Na John Gagarini, Kibaha
WATU wasiofahamika wamevunja vioo vya madisrisha na kupaka kinyesi kwenye ya ofisi ya kata ya Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani na kusababisha watumishi wa kata hiyo kushindwa kuingia ofisini mwishoni mwa wiki.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisa mtendaji wa kata ya Maili Moja Thadeo Mtae alisema alipofika ofisni majira ya saa moja asubuhi Juni 17 alikuta ofisi hiyo imepakazwa vinyesi vya binadamu na vioo vya madirisha ya vioo nane kuvunjwa kwa kupigwa mawe na watu hao.
Mtae alisema inadhaniwa kuwa kitendo hicho kimefanywa na baadhi ya watu waliovunjiwa nyumba zao ambao walikuwa na hasira ya kuvunjiwa nyumba zao na Halmashauri ya Mji wa Kibaha na kudai kuwa ofisi hiyo haikuwasaidia lolote.
“Eneo hilo lipo chini ya halmashauri ya Mji hivyo wananchi hao walikuwa wamevamia na kuishi hapo kinyume na sheria hawa wananchi walipoona wamevunjiwa nyumba zao wakaanza kulalamika kwanini ofisi yangu haiwasaidii,kiukweli wapo kinyume na taratibu tusingeweza kuwaunga mkono kwa hilo”alisema Mtae.
Aidha alisema kuwa baada ya kuona hali ile walikwenda kutoa taarifa kwenye ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha na polisi juu ya tukio hilo ambapo hadi sasa haijaweza kufahamika nani aliyetekeleza uharibifu huo.
“Tumeshatoa taarifa polisi na mlinzi Richard Maduhu anahojiwa polisi kuhusiana na tukio hilo kwani wakati tukio hilo linatokea hakuweza kutoa taarifa sehemu yoyote hadi wao walipofika ofisini hapo,” alisema Mtae.
Naye diwani wa kata ya Maili Moja Ramadhan Lutambi alisema kuwa kitendo hicho si cha kiungwana kwani hata kama wananchi hao walikuwa na madai yao ni vema wakafuata taratibu kuliko kuharibu ofisi ambayo inatoa huduma kwa wananchi.
Lutambi alisema kuwa suala hilo tayari wamelipeleka polisi ili kufuatilia kujua nani aliyefanya hivyo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake kwani hali hiyo ina hatarisha hali ya usalama wa watendaji wa ofisi ya kata ambapo kwa siku hiyo hawakuweza kufanya kazi kutokana na tukio hilo.
Mwisho.
|
|
Show details
|
Saturday, June 18, 2016
WAVUNJUA VIOO VYA MADIRISHA WAPAKA KINYESI OFISI YA KATA
BOMOABOMOA YALIZA WENGI KIBAHA
Na John Gagarini, Kibaha
ZOEZI la bomoabomoa kwenye eneo ambalo Halmashauri ya Mji wa Kibaha linadai kuwa wananchi hao walijenga kinyume cha taratibu limewaacha wakazi 55 kwenye Mtaa wa Machinjioni, kata ya Mailmoja Kibaha mkoani Pwani wakiwa hawana mahali pa kuishi baada ya kutekeleza zoezi hilo.
Wakazi hao wakizungumzia bomoa bomoa hiyo akiwemo Said Tekelo, Sauda Lameck na Ally Saidi walisema bomoa bomoa hiyo imewaathiri kwa kiasi kikubwa kwani hawana pa kuishi,kuhifadhiwa kwa majirani na jamaa na wengine kuamua kwenda kuishi kwenye nyumba za kupanga .
Walisema kuwa kitendo walichofanyiwa ni kimewaumiza kutokana na kuwarudisha nyuma kimaendeleo huku wengine waliovunjiwa nyumba zao wamejikuta wakiibiwa baadhi ya vitu vyao na watu wasio wema.
“Tulipewa taarifa ya tukio hilo ilishatolewa mapema ambapo tulienda mahakamani kukata rufaa lakini tunashangaa kuona greda limeletwa na kuanza kubomoa nyumba zetu kabla ya shauri la mwisho,” Walisema.
Kwa upande wake ofisa habari wa halmashauri ya Mji wa Kibaha,Innocent Byarugaba alisema zoezi la bomoa boma limefanyika kwa siku mbili kuanzia june 15 na june 16.
Byarugaba alisema zoezi limefanyika kwa kufuata taratibu kwani kuanzia tarehe 31 may wakazi hao wote walipewa hati za kuwataka wabomoe wenyewe na kila mmoja katika nyuma zote 55 alipatiwa hati hiyo kwa jina lake.
Byarugaba alisema baada ya siku 16 walivunja nyumba hizo ambapo kisheria unapompa mtu hati ya kuvunja nyumba yake mwenyewe na badala yake kumvunjia kisheria ya mipango miji kifungu 74 kifungu kidogo cha 4,na sheria ya serikali za mitaa kifungu cha 139 kifungu kidogo cha 3 anatakiwa kulipia hizo gharama.
Alisema eneo hilo lilimilikishwa watau watano ambapo mwaka 2009 walitakiwa kuondoka na kulipwa fidia zao na kuanzia hapo watu wengine wasio waaminifu waliwauzia wengine kinyume na tararibu.
Eneo hilo lilipimwa kihalali kama eneo la viwanda na watu watano walimilikishwa ambapo mwaka 2006 miliki ya viwanja hivyo ilifutwa kwa tangazo la serikali ili kupisha uendelezaji wa kitovu cha Mji na ujenzi wa soko .
Mwisho. |
MIGOGORO YA NDOA ISIWANYIME HAKI ZA MSINGI WATOTO
Na John Gagarini, Bagamoyo
WAZAZI na walezi wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wametakiwa kutowanyima haki za msingi ikiwa ni pamoja na elimu watoto wao kutokana na migogoro yao ya ndoa.
Hayo yalisemwa na mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo Abdul Sharifu wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika kwenye wilaya hiyo yaliyofanyika shule ya Msingi Mwanamakuka Bagamoyo.
Sharifu alisema kuwa ugomvi baina ya wazazi imekuwa ikisababisha watoto wengi kukosa haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na elimu hali ambayo imesababisha wakose maadili mazuri.
“Kutokana na migogoro ya kifamilia au ndoa imekuwa ikisababisha watoto wengi kukosa elimu ambayo ndiyo urithi pekee ambao anaweza kurithishwa mtoto na si mali ambazo zinaweza kwisha lakini elimu ni urithi wa kudumu,” alisema Sharifu.
Alisema kuwa mbali ya changamoto ya watoto kukosa elimu pia watoto wa kike hujikuta wakipata mimba za utotoni ambazo ni hatari kwa masiha yao kutokana na maumbile yao.
“Tunataka mashirika yasiyo ya kiserikali na serikali kuwachukua wale wote wanaobainika kuwapa mimba lazima hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa kufuata mkondo wake ili kukomesha tabia hiyo mbaya,” alisema Sharifu.
Aidha alisema kuwa watoto wenye ulemavu wa viungo na walemavu wengine wana haki kama wengine hivyo jamii isiwanyanyapae ni lazima haki zao zitazamwe na kuwashirikisha katika mikutano mbalimbali na shughuli za kijamii ili kuibua vipaji vyao viweze kuwasaidia kuacha vitendo vya kuwaajiri watoto. Kwa upande wake mkurugenzi wa Kaya Fm, Marie Shaba alisema katika bara la Afrika, Kusini, Mashariki, mitaa, kwenye familia watoto walio wengi hawaishi kwa raha na wanakosa haki zao ambapo sherehe hizo zinapaswa kuwakumbusha kwa yaliyotokea nchini Afrika ya Kusini huko Soweto ambapo watoto 700 walifariki kwa kudai haki zao.
Kwa upande wa watoto akiwemo Fatuma Sadik, kutoka shule ya msingi Mbaruku alisema kufiwa na wazazi pia husababisha baadhi ya watoto kufukuzwa na ndugu na jamaa kwa tamaa za mali zilizoachwa na wazazi.
Alisema suala hilo husababisha watoto kukosa haki zao msingi za kuishi kwa amani na upendo na kwa mtazamo wa haraka hiyo si migogoro bali ni vita, machafuko na ukosefu wa amani na haki za msingi dhidi ya watoto na aliiomba jamii ilinde haki zao na kuzifanyia kazi kisheria ikiwemo haki ya kupata elimu, kulindwa, kusikilizwa na kupendwa pasipo kubaguliwa. Mwisho |
Tuesday, June 14, 2016
WATATU WASHIKILIWA KWA MAUAJI YA DEREVA WA NOAH
Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani
linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya dereva wa gari la abiria
aina ya Toyota Noah Mohamed Ramadhan (21) mkazi wa Mlandizi wilayani Kibaha
mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa
habari ofisini kwake mjini Kibaha kamanda wa Polisi mkoani humo Bonaventura
Mushongi alisema kuwa watu hao walimkodisha dereva huyo.
Mushongi alisema kuwa tukio
hilo lilitokea Juni 13 mwaka huu majira ya saa 19:45 usiku eneo la Vigwaza
Tarafa ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo.
“Watu hao walimuua dereva huyo
kwa kumkaba shingoni kisha kupora gari hilo lenye namba za usajili T 119 DDM
rangi nyeupe lililokuwa likitumiwa na marehemu baada ya kumkodi wakimataka
awapeleke Kanisa la Pentekoste Vigwaza,” alisema Mushongi.
Alisema kuwa watu hao kabla ya
kumuua marehemu walimkaba wakiwa njiani ambapo alipiga kelele kuomba msaada na
madereva bodaboda walizisikia na kuamua kufuatilia gari hilo barabara ya vumbi
kwenye njia kuu ya umeme wa Tanesco.
“Watu wale walipoona taa za
bodaboda waliamua kusimama na kutoka ndani ya gari na kuanza kukimbia kutokomea
porini lakini mmoja wao alikamatwa palepale na walipoangalia ndani walikuta mwili
wa marehemu ukiwa umewekwa kiti cha nyuma kwa lengo la kwenda kuutupa mwili huo
porini ili kuondoka na gari hilo,” alisema Mushongi.
Aidha alisema kuwa juhudi za
wananchi, dereva bodaboda na polisi zilifanikisha kukamatwa watuhumiwa wawili
ambao majina ya watuhumiwa hao yamehifadhiwa ili kutoharibu upelelezi kwani
watu hao ni mtandao wa majambazi ambao wengine wako Jijini Dar es Salaam.
Alibainisha kuwa mwili wa
marehemu umehifadhiwa kwenye hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Tumbi kusubiri ndugu
na uchunguzi wa daktari kwa ajili ya mazishi.
Aliwataka madereva wa vyombo
vya moto hasa wale wanaofanya biashara za usafirishaji nyakati za usiku kuwa
makini ili kujiepusha na matukio kama hayo ya wizi.
Mwisho.
Thursday, June 9, 2016
RC ATAKA MKATABA WA UWEKEZAJI KUPITIWA UPYA
Na John Gagarini, Mafia
MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo ametaka
kupitiwa upya mkataba wa kuuziwa mwekezaji eneo la Magofu ya Chole wilaya ya
Mafia mkoani Pwani ambapo kampuni ya Chole Mjini Conservation and Development
Ltd imemilikishwa ambapo eneo hilo kuna gereza walilokuwa wanafungwa watumwa
enzi za ukoloni wakati wa Utawala wa Wajerumani.
Aidha ameunda tume ya kufuatilia undani wa mkataba huo na
amezuia marekebisho yaliyokuwa yanafanywa na kampuni hiyo kwa kipindi cha mwezi
mmoja hadi pale ufumbuzi wa kujua namna mkataba huo ulivyoingiwa baina ya Kijiji
cha Chole na mwekezaji huyo kama umezingatia taratibu.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Chole Mjini kata ya
Jibondo kwenye mkutano wa hadhara Ndikilo alisema kuwa mkoa hauna nia mbaya na
mwekezaji huyo ambaye amepewa hati miliki ya eneo hilo kwa kipindi cha miaka 33.
Ndikilo alisema kuwa eneo hilo ambalo lina kumbukumbu
mbalimbali ambalo liko jirani na Bahari ya Hindi lilikuwa likitumika kwa ajili
ya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na soko la Watumwa pamoja na gereza lina
ukubwa wa hekta 3.7 ambapo eneo hilo liko chini ya Wizara ya maliasili na
Utalii Idara ya Malikale.
“Mkataba huo ambao ulisainiwa mwaka 2007 shamba namba 2031 baina
ya mwekezaji Dk Jean de Villiers na Kijiji
hicho ambapo mwenyekiti wa Kijiji hicho Maburuki Sadiki alisaini kwa niaba ya
Kijiji na kushuhudiwa na mkuu wa wilaya wakati ule Manzie Mangochi pasipo
kuishirikisha Halmashauri ya wilaya ambayo haipati mapato yoyote kutokana na
uwekezaji huo licha ya kutoa huduma za kijamii kwa wakazi wa Kijiji cha Chole”
alisema Ndikilo.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo amemtaka mwekezaji huyo
kusimamisha ukarabati na kuunda tume ya kufanya uchunguzi na itatoa majibu
baada ya mwezi mmoja ili kujiridhisha na kumilikishwa eneo hilo mtu binafsi
eneo la serikali la kihistoria na kujengwa hoteli ya kitalii kwa kukarabati
jengo la zamani.
Alibainisha kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii ilituma barua
ambayo iliyosainiwa na John Kimaro kwa niaba ya katibu mkuu kwa Halmashauri ya
Wilaya ya Mafia kuhirikiana na mwekezaji na kusema kuwa sheria ya Mambo ya Kale
ya mwaka 1964 na marekebisho yake ya mwaka 1979 na sera ya Malikale ya mwaka
2008 inasema Malikale au Magofu yanaweza kumilikiwa na mtu binafs, taasisi na
serikali.
Barua hiyo inaendelea kusema kuwa jukumu la serikali (Idara
ya Mambo ya Kale) ni kuhakikisha kuwa mmiliki hatabomoa au kufanya chochote
katika magofu hayo kinyume cha sheria.
Akitoa maelezo juu ya umiliki wake mkurugenzi wa Chole Mjini
Conservation and Development Company Ltd Anne De Villiers amesema kuwa kampuni
hiyo iliingia Mafia na kukuta hali ya majengo hayo ya kale yakiwa kwenye hali
mbaya ndipo walianza mchakato wa kuyakarabati.
Dk Villiers alisema kuwa lengo la kuchukua eneo hilo ni
kuhakikisha uasili wa mahali hapo haupotei kwa kuyafanyia ukarabati magofu hayo
ambapo moja lilibaki ukuta mmoja na kutumia fedha nyingi kwa ajili ya ukarabati
huo.
Naye mkuu wa wilaya ya Mafia Dk Nasoro Hamid alisema kuwa
serikali haishirikishwi jambo lolote wala haijui ni watalii wangapi wanaoingia
hapo wala mapato yanayopatikana kwenye eneo hilo.
Dk Hamid amesema kuwa Kijiji cha Chole ndicho kiliingia
mkataba na mwekezaji huyo ambapo hugawana asilimia kutokana na watalii
wanaoingia kwenye eneo hilo la makumbusho lakini tatizo haijulikani
kinachopatikana hapo ni kiasi gani katika mgawanyo huo wa mapato.
Awali baadhi ya wanakijiji wakizungumzia suala hilo wakiongozwa
na Ally Sikubali na Hemed Ally walisema kuwa moja ya changamoto iliyokuwepo ni
mkataba Kiswahili unasema kuwa endapo kutakuwa na kutoeleweka mkataba wa
Kiingereza ndiyo utakaotumika.
Waliomba mkataba huo uangaliwe upya na kufanya marekebisho
ili kila upande unufaike kwani kwa sasa inaonekana kuwa pande nyingine
hazinufaiki na mkataba huo.
Mwisho.
WATAKA TAARIFA KUHUSU ENEO LA UWEKEZAJI BAADA YA MRADI WA MIWA KUFUTWA
Na John Gagarini, Bagamoyo
HALMASHAURI ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani imetakiwa
kutoa taarifa rasmi kwenye vijiji vilivyokuwa kwenye mradi wa kilimo cha miwa
chini ya kampuni ya Eco Energy uliosimamishwa na serikali ili eneo hilo lisije
kuchukuliwa na mtu mwingine ili hali wananchi hao hawajalipwa fidia.
Mradi huo ulisimamishwa kupitia majibu ya Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa akiwa anajibu swali la kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni Freeman
Mbowe aliyetaka kujua ni kwanini serikali imeshindwa kuweka jitihada za
makusudi ili mradi huo ukamilike ambao ulibainika kuwa ungetumia maji mengi ya
Mto Wami na kuathiri usatawi wa wanyama kwenye Mbuga ya Saadani.
Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Bagamoyo katibu wa
kamati ya ardhi ya Asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Mkombozi Bakari Salum
alisema kuwa kwa kuwa kauli ya Waziri
Mkuu ni agizo ni vema Halmashauri ingetoa tangazo rasmi kwa wananchi husika.
“Kwa kuwa wakati anakuja mwekezaji kuchukua maeneo ya
wananchi kwa ajili ya mradi huo kulikuwa na taarifa rasmi na wananchi walitoa
maeneo yao kwa ajili ya kilimo hicho cha miwa ambacho baadaye kungejengwa
kiwanda kwa ajili ya kuzalisha sukari hivyo baada ya kushindikana
wangewajulisha wananchi,” alisema Salum
Kwa upande wake mjumbe wa kamati hiyo Jackson Mkango alisema
kuwa eneo ambalo lilichukuliwa na mwekezaji ni hekari zaidi ya hekta 22,000
wananchi hao hawajalipwa fidia yoyote licha ya kuwa tathmini kufanyika mwaka
2011 hadi leo hawajalipwa.
Mkango alisema kuwa sheria inasema kuwa tathmini ikifanyika
walengwa wanapaswa kulipwa ndani ya kipindi cha miezi sita lakini sasa imepita
miaka mitano sasa.
“Tunaiomba Halmashauri kutoa tamko juu ya ardhi hiyo ya
wananchi ambayo toka imechukuliwa wananchi hawakufanya chochote licha ya kuwa
eneo hilo walikuwa wakitegemea kwa ajili ya kilimo na hawajui hatma yao kwani
walitegemea wangelipwa fidia,” alisema Mkango.
Vijiji vilivyokuwa kwenye mpango huo ni Razaba, Matipwili,
Kitame, Fukayosi, Makaani na Gongo ambapo kuna jumla ya wananchi zaidi ya 700
ambao walikuwa wakiishi kwenye maeneo hayo yaliyoingizwa kwenye mradi huo ambao
ulikuwa na lengo la kukabiliana na upungufu wa sukari hapa nchini.
Mwisho.
WAWEKEZAJI WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUDUMISHA AMANI YA NCHI
Na John Gagarini, Mafia
MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amewataka
wawekezaji kwenye Visiwa vilivyopo Wilayani Mafia kushirikiana na serikali ili
kudhibiti usalama wa nchi kukabiliana na wageni wasio waaminifu ambao wanaoweza
kuvitumia visiwa hivyo kuhatarisha amani ya nchi.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati kamati ya Ulinzi na
Usalama ya mkoa ilipotembelea Kisiwa cha Shungimbili kwenye Hoteli ya Thanda
ambayo inamilikiwa na raia wa kigeni na kusema kuwa kuna haja ya kuwa na kituo
cha kufuatilia wageni wanaoingia na kutoka.
Ndikilo alisema kuwa kutokana na hali ya sasa kuwa mbaya
kiusalama kutokana na matukio ya mauaji ya kutisha ambayo yanatokea hapa nchini
ni vema ulinzi ukaimarishwa.
“Kuna haja ya kuwa na ushirikiano na baina ya wawekezaji na
serfikali ili kukabiliana na wahalifu ambao wanaweza kutumia visiwa kujiingiza
hapa nchini na kufanya uhalifu ikiwa ni pamoja na mauaji,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa dunia ya sasa imebadilika na baadhi ya watu
wamekuwa wakitumia njia ya Bahari kupitisha wahamiaji haramu, dawa za kulevya
pamoja na uingizwaji wa silaha.
“Serikali haina nia mbaya ya kutaka kujua mambo yanayofanywa
na wawekezaji kwa kujua wageni wanaoingia na kutoka na wameleta nini wanatoka
na nini na hapa kutakuwa na kituo cha ukaguzi ambacho kitakuwa na polisi kwa
ajili ya kulinda eneo la Kisiwa kwani wageni watakuwa wanafika kwa wingi,”
alisema Ndikilo
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Thanda Island Tanzania
Ltd Oscar Pucci alisema kuwa hana tatizo na ushirikiano na serikali kwani
anashirikiana vizuri na Halmashauri.
Pucci alisema kuwa wamekuwa wakisaidia shughuli za maendeleo
kama kuchangia kwenye Hospitali ya wilaya na hata wavuvi wanaovua jirani na
hoteli yao.
Mwisho.
Subscribe to:
Comments (Atom)
