri si kikwazo kwa ndoto kubwa.

Katika siku zinazofuata, Rais Mstaafu Kikwete anatarajiwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe. T. Miyaji, pamoja na wabunge wa Bunge la Japan, ambapo ajenda kuu itakuwa nafasi ya elimu na teknolojia katika maendeleo ya jamii.

Pia, atashiriki mijadala maalum kuhusu elimu na teknolojia, kufanya mahojiano na vyombo vya habari, pamoja na kukutana na Mhe. Tetsuro Yano, Rais wa Taasisi ya AFRECO, ambayo inahusika na kukuza ushirikiano kati ya Japan na Afrika.

Ziara hii ni sehemu ya juhudi endelevu za Dkt. Kikwete katika kuboresha mifumo ya elimu duniani, hasa katika nchi zinazoendelea. 

Japan ni mshirika muhimu wa maendeleo ya elimu barani Afrika, na ushirikiano huu unaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha watoto wengi zaidi wanapata fursa ya elimu bora.

 


Thursday, March 13, 2025

KIWANDA CHA KEDS CHATOA MSAADA KWA WANAWAKE

KIWANDA cha kuzalisha sabuni cha Keds Tanzania Company Ltd cha Kibaha Mkoani Pwani kimetoa misaada ya sabuni kwa wanawake wa Mtaa wa Lulanzi ambao uko jirani na kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe ya siku ya wanawake Duniani.

Akizungumza kiwandani hapo mara baada ya kukabidhi msaada hiyo Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Bob Cheng amesema kuwa wanaungana na jamii katika kusaidia wanawake ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe hizo.

Cheng amesema kuwa wamewapatia misaada hiyo ikiwa ni sehemu ya kuenzi mchango wa wanawake ambao ni mkubwa katika kuleta maendeleo kwenye jamii.

"Kiwanda kinaungana na wanawake katika maadhimisho haya hivyo tumeona turudishe kwa jamii ikiwa ni katika ushirikiano na wananchi katika kuleta maendeleo,"amesema Cheng.

Amesema kuwa kiwanda kitaendelea kushirikiana na jamii katika masuala mbalimbali ya maendeleo hususani kwa wananchi walio jirani na kiwanda na wananchi wote kwa ujumla.

Akishukuru kwa msaada huo wa sabuni za unga na vipande Jasmini Issa amesema kuwa wanashukuru kwa msaada huo kwani utawasaidia katika matumizi ya kila siku.

Issa amesema kuwa msaada huo umeonyesha jinsi kiwanda hicho kinavyoshirikiana na jamii katika suala zima la maendeleo ambapo wamekuwa wakisaidia miradi mbalimbali inayohusu wananchi.

Naye Meri Mkwizu amesema kuwa sabuni ni muhimu sana kwa familia na ni moja ya vitu muhimu katika mahitaji kwenye familia na hutumika muda wote.

Mkwizu amesema kuwa sabuni ina bajeti kubwa kutokana na matumizi yake ikiwa ni pamoja na kufulia nguo, kuoshea vyombo, kuogea na kufanyia usafi wa aina mbalimbali ambapo jumla ya wanawake 89 walipewa msaada huo.

KEDS KUENDELEA KUZALISHA BIDHAA BORA

KIWANDA cha Keds Tanzania Company Ltd kimesema kitaendelea kuzalisha bidhaa zenye ubora na bei nafuu kulingana na hali ya soko.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mkurugenzi wa kiwanda hicho Bob Cheng alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Cheng amesema kuwa katika utengenezaji wa bidhaa zao wanazingatia ubora ili kuendelea kuwa na soko kwa kuwapatia wananchi kitu kilicho bora.

"Malengo ya kuanzishwa kiwanda ni kukuza uchumi wa wananchi kwa kutoa ajira kwa watu wengi pia kutengeneza bidhaa bora zinzokubalika,"amesema Cheng.

Amesema kuwa malengo yao ni kutengeneza bidhaa nyingine lakini kwa sasa wanafanya kwanza utafiti ili kujua ni bidhaa gani watakayoizalisha.

"Kiwanda kinajihusisha na uzalishaji wa sabuni za unga, vipande, pampasi na pedi za akinamama na kinashirikiana na serikali kwa kufuata taratibu zote za kisheria,"amesema Cheng.

Aidha amesema kuwa kiwanda kinashirikiana na jamii kwa kurudisha kwa jamii kwa kusaidia kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kwenye sekta za elimu, afya, barabara na sekta mbalimbali.

"Kuhusu maji yanayotoka kiwandani hayana athari zozote za kiafya na kimazingira ambapo hata wafanyakazi wetu wanaishi jirani na kiwanda ni asilimia 60 hivyo hayana tatizo lolote,"amesema Cheng.

Kiwanda hicho kinauza bidhaa zake kote nchini pamoja na nchi za jirani baadhi zikiwa ni Uganda, Kenya na Malawi.