Na John Gagarini, Bagamoyo
HALMASHAURI ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani imetakiwa
kutoa taarifa rasmi kwenye vijiji vilivyokuwa kwenye mradi wa kilimo cha miwa
chini ya kampuni ya Eco Energy uliosimamishwa na serikali ili eneo hilo lisije
kuchukuliwa na mtu mwingine ili hali wananchi hao hawajalipwa fidia.
Mradi huo ulisimamishwa kupitia majibu ya Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa akiwa anajibu swali la kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni Freeman
Mbowe aliyetaka kujua ni kwanini serikali imeshindwa kuweka jitihada za
makusudi ili mradi huo ukamilike ambao ulibainika kuwa ungetumia maji mengi ya
Mto Wami na kuathiri usatawi wa wanyama kwenye Mbuga ya Saadani.
Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Bagamoyo katibu wa
kamati ya ardhi ya Asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Mkombozi Bakari Salum
alisema kuwa kwa kuwa kauli ya Waziri
Mkuu ni agizo ni vema Halmashauri ingetoa tangazo rasmi kwa wananchi husika.
“Kwa kuwa wakati anakuja mwekezaji kuchukua maeneo ya
wananchi kwa ajili ya mradi huo kulikuwa na taarifa rasmi na wananchi walitoa
maeneo yao kwa ajili ya kilimo hicho cha miwa ambacho baadaye kungejengwa
kiwanda kwa ajili ya kuzalisha sukari hivyo baada ya kushindikana
wangewajulisha wananchi,” alisema Salum
Kwa upande wake mjumbe wa kamati hiyo Jackson Mkango alisema
kuwa eneo ambalo lilichukuliwa na mwekezaji ni hekari zaidi ya hekta 22,000
wananchi hao hawajalipwa fidia yoyote licha ya kuwa tathmini kufanyika mwaka
2011 hadi leo hawajalipwa.
Mkango alisema kuwa sheria inasema kuwa tathmini ikifanyika
walengwa wanapaswa kulipwa ndani ya kipindi cha miezi sita lakini sasa imepita
miaka mitano sasa.
“Tunaiomba Halmashauri kutoa tamko juu ya ardhi hiyo ya
wananchi ambayo toka imechukuliwa wananchi hawakufanya chochote licha ya kuwa
eneo hilo walikuwa wakitegemea kwa ajili ya kilimo na hawajui hatma yao kwani
walitegemea wangelipwa fidia,” alisema Mkango.
Vijiji vilivyokuwa kwenye mpango huo ni Razaba, Matipwili,
Kitame, Fukayosi, Makaani na Gongo ambapo kuna jumla ya wananchi zaidi ya 700
ambao walikuwa wakiishi kwenye maeneo hayo yaliyoingizwa kwenye mradi huo ambao
ulikuwa na lengo la kukabiliana na upungufu wa sukari hapa nchini.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment