Thursday, March 13, 2025

KIWANDA CHA KEDS CHATOA MSAADA KWA WANAWAKE

KIWANDA cha kuzalisha sabuni cha Keds Tanzania Company Ltd cha Kibaha Mkoani Pwani kimetoa misaada ya sabuni kwa wanawake wa Mtaa wa Lulanzi ambao uko jirani na kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe ya siku ya wanawake Duniani.

Akizungumza kiwandani hapo mara baada ya kukabidhi msaada hiyo Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Bob Cheng amesema kuwa wanaungana na jamii katika kusaidia wanawake ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe hizo.

Cheng amesema kuwa wamewapatia misaada hiyo ikiwa ni sehemu ya kuenzi mchango wa wanawake ambao ni mkubwa katika kuleta maendeleo kwenye jamii.

"Kiwanda kinaungana na wanawake katika maadhimisho haya hivyo tumeona turudishe kwa jamii ikiwa ni katika ushirikiano na wananchi katika kuleta maendeleo,"amesema Cheng.

Amesema kuwa kiwanda kitaendelea kushirikiana na jamii katika masuala mbalimbali ya maendeleo hususani kwa wananchi walio jirani na kiwanda na wananchi wote kwa ujumla.

Akishukuru kwa msaada huo wa sabuni za unga na vipande Jasmini Issa amesema kuwa wanashukuru kwa msaada huo kwani utawasaidia katika matumizi ya kila siku.

Issa amesema kuwa msaada huo umeonyesha jinsi kiwanda hicho kinavyoshirikiana na jamii katika suala zima la maendeleo ambapo wamekuwa wakisaidia miradi mbalimbali inayohusu wananchi.

Naye Meri Mkwizu amesema kuwa sabuni ni muhimu sana kwa familia na ni moja ya vitu muhimu katika mahitaji kwenye familia na hutumika muda wote.

Mkwizu amesema kuwa sabuni ina bajeti kubwa kutokana na matumizi yake ikiwa ni pamoja na kufulia nguo, kuoshea vyombo, kuogea na kufanyia usafi wa aina mbalimbali ambapo jumla ya wanawake 89 walipewa msaada huo.

No comments:

Post a Comment