Monday, August 7, 2017

SIMBA WATOA MISAADA WAFANYA USAFI ZAHANATI YA MWENDAPOLE KIBAHA













Na John Gagarini, Kibaha

TAWI la Simba wilayani Kibaha limepongezwa na zahanati ya Mwendapole wilayani Kibaha kwa kujitolea zawadi kwa wagonjwa pamoja na kufanya usafi.

Hayo yalisemwa na muuguzi mganga mfawidhi wa zahanati hyo Gloria Leonidas wakati wa kuushukuru uongozi wa tawi hilo baada ya kumaliza kufanya usafi na kutoa zawadi za sabuni kwa wagonjwa.

Dk leonidas alisema kuwa vilabu vyote vinapaswa kuunga mkono kitu kilichofanywa na tawi hilo la Simba kwa kufanya shughuli za usafi na kujitolea kile walichonacho.

“Timu zinapaswa kuangalia mbali zaidi kwa kujishughulisha na kuisaidia jamii kama walivyofanya Wanasimba hawa kwani wameonyesha uzalendo wa hali ya juu,” alisema Dk Leonidas.

Alisema kuwa kusaidia sehemu kama hizo za jamii kunaleta motisha kwa watumishi wanaofanya kazi sehemu hizo za kutolea huduma inawafanya kuona kuwa wanawajali.

“Mkitusaidia kama hivi tunapata faraja hata wagonjwa nao wanajisikia vizuri kufarijiwa kama walivyofanya Wanasimba Kibaha tunaomba na klabu za hapa nazo ziige mfano huu,” alisema Dk Leonidas.

Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa tawi la Simba Kibaha Said Tisa alisema kuwa wamekuwa na utaratibu wa kujitolea kwa jamii na sehemu za kutolea huduma.

Tisa alisema kuwa wanaungana na Simba makao makuu wakati wa kuelekea tamasha la Simba Day ambalo huazimishwa kila mwaka ambapo mwaka huu linafanyika leo uwanja wa taifa.

Alisema kuwa wataendelea na utamaduni huo ili kuisaidia jamii iweze kuona faida ya timu na siyo kushiriki uwanjani pekee bali hata kuwajibika kwa jamii.


Mwisho.  
                                         



NETIBOLI PWANI WACHAGUANA


Na John Gagarini, Kibaha

CHAMA cha Netiboli mkoa wa Pwani kimefanya uchaguzi wa kuwachagua viongozi wake ambao wataongoza kwa kipindi cha miaka minne ambapo Fatuma Mgeni amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Uchaguzi huo ambao ulifanyika mjini Kibaha na kusimamiwa na kamati ya michezo ya mkoa ikiongozwa na ofisa michezo wa mkoa huo Grace Bureta ulimrudisha madarakani mwenyekiti huyo.

Wengine waliochaguliwa ni makamu mwenyekiti Faraji Makale, katibu ni Steven Mzee, katibu msaidizi ni Rehema Kiharaza, mweka hazina Octavian Chuma.
Kwa upande wa wawakilishi mkutano mkuu taifa ni Ndimbumi Ifuge, Lonjin Mzava, Omega Shuma, Witnes Kitereja na Grace Paschal.

Akiwaasa viongozi waliochaguliwa ofisa michezo huyo aliwataka viongozi hao kuwa kitu kimoja na kushirikiana ili kuinua mchezo huo kwenye mkoa kwa manufaa ya wachezaji wa mchezo huo.

Bureta alisema kuwa uongozi imara ndiyo utakaofanikisha kukabili changamoto mbalimbali zilizopo za kuuboresha mchezo huo ambao ulikuwa maarufu kwenye mkoa wa Pwani kwa miaka ya nyuma.

“Muwe na maamuzi ya pamoja na si ya mtu mmoja na kusitokee akafanya kama ni mali yake hali ambayo itasababisha mchezo huo ushindwe kupiga hatua,” alisema Bureta.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama hicho Fatuma Mgeni alisema kuwa moja ya vitu atakavyovifanyia kazi ni kufanya mafunzo kwa walimu wa mchezo huo ili wajue sheria mpya za mchezo huo ambazo zilifanyiwa marekebisho mwaka 2016 nchini Afrika Kusini.

Mgeni alisema kuwa mafunzo hayo yatakuwa kwa walimu wa mashule, vyuo na kwa wadau mbalimbali wanaoupenda mchezo huo na wanaotaka kuwa walimu wa kufundisha netiboli.


Mwisho.

Sunday, August 6, 2017

WATOTO WAFA MTO RUVU MMOJA WA MIEZI MINNE













Na John Gagarini, Chalinze

WATU watatu wakiwemo mtoto wa miezi minne na wa mwaka mmoja wamekufa huku watu wawili wakinusurika kifo baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kuzama kwenye mto Ruvu.

Akizungumza na waandishi wa habari kamanda wa polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alisema kuwa licha ya watu hao kubainika kufa dereva wa mtumbwi huo hajulikani alipo.

Shana alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 5 majira ya saa 4:00 asubuhi wakati watu hao walipokuwa wakijaribu kuvuka mto kutoka Vigwaza kwenda Mlandizi kwenye mto Ruvu wilaya ya kipolisi Chalinze.

“Ajali hiyo imepoteza maisha ya watoto wawili ambao ni Nusrat Haji miezi minne na Feisal Hamza mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu pamoja na Sikuzani Musa (41) ambaye mwili wake bado haujapatikana,” alisema Shana.

Alisema kuwa walionusurika ni Zuwena Ramadhan (29) na Tero Mziray (20) ambapo dereva wa mtumbwi huo hajulikani alipo na inaaminika hakufa maji.

“Chanzo cha mtumbwi huo kuzama bado kinachunguzwa na miili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa ndugu zao kwa ajili ya mazishi,” alisema Shana.

Aliwataka wamiliki wa vyombo hivyo kuhakikisha vinakuwa kwenye hali nzuri ili kuepukana na ajali kama hizo ambazo zinapoteza uhai wa watu kutokana na ubovu.

Mwisho.   


WAETHIOPIA 72 WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUINGIA NCHINI BILA YA KIBALI

Moja ya watu wanaotuhumiwa kuwa ni wahamiaji haramu kutoka nchi ya Ethiopia akiwahudumia wenzake kwa kuwapa mikate kwenye kituo cha Polisi wilaya ya Kipolisi ya Chalinze baada ya kukamatwa huko Ruvu Vigwaza wilayani Bagamoyo mkoani Pwani

 Moja ya watu wanaotuhumiwa kuwa ni mhamiaji haramu toka nchi ya Ethiopia akiwekewa uji pembeni ni askari akisubiri kupewa uji kwa ajili ya kuwapa watuhumiwa hao.

 Baadhi ya waethiopia wanaotuhumiwa kuingia nchini bila ya kibali wakipata kifungua kinywa cha uji.

 Askari akiwapatia mikate watu wanaotuhumiwa kuingia nchini bila ya kibali raia wa Ethiopia wakipata uji.

 Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani Jonathan Shana akiwa mbele ya watu ambao wanatuhumiwa kuwa ni wahamiaji haramu  kutoka nchi ya Ethiopia ambao walikamatwa mkoani humo.
Na John Gagarini, Chalinze

HUKU Serikali ikiwa inaweka mikakati ya kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu hapa nchini Jeshi la polisi mkoa wa Pwani limewakamata wahamiaji haramu 72 kutoka nchi ya Ethiopia kwa tuhuma za kuingia nchini bila ya kibali.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye kituo cha wilaya ya Kipolisi ya Chalinze kamanda wa polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alisema kuwa wahamiaji hao walikuwa safarini kwenda Afrika ya Kusini.

Shana alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 5 majira ya saa 3:30 asubuhi kwenye Pori la Ranchi ya Taifa (NARCO) kata ya Vigwaza wilaya ya Kipolisi ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo.

“Mbali ya wahamiaji hao haramu pia tunamshikilia Rajabu Hitaji (30) mkazi na mfanyabiashara wa Vigwaza baada ya msako mkali uliofanywa na makchero wa jeshi la polisi baada ya kupata taarifa kuwa kuna wahamiaji haramu wameingia bila ya kibali,” alisema Shana.

Alisema kuwa wahamiaji hao haramu baada ya kugundua kuwa kuna gari la polisi linawafuatilia waliingia kwenye hifadhi hiyo kwa lengo la kujificha lakini msako mkali uliofanywa uliweza kuwabaini na kukamata kundi la kwanza la watu 63 ambao walikaa sehemu ambayo gari haliwezi kufika.

“Baada ya kuwakamata wahamiaji hao haramu kundi la kwanza askari waliendelea na msako ambapo waliwakamata wahamiaji wengine tisa waliokuwa wakijaribu kutaka kutoka kwenye pori hilo,” alisema Shana.

Alisema kuwa wahamiaji hao haramu wanatarajiwa kukabidhiwa idara ya Uhamiaji kwa ajili ya hatua za kisheria pamoja na mfanyabiashara aliyekamatwa ambaye anatuhumiwa kuwasafirisha.


Mwisho.

Friday, August 4, 2017

AUWAWA NA WANANCHI WENYE HASIRA KALI KWA TUHUMA ZA WIZI


Na John Gagarini, Kibaha

JESHI la Polisi limesema kuwa bado linaendelea kumshikilia kijana wa kiume mkazi wa Mbagala Jijini Dar es Salaam ambaye alivalia mavazi ya kike ikiwemo dera hijabu na kuficha sura yake kwa kuva nikabu.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alisema kuwa kijana huyo alikamatwa Agosti 2 maeneo ya Picha ya Ndege barabara ya kuelekea Magereza huku akiwa amevaa mavazi hayo.

Shana alisema kuwa kwa sasa jeshi hilo bado linamshikilia kijana huyo kwa ajili ya mahojiano ili kubaini mtandao anaoshirikiana nao kwenye matukio ya uhalifu.

“Kijana huyu tulimkamata baada ya kumwekea mtego uliowekwa na makachero wetu waliokuwa wamepata taarifa kutoka kwa wasiri waliokuwa wanamtilia mashaka na walifanikiwa kumkamata akiwa kwenye bodaboda akielekea maeneo ya Magereza,” alisema Shana.

Alisema kuwa hadi sasa bado hawajajua kijana huyo alikuwa na lengo gani la kuvaa nguo hizo za kike hali ambayo hadi sasa bado haijafahamika hasa alidhamiria nini.

“Hadi sasa tunaendelea kumhoji kujua ni kwanini avae mavazi ya kike na tunawashukuru wananchi na wasiri wetu kwa kuendelea kutupa ushirikiano wa kufanikisha kukamatwa kwa wahalifu,” alisema Shana.


Mwisho.

KIJANA WA KIUME MVAA DERA BADO ASHIKILIWA NA POLISI


Na John Gagarini, Kibaha

JESHI la Polisi limesema kuwa bado linaendelea kumshikilia kijana wa kiume mkazi wa Mbagala Jijini Dar es Salaam ambaye alivalia mavazi ya kike ikiwemo dera hijabu na kuficha sura yake kwa kuva nikabu.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alisema kuwa kijana huyo alikamatwa Agosti 2 maeneo ya Picha ya Ndege barabara ya kuelekea Magereza huku akiwa amevaa mavazi hayo.

Shana alisema kuwa kwa sasa jeshi hilo bado linamshikilia kijana huyo kwa ajili ya mahojiano ili kubaini mtandao anaoshirikiana nao kwenye matukio ya uhalifu.

“Kijana huyu tulimkamata baada ya kumwekea mtego uliowekwa na makachero wetu waliokuwa wamepata taarifa kutoka kwa wasiri waliokuwa wanamtilia mashaka na walifanikiwa kumkamata akiwa kwenye bodaboda akielekea maeneo ya Magereza,” alisema Shana.

Alisema kuwa hadi sasa bado hawajajua kijana huyo alikuwa na lengo gani la kuvaa nguo hizo za kike hali ambayo hadi sasa bado haijafahamika hasa alidhamiria nini.

“Hadi sasa tunaendelea kumhoji kujua ni kwanini avae mavazi ya kike na tunawashukuru wananchi na wasiri wetu kwa kuendelea kutupa ushirikiano wa kufanikisha kukamatwa kwa wahalifu,” alisema Shana.


Mwisho.

Thursday, August 3, 2017

WAZIRI NCHEMBA ALIA NA WANAOWASIDIA WAHAMIAJI HARAMU





                                    Na John Gagarini, Kibaha

SERIKALI imesema imefika wakati kuwakamata watu wanaowasaidia kuwalipia faini wanazopigwa wahamiaji haramu mara wanapohukumiwa mahakamani.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba alipotembelea ofisi za Uhamiaji mkoa wa Pwani na kusema kuwa watu hao ndiyo wanaosababisha kuendelea kuingia kinyume cha sheria wahamiaji haramu.

Nchemba alisema kuwa nchi imekuwa ikiingia gharama kubwa kuwatunza wahamiaji haramu wanapoingia nchini na nchi kutumia muda mwingi kuhangaika na wahamiaji hao.

“Hii ni mipango kwani wameshafanya biashara hii kama halali na kuona kuwa hata wakiwalipia adhabu za fedha zinazotolewa na mahakama na kufanya wahamiaji hawa kuingia mara kwa mara hivyo wanaokuja kuwalipia nao kamateni, magari wanayosafirishia wahamiaji haramu taifisheni na boti wanazotumia kamateni,” alisema Nchemba.

Alisema inashangaza kuona Watanzania eti wanawalipia faini wanazopigwa kama adhabu baada ya kubainika kuingia nchini bila ya kibali jambo hilo halikubaliki.

“Hii ni biashara ambayo kuna baadhi ya wenzetu wanajihusisha nayo ndiyo maana tatizo hili haliishi na pia kuna baadhi ya watumishi wa serikali nao wanahusika na tutawachukulia hatua kali watakaobainika kushiriki kwenye mtandao huu wa kuwaingiza wahamiaji haramu,” alisema Nchemba.

Aidha alisema kuwa nchi haiwezi kutumia fedha ambazo zingetumika kwa ajili ya kununulia dawa za wagonjwa mahospitalini, kujenga barabara, kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu na fedha hizo kuzipeleka kuwahudumia wahamiaji haramu jambo hilo hatutakubali liendelee.

Awali Ofisa Uhamiaji mkoa Plasid Mazengo alisema kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni upungufu wa vitendea kazi ikiwa ni pamoja usafiri na boti kwa ajili ya kudhibiti wahamiaji haramu ambao wamekuwa wakitumia bandari ya Bagamoyo ambayo ina vipenyo vingi vya kuingilia nchini.

Mazengo alisema kuwa changamoto nyingine ni ukosefu wa wakalimani kwa ajili ya kutafsiri lugha za Kihabeshi na upungufu wa watumishi kwenye baadhi ya wilaya.

Mwisho.