Friday, March 28, 2025

VIJANA WAFUNDISHWE UMUHIMU WA MBIO ZA MWENGE

TAASISI mbalimbali nchini zimetakiwa kuwajengea uwezo vijana juu ya umuhimu wa mbio za Mwenge wa Uhuru katika kujenga uzalendo na uwajibikaji katika usimamizi wa shughuli za maendeleo na kutambua fursa za kiuchumi.

Hayo yamesemwa na Skauti Mkuu Nchini na Katibu Tawala (RAS) Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta wakati Kongamano la Vijana juu ya umuhimu wa kushiriki Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025.

Mchatta amesema kuwa vijana wanapaswa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa namna ambavyo mtaelekezwa na viongozi katika maeneo wanayoishi.

"Tukifanya hivyo tutaupata ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa ufasaha ili muweze kushuhudia kwa vitendo yale yote mtakayojifunza katika Kongamano hili,"amesema Mchatta.

Amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kundi la vijana katika kuleta mageuzi ya Kijamii na Kiuchumi kutokana na ari, nguvu na ubunifu walionao. 

"Kwa kutambua hilo serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikitoa kipaumbele kwa vijana kupata elimu na makuzi bora kuwapa fursa ya kupata mikopo ya asilimia 10 kupitia Halmashauri na Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (Build Better Tomorrow – BBT) 

Amesema kuwa Mwenge wa Uhuru Mwaka 2025 utazinduliwa mkoa wa Pwani kitendo ambacho kinaonesha nia njema ya Dk Samia Suluhu Hassani Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendeleza na kuenzi kwa vitendo yale yote aliyoturithisha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Rais wa Kwanza wa Tanzania. 

Kwa upande wake mratibu wa Kongamano hilo Omary Punzi amesema kuwa ili vijana waweze kufikia mafanikio ya kimaendeleo lazima wazingatie falsafa za Mwalimu Nyerere alizotumia wakati wa kuwashwa Mwenge wa Uhuru.

Punzi amesema moja ya falsafa za Mwenge wa Uhuru ni kuwafanya watu wawe na uzalendo kwa kujitoa kwa ajili ya nchi yao na kutokomeza maadui watatu ujinga umaskini na maradhi. 

Mbio za Mwenge wa Uhuru zitazinduliwa katika viwanja vya Shirika  la Elimu Kibaha Mkoani Pwani na Mgeni rasmi atakuwa Dk Philip Isdor Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

mwisho.


No comments:

Post a Comment