Na John Gagarini, Kibaha
WATU wasiofahamika wamevunja vioo vya madisrisha na kupaka kinyesi kwenye ya ofisi ya kata ya Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani na kusababisha watumishi wa kata hiyo kushindwa kuingia ofisini mwishoni mwa wiki.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisa mtendaji wa kata ya Maili Moja Thadeo Mtae alisema alipofika ofisni majira ya saa moja asubuhi Juni 17 alikuta ofisi hiyo imepakazwa vinyesi vya binadamu na vioo vya madirisha ya vioo nane kuvunjwa kwa kupigwa mawe na watu hao.
Mtae alisema inadhaniwa kuwa kitendo hicho kimefanywa na baadhi ya watu waliovunjiwa nyumba zao ambao walikuwa na hasira ya kuvunjiwa nyumba zao na Halmashauri ya Mji wa Kibaha na kudai kuwa ofisi hiyo haikuwasaidia lolote.
“Eneo hilo lipo chini ya halmashauri ya Mji hivyo wananchi hao walikuwa wamevamia na kuishi hapo kinyume na sheria hawa wananchi walipoona wamevunjiwa nyumba zao wakaanza kulalamika kwanini ofisi yangu haiwasaidii,kiukweli wapo kinyume na taratibu tusingeweza kuwaunga mkono kwa hilo”alisema Mtae.
Aidha alisema kuwa baada ya kuona hali ile walikwenda kutoa taarifa kwenye ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha na polisi juu ya tukio hilo ambapo hadi sasa haijaweza kufahamika nani aliyetekeleza uharibifu huo.
“Tumeshatoa taarifa polisi na mlinzi Richard Maduhu anahojiwa polisi kuhusiana na tukio hilo kwani wakati tukio hilo linatokea hakuweza kutoa taarifa sehemu yoyote hadi wao walipofika ofisini hapo,” alisema Mtae.
Naye diwani wa kata ya Maili Moja Ramadhan Lutambi alisema kuwa kitendo hicho si cha kiungwana kwani hata kama wananchi hao walikuwa na madai yao ni vema wakafuata taratibu kuliko kuharibu ofisi ambayo inatoa huduma kwa wananchi.
Lutambi alisema kuwa suala hilo tayari wamelipeleka polisi ili kufuatilia kujua nani aliyefanya hivyo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake kwani hali hiyo ina hatarisha hali ya usalama wa watendaji wa ofisi ya kata ambapo kwa siku hiyo hawakuweza kufanya kazi kutokana na tukio hilo.
Mwisho.
|
Show details
|
Saturday, June 18, 2016
WAVUNJUA VIOO VYA MADIRISHA WAPAKA KINYESI OFISI YA KATA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment