Thursday, March 20, 2025

TANROADS YATOA UFAFANUZI LORI LILILOZIDISHA UZITO MIZANI YA VIGWAZA.

WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) imetoa ufafanuzi juu ya taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ya lori la mizigo lililokamatwa kwenye mizani ya Vigwaza kuwa taratibu za kulikamata lori hilo ulifuatwa.

Aidha gari hilo lilipigwa faini hiyo kwa kuzingatia sheria ya udhibiti wa uzito barabarani ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018.

Akizingumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za mizani hiyo ya Vigwaza Mtaalamu wa Kitengo cha Mizani Tanroads Makao Makuu Vicent Tarmo amesema kuwa gari hilo lilizidisha uzito zaidi ya tani moja.

Tarmo amesema kuwa gari hilo lenye namba za usajili T 137 DLR na tela namba T 567 CUR lilikuwa limetokea nchini Congo likiwa limebeba madini ya Shaba ambapo uwezo wake ni kubeba tani 48 lakini lilikutwa likiwa na uzito tani 48.1.

"Kutokana na kuzidisha uzito huo gari hilo lilitakiwa kulipiwa faini ya shilingi 900,000 ikiwa ni adhabu ya kuzidisha uzito halisi lakini dereva huyo alisema kuwa amezidishiwa uzito hivyo kupinga faini hiyo,"amesema Tarmo.

Amesema kuwa sheria inataka magari yote yenye uzito kuanzia tani 3 na nusu lazima yapime uzito ili kuepusha uharibifu wa barabara hivyo kutokana na gari hilo kuzidisha uzito alipaswa kulipa faini hiyo.

"Dereva huyo amesema kuwa amepita mizani mbalimbali uzito haukuzidi hivyo kwa nini hapa uzidi lakini kwa mujibu wa sheria alipaswa kulipa na siyo kukaidi kulipa,"amesema Tarmo.

Amesema kuwa gari hilo lilipita hapo Machi 13 ambapo kwa siku hiyo yalipimwa mwagari 819 ambapo saba yalibainika kuzidisha uzito ambapo mengine yalilipa na kuendelea safari lakini gari hilo dereva wake aligoma kulipa akidai amezidishiwa uzito.

"Mzani huu ni automatiki lakini yeye alitaka uzito  urudiwe kupimwa jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu ambapo hupaswa kupunguza na kulipa uliizidi na kupima tena na siyo kupima upya,"amesema Tarmo.

Ameongeza kuwa uzito unaweza kuzidi kutokana na sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na kuongeza mafuta, abiria na busta endapo zitakuwa na hitilafu ambapo hata walipofuatilia mizani nchini Zambia uzito ulikuwa na mabadiliko ikionekana kuzidi.

"Dereva baada ya kuona hizo tofauti alipaswa kuangalia mfumo wa gari lake kwani kutokana na baadhi ya changamoto kama hizo uzito unaweza kuongezeka,"amesema Tarmo.

Kwa upande wake Meneja wa Tanroads Mkoa wa Pwani Baraka Mwambage amesema kuwa kama kunatokea changamoto yoyote kuna taratibu za kufuata ili kuweza kupata haki zao na si kutumia mitandao kutoa malalamiko yao.

Mwambage amesema kuwa malalamiko yanaweza kupelekwa ofisini au kama wana wasiwasi wanaweza kupeleka kwenye vyombo vingine ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) kama sehemu ya kujua ukweli zaidi.

Hivi karibuni zilisambaa habari kupitia mitandao ya kijamii ambapo picha mjongeo ilimuonyesha dereva mmoja akilalamikia mizani ya Vigwaza kuwa imezidisha uzito.

No comments:

Post a Comment