Na John Gagarini, Kibaha
SHIRIKA la
Kuendeleza Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO)
kwa kushirikiana na wafadhili wake limetumia kiasi cha dola milioni mbili za
Kimarekani kwa ajili ya kutoa mafunzo ya uzalishaji bidha za vyakula zisizo na
madhara kwa wajasiriamali zaidi ya 700.
Mratibu wa mafunzo
hayo Happines Mchomvu alisema kuwa mafunzo hayo ambayo yametolewa kwa kipindi
cha miaka miwili kwa lengo la kuhakikisha bidhaa wanazozalisha zinakuwa hazina
madhara kwa watumiaji zinakuwa na usalama.
Mchomvu alisema
kuwa mbali ya kuwa na usalama pia zinakuwa na viwango vya wa ubora wa kimataifa
ili viweze kuuzwa sehemu yoyote ile duniani.
“Mafunzo hayo
yalikuwa na malengo ya kuboresha bidhaa za maembe, viungo na asali ambapo wameweza
kuwajengea uwezo wajasiriamali hao kutoka mikoa ya Tabora, Singida, Shinyanga,
Morogoro, Pwani na Dar es Salaam,” alisema Mchomvu.
Aidha alisema
lengo ni kuhakikisha wajasiriamali kote nchini kuanzia ngazi ya mikoa hadi
kwenye mitaa wanazalisha bidhaa zenye ubora na viwango kwa lengo la kuwa na
soko la uhakikka la ndani na nje ya nchi ambapo bidhaa za Tanzania zinapendwa
kutokana na uhalisia wake.
Kwa upande
wake ofisa udhibiti wa ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Magdalena
Sademaki alisema kuwa kupitia mafunzo hayo wajasiriamali hao wameweza
kutengeneza mifumo yao kimataifa kwa kupambana na vihatarishi ili visiweze
kuingia kwenye vyakula.
Sademaki alisema
kuwa katika kuhakikisha wajasiriamali hao wanatengeneza bidhaa zenye viwango
wanashirikiana na SIDO kuwatambua ili waweze kufikia viwango vya uzalishaji wa
bidhaa bora ili ziendane na viwango vya kimataifa.
Na mmoja wa
wajasiriamli ambaye amehudhuria mafunzo hayo Zaloki Mohamed ameishukuru SIDO kwa
kuwapatia elimu juu ya viwango vya bidhaa wanazozalisha kwa
kuzingatia utaratibu wa viwango vya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika
la Viwango Tanzania (TBS) na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO).
Mohamed ameiomba serikali iwapunguzie tozo zinazotozwa
kwa wajasiriamali ili wapate hati ya viwango ya bidhaa wanazozalisha na kuweza
kufikia malengo ya Tanzania ya kuwa na viwanda.
Mafunzo hayo
yameendeshwa kwa ufadhili wa Shirika la Biashara la Kimataifa (ITC) kupitia
mpango wa kuendesha biashara wa shirika la World Trade Organisation (WTO) kwa
kushirikiana na SIDO.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment