Sunday, March 30, 2025

WAZIRI MKUU MAJALIWA ARIDHISHWA MAANDALIZI UZINDUZI WA MWENGE WA UHURU PWANI 2025

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea kuangalia maandalizi ya uwanja utakaotumika kuzindua mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2025 mkoani Pwani.

Majaliwa alitembelea uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha kuangalia maandalizi ya uzinduzi huo na kuridhishwa na maandalizi hayo na kutaka wakamilishe sehemu ambazo bado hazijakamilika.

Alisema kuwa ameridhishwa na maandalizi hayo ambapo pia alitumia muda huo kutembelea watoto wa halaiki na kusema amefurahishwa na jinsi walivyokuwa na hamasa ya uzinduzi huo.

"Nawapongeza kwa maandalizi mnayoendelea nayo nimeridhishwa kamilisheni sehemu zilizosalia ili kukamilisha mapema,"alisema Majaliwa.

Alisema kuwa amefurahishwa kuona viongozi wakiwemo mawaziri na makatibu wakuu wakiwa mstari wa mbele kuhakikisha maandalizi yanakuwa mazuri.

"Alikeni hata mikoa ya jirani Dar es Salaam, Morogoro na Tanga na watu mbalimbali kwani hili ni jambo la kitaifa shirikisheni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili hamasa iwe kubwa,"alisema Majaliwa 

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete maandalizi yako vizuri ila baadhi ya maeneo ikiwemo katikati ya uwanja ndiyo kunahitaji marekebisho kidogo.

Kikwete alisema kuwa mialiko kwa wageni mbalimbali imetolewa ikiwa ni pamoja na wakuu wa mikoa, wakurugenzi na watu wengine ili kushiriki uzinduzi huo.


No comments:

Post a Comment